Prime
Percy Tau mezani Yanga

Muktasari:
- Yanga imemuuza Aziz KI kwenda Wydad Casablanca ya Morocco na tayari nyota huyo ameondoka akiiacha timu hiyo ikimalizia Ligi Kuu Bara na fainali ya Kombe la FA.
DAU la kuvutia walilopata baada ya kuondoka kwa Stephane Aziz KI Yanga, kumeifanya klabu hiyo mapema kuingia sokoni kumsaka mbadala wake ambapo hadi sasa ina majina ya wachezaji wawili walio kwenye hatua nzuri ya kumalizana nao.
Yanga imemuuza Aziz KI kwenda Wydad Casablanca ya Morocco na tayari nyota huyo ameondoka akiiacha timu hiyo ikimalizia Ligi Kuu Bara na fainali ya Kombe la FA.
Katika kumpata mrithi sahihi wa Aziz KI, Yanga ipo kwenye mazungumzo na uongozi unaomsimamia winga wa zamani wa Al Ahly ya Misri, Percy Tau raia wa Afrika Kusini.
Tau ambaye kwa sasa anaichezea Qatar SC aliyojiunga nayo Januari mwaka huu akitokea Ahly, inaelezwa hafurahishwi na maisha ya huko inapopatikana klabu hiyo yenye makazi yake jijini Doha.
Uamuzi wa Yanga kuanza mazungumzo ya kumsajili Tau, ni uhitaji wao wa mchezaji ambaye atakuwa na uwezo mkubwa na kuisaidia timu kama ilivyokuwa kwa Aziz KI.
Taarifa za ndani kutoka Yanga zinasema kuwa, wakati uongozi ukipambana na ishu ya Tau, wameweka chaguo la pili kwa Gibril Sillah raia wa Gambia anayemaliza mkataba ndani ya Azam ambayo haina mpango wa kumuongezea. “Tunapambana kwanza na Tau kama tukifanikiwa itakuwa safi, lakini kama itashindikana tutarudi kwenye chaguo la pili, unajua Tau ana uzoefu mkubwa ingawa tunapambana na klabu nyingi kama tatu hivi,” kilisema chanzo hicho.
UHAMISHO WA TAU
Wakati Tau mwenye umri wa miaka 31 akitoka Al Ahly na kutua Qatar, Waarabu hao walitoa kiasi cha euro 155,000 (sawa na Sh475.8 milioni) ambacho Yanga kwa sasa ina jeuri ya kukitoa kwani ina mkwanja mrefu wa Sh2 bilioni zilizotokana na mauzo ya Aziz KI.
Tau ambaye amewahi kucheza Ligi Kuu England akiitumikia Brighton, mkataba wake na Qatar unafikia tamati Juni 30, mwaka huu, hivyo Yanga inaweza kumsajili akiwa mchezaj Cairo International Stadium i huru.
Nyota huyo ambaye kiasili ni winga akicheza zote mbili kulia na kushoto, pia ana uwezo wa kucheza eneo la mshambuliaji wa kati, nafasi ambazo Aziz KI pia anazimudu. Kumbuka wote wanatumia mguu wa kushoto.
KUHUSU SILLAH
Kama Tau ishu yake itakuwa ngumu, basi Yanga haitapoteza muda itamalizana na Sillah, ambaye alishapewa mkataba aupitie kabla ya kusaini na kuitumikia timu hiyo.
Sillah raia wa Gambia, ndiye chaguo la pili kwa Yanga endapo ikimkosa Tau, lakini klabu hiyo inamuangalia winga huyo kwa jicho la tatu ikiamini kwa wale wanaocheza ndani ya Ligi Kuu Bara hivi sasa, ndiye mtu sahihi kwao.
Msimu huu Sillah amefanya vizuri zaidi kwenye ligi akifunga mabao tisa na asisti mbili akiwa ndiye kinara wa ufungaji kikosini hapo akifuatiwa na Nassoro Saadun mwenye mabao manane. Msimu uliopita winga huyo alimaliza na mabao manane.
“Kwa sasa Sillah ndio chaguo la pili kabla ya kuja kwa jina la Tau, lakini awali ndiye alikuwa chaguo la kwanza, hivyo kama Tau itakuwa ngumu kumpata basi tutamalizana na Sillah kwa kuwa tayari mkataba tulishampa,” kilibainisha chanzo hicho.
Sillah nafasi yake halisi uwanjani ni winga akicheza kushoto na kulia, lakini pia ana uwezo wa kucheza kama kiungo mshambuliaji anayetokea katikati akitumia mguu wa kushoto. Habari kutoka ndani ya Azam zinasema kwamba uwezekano wa Sillah kuongezewa mkataba mpya ni mdogo kwani sehemu kubwa ya uongozi unaamini kwamba ameshindwa kuibeba timu hiyo kimataifa.