Prime
Yanga yamleta Dar beki wa Mazembe

Muktasari:
- Yanga imeamua kumuita beki huyo Dar ili kufanya mazungumzo ya mwisho kabla ya kumpa mkataba wa kukiwasha katika kikosi hicho, ikielezwa ataziba pengo la Yao Kouassi ambaye kwa sasa ni majeruhi na mmoja ya wachezaji waliokosekana uwanjani kwa muda mrefu.
BEKI wa TP Mazembe ya DR Congo, Ibrahim Keita yupo njiani kuja jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kufanya mazungumzo na mabosi wa Yanga inayompigia hesabu kumsajili kwa kikosi cha msimu ujao.
Yanga imeamua kumuita beki huyo Dar ili kufanya mazungumzo ya mwisho kabla ya kumpa mkataba wa kukiwasha katika kikosi hicho, ikielezwa ataziba pengo la Yao Kouassi ambaye kwa sasa ni majeruhi na mmoja ya wachezaji waliokosekana uwanjani kwa muda mrefu.
Keita ambaye ameichezea Mazembe ndani ya misimu mitatu, mkataba wake kwa sasa upo ukingoni na klabu ya hiyo.
Mwanaspoti ilizungumza na mtu wa karibu na beki huyo ambapo alisema, Keita yuko katika hatua za mwisho na Yanga huku akifuchua mwezi ujao hautamalizika atakuwa amekuja Tanzania.
"Makubaliano yao ni kuja huko Juni 12 ili kuonana na mabosi wa Yanga kwa ajili ya kukamilisha mazungumzo yao na inavyoonekana kila kitu kiko vyema," alisema mtu huyo.
Keita aliwahi kuzungumza na Mwanaspoti akisema: "Ni kweli nimefanya mazungumzo na Yanga, lakini bado hatujafikia makubaliano, nilikiona kikosi chao katika michuano ya kimataifa, ni timu nzuri.
"Kwa sasa namalizia mkataba wangu, lakini misimu mitatu ni mingi kucheza timu moja, mipango yangu ni kutafuta changamoto mpya."
YAO AMPA TIKETI
Majeraha ya Yao Kouassi, ndio yamempa tiketi Keita kutua Yanga, kwani mabosi wa klabu hiyo walishindwa kumalizana na beki huyo mapema ili kusikilizia.
Yao amefanyiwa upasuaji huo wiki mbili zilizopita kwenye goti lake la mguu wa kushoto, baada ya awali kupona jeraha la kifundo cha mguu na nyama za paja.
Taarifa za ndani kutoka Yanga zililiambia Mwanaspoti kuwa: "Yao kwa kweli maisha yake msimu huu wa pili hayakuwa mazuri, kama unavyosema amekumbana na janga la majeraha, hivi karibuni tuliona kama amepona, lakini ghafla amerejea tena kwenye majeraha na sidhani kama tutamuona uwanjani hata msimu ujao ukianza.
"Ilikuwa tumalizane na yeye, lakini isingekuwa majeraha bado kwetu ni mchezaji bora sana, tunaangalia namna ya kumuongeza mkataba ila atakuwa nje mpaka atakapokuwa sawa."
NAFASI
Kwa sasa ndani ya Yanga nafasi ya beki wa kulia anacheza Kibwana Shomari na Israel Mwenda, hivyo kama Keita atatua msimu ujao kutakuwa na kazi ya ziada kupata namba katika kikosi cha kwanza.
Wakati Yao akiwa timamu, alikuwa akimkalisha nje Kibwana kabla ya Mwenda kusajiliwa dirisha dogo msimu huu akitokea Singida Black Stars baada ya kuondoka Simba.