Kiungo Singida agomea mamilioni

Muktasari:
- Chukwu alisaini mkataba wa miaka mitatu na timu hiyo, huku akiwa amezitumikia klabu tatu tofauti hadi sasa kote alikwenda kwa mkopo.
SINGIDA Black Stars imeanza harakati za mapema za kumuongeza mkataba mpya, kiungo Morice Chukwu, huku Mnigeria huyo akiwagomea mabosi hao, licha ya kuahidiwa donge nono.
Chukwu alisaini mkataba wa miaka mitatu na timu hiyo, huku akiwa amezitumikia klabu tatu tofauti hadi sasa kote alikwenda kwa mkopo.
Mnigeria huyo alianzia Singida Black Stars, kisha akapelekwa Singida Fountain Gate (Ihefu) msimu uliopita kabla ya msimu huu kuichezea Tabora United, kabla ya kurudishwa Singida BS.
Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti kuwa Mnigeria huyo amechomoa kuongeza mkataba mpya akiwa katika meza ya mazungumzo.
“Mabosi wa klabu wamemuwekea mamilioni ila jamaa (Chukwu) amekataa kwa sababu anataka kumaliza mkataba wa awali kwanza. Huenda anataka kuchezea timu nyingine nje na Singida, kwani hakupata muda wa utulivu, kutokana na kuhamishwa mara kwa mara.”
Akizungumza na Mwanaspoti, Chukwu alisema ni kweli mabosi wake wametaka aongeze mkataba ila hakukubaliana nao kwa sababu zake binafsi.
“Walinitaka niongeze mkataba wa miaka miwili, ila ni kweli nimekataa, kwa vile nataka kupata changamoto mpya nimeshaijua Singida sio timu mbaya,” alisema nyota huyo wa zamani wa Rivers United ya Nigeria aliyeongeza;
“Nataka kupata changamoto mpya misimu niliyoichezea hii ligi nimejifunza mengi, kwa sababu nimekuwa na timu tofauti na kote nimefurahia.”
Morice amefunga mabao manne ndani ya misimu hii miwili, huku akifunga moja kwa Fountain na Singida na mawili kwa Tabora.
Singida kama itamaliza katika nafasi iliyopo kwa sasa, msimu ujao itarudia rekodi yake ya kucheza michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Timu hiyo inashika nafasi ya nne ikiwa imecheza mechi 27 na kufikisha pointi 53, ikiweka rekodi ya kushinda michezo 16, sare tano na kupoteza sita.
MECHI ZILIZOSALIA
Mei 27 : Simba vs Singida Black Stars
Juni 18: Dodoma Jiji vs Singida Black Stars
Juni 22: Singida Blacks Stars vs Tanzania Prisons