Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Bonabucha: Nilipigwa ngumi nikacheua nyama

BONABUCHA Pict

Muktasari:

  • Makundi hayo yalizalisha vijana wengi hodari akiwemo msanii wa Bongo Fleva, Msami aliyeimba Step by Step na ule wa Mabaya, huku mwingine akiwa Papaa Msai ambao wote kwa sasa wanaishi kupitia kuimba na kucheza muziki.

MIAKA ya 2000 mwanzoni, vijana wa mitaa ya Temeke, Dar es Salaam walisumbua katika makundi ya kudansi kwenye matamasha waliyokuwa wakiyaandaa kupitia makundi. Ukweli pesa ilitembea siyo kitoto na makundi hayo makubwa kwa Temeke yalikuwa Umangani na Best Friend ambayo yalikuwa na upinzani mkali wa kucheza nyimbo tofauti.

Makundi hayo yalizalisha vijana wengi hodari akiwemo msanii wa Bongo Fleva, Msami aliyeimba Step by Step na ule wa Mabaya, huku mwingine akiwa Papaa Msai ambao wote kwa sasa wanaishi kupitia kuimba na kucheza muziki.

Lakini usilolijua kuwa kijana wa Kurasini ambaye serikali inayatambua majina yake kama George Costantine Mbonabucha, ila katika mchezo wa ngumi akitambulika kwa jina la George Bonabucha ni mmoja kati ya vijana waliokuwa madansa katika makundi hayo.

Licha ya kuwa alikuwa anapenda kucheza muziki kupitia makundi hayo, lakini bado ulikuwa humuelezi chochote kuhusu mchezo wa ngumi ambao alianza kuucheza tangu akiwa anasoma darasa la sita katika Shule ya Msingi Kurasini.

BONA 01

Bonabucha ambaye kwa sasa ni askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ’) ni kati ya mabondia wa jeshi hilo waliopotea kabisa katika anga za ngumi za kulipwa kutokana na muda mrefu kutopanda ulingoni.

Kwa sasa bondia huyo siyo dansa tena, bali ni askari wa JWTZ mwenye cheo cha koplo ambapo rekodi yake inaonyesha amecheza jumla ya mapambano manane.

Katika mapambano hayo ameshinda saba kati ya hayo mawili kwa knockout na amepigwa mara moja kwa pointi nchini Kenya dhidi ya Albert Kimario 2023, na tangu apoteze pambano hilo Bonabucha hakuwahi kurejea ulingoni mpaka sasa.

BONA 02

Mwanaspoti limefanya mahojiano na bondia huyo ambaye anajiandaa na pambano litakalofanyika Morocco, Mei 12, mwaka huu, ambapo amefichua mambo mengi makubwa aliyokutana nayo kwenye mchezo wa ngumi.

“Unajua ngumi nimeanza kitambo tangu nilipokuwa mwanafunzi. Nilikuwa nacheza muziki, lakini bado najishughulisha na mchezo wa ngumi japo sikuwa nafahamu kama ipo siku nitapata ajira kupitia ngumi, nilikuwa nacheza ngumi kutokana na mazingira ya mtaani ukiwa mnyonge huwezi kupata pesa. Hali hiyo ilifanya wengi kucheza ngumi.

BONA 03

SWALI: Uliwezaje kucheza ngumi na kudansi kwa wakati mmoja?

JIBU: “Unajua wakati ule vijana wadogo tunadansi ilikuwa ni wakati wa TID ameachia ngoma yake ya Zeze. Kutokana na wimbo huo kupendwa basi vijana wengi tuliingia kwenye kudansi.

“Lakini haikuweza kunifanya nisipende au kuichukia ngumi kwa sababu asilimia 90 ya watu mtaani kwetu walikuwa wanacheza ngumi wakati ule na usipocheza kila mtu atakuonea.

“Binafsi sikuwa napenda unyonge ndiyo maana nilikuwa na kina Muki wa Makomandoo, Msami ambao wote tumekimbiza sana kwenye hayo mambo.

“Upande wangu mtu ambaye aliniingiza kwenye ngumi za ushindani kuna kocha anaitwa Serenge yeye yupo JKT pale Mgulani aliniona na kugundua kipaji changu.

“Nakumbuka alinichukua na kunipeleka kambini na kuanza kufundishwa namna ngumi za ushindani zinavyokuwa, baadaye nikapata nafasi ya kuandikishwa jeshini kupitia mchezo huu wa ngumi.

BONA 04

SWALI: Pambano gani kwako lilikuwa gumu?

JIBU:”Katika ngumi za kulipwa awali sikuwa najua zinataka nini maana nakumbuka nilitishwa na wakati huo Fadhili Majiha ameshinda ubingwa Uingereza, nikawa naongea naye kwa simu ya video akanimbia ninayecheza naye ni bondia mzuri kutoka Bagamoyo.

“Kiukweli ilinipa hofu kubwa kwa sababu vitisho hivyo havikutoka kwa Majiha peke yake maana akaingia na Ibrahim Class ambaye aliniambia huyu mtoto ana nguvu na alishawahi kumpiga Loren Japhet.

“Licha ya kuambiwa hayo maneno lakini bado nilipokuwa naangalia rekodi yake nilikuwa naona ni bondia wa kawaida, nashukuru Mungu nilifanikiwa kumpiga pale katika Uwanja wa Kinesi na ndiyo lilikuwa pambano langu la kwanza.


SWALI: Uliwahi kupigwa ngumi ambayo huwezi kusahau kwenye maisha yako?

JIBU: “Daah! Nakumbuka kuna pambano moja nilicheza China katika mashindano ya majeshi ya dunia ‘Cism’, nilicheza na bondia kutoka Uzbekistan, jina lake limenitoka lakini yule bondia sitaweza kuja kumsahau.

“Nakumbuka alinipiga ngumi ya tumbo halafu kabla ya pambano kwenye mlo wangu nilikula nyama, basi huwezi amini kwa ngumi ya tumbo aliyonipiga yule jamaa hadi nikacheua.

“Nyama zikaja hadi mdomoni kwenye ‘gam sheet’ pambano lilivyoanza jamaa alinidharau lakini ikawa tofauti kwa sababu kuna wakati naye alinihofia.

BONA 05

SWALI: Hivi kwa nini huwa unavaa kitenge ukiingia ulingoni?

JIBU: “Hahahahaha! Nadhani ule ni mtindo ambao nimeuchagua kwenye maisha yangu ya ngumi katika kila pambano napanda nikiwa nimevaa kitenge lakini pia ili watu wanitambue kirahisi.


SWALI: Ulishawahi kukutana na   mambo ya ushirikina kwenye mapambano yako?

JIBU: “Kiukweli sijawahi kuamini hata siku moja ndiyo maana hata mimi huwa wakati wa kupigana ulingoni napanda nikiwa nimevalia rozali na kitenge kwa sababu siamini ushirikina.


SWALI: Baada ya kupigwa Kenya mwaka 2023 umepotea, nini shida?

JIBU: “Nimekuwa kimya ni jambo la kweli, nakumbuka ile mechi nilipoteza kwa pointi na wewe ulikuwepo (mwandishi). Kila mtu aliona lile pambano mazingira yalivyokuwa, baada ya pale sijawahi kupata pambano lolote licha ya kuwa napigiwa simu nyingi lakini kwenye maslahi hatufikii muafaka kabisa.

“Lakini natamani hata kesho nipate pambano nipigane, kazi yangu ni kupigana kwa hiyo siwezi kukataa pambano nafanya mazoezi lakini bado sijapata pambano.

“Nimekaa muda mrefu, mashabiki wanatamani kuniona tena ulingoni akitokea bondia yeyote nitapigana naye kwa sababu ni kazi yangu.

“Unajua mimi ndiyo bondia pekee ambaye naweza kuburudisha nikiwa napigana labda mwingine anaweza kuwa Mfaume Mfaume, hivyo mapromota walete kazi waone mambo yanavyokuwa.


SWALI: Unadhani mabondia gani wa Bongo wakikutana pambano litakuwa kali?

JIBU: “Kwa upande wangu kama itakuja kutokea pambano kati ya Ismail Galiatano na Loren Japhet kiukweli hapo moto utawaka kwa sababu wote ni mafundi wa ngumi kweli.”