Prime
Mambo matano yaliyotenganisha fainali za Simba, Yanga CAF

Muktasari:
- Ilianza Yanga kucheza fainali ya michuano hiyo msimu wa 2022-2023 na kupoteza ubingwa kwa kanuni ya bao la ugenini dhidi ya USM Alger ya Algeria kufuatia matokeo ya jumla kuwa 2-2. Mechi ya kwanza nyumbani Yanga ilifungwa 2-1, ugenini ikashinda 1-0.
YANGA na Simba zinaendelea kuwa kwenye vitabu vya kumbukumbu za soka la Tanzania kwamba ndiyo timu zilizocheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Ilianza Yanga kucheza fainali ya michuano hiyo msimu wa 2022-2023 na kupoteza ubingwa kwa kanuni ya bao la ugenini dhidi ya USM Alger ya Algeria kufuatia matokeo ya jumla kuwa 2-2. Mechi ya kwanza nyumbani Yanga ilifungwa 2-1, ugenini ikashinda 1-0.
Kwa upande wa Simba, imecheza fainali msimu huu 2024-2025 dhidi ya RS Berkane ya Morocco, ikiwa imepita misimu miwili tu tangu Yanga ifanye hivyo. Simba imepoteza fainali kwa jumla ya mabao 3-1, mechi ya kwanza ugenini nchini Morocco ilifungwa 2-0, nyumbani ikatoka sare ya 1-1.
MECHI ZAO
Wakati Simba ikimaliza katika nafasi ya pili kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, safari yake nzima katika michuano hiyo imecheza mechi 14 kuanzia hatua ya pili hadi fainali, ikishinda saba, sare nne na kupoteza tatu. Yanga nayo ilicheza mechi kwa idadi hiyo ikishinda tisa, sare tatu na kupoteza mbili. Msimu huo Yanga ilianzia Ligi ya Mabingwa Afrika, baadaye ikaangukia Shirikisho tofauti na Simba iliyoanzia moja kwa moja Shirikisho.
Kwa kiasi fulani, timu hizo zimefanana matokeo ya hatua za mwanzoni kwani zote mechi za kwanza katika mtoano zilitoka 0-0, zikaja kushinda marudiano na kufuzu makundi.
Hatua ya makundi, zote zilimaliza kileleni kwa kukusanya pointi sawa ambazo ni 13 zilitokana na kushinda mechi nne, sare moja na kupoteza moja.

YANGA UGENINI, SIMBA NYUMBANI
Katika mechi hizo 14 kila moja, takwimu zinaonyesha Yanga na Simba zimegawana sehemu za kutamba. Yanga ilifanya vizuri mechi za ugenini ikishinda tano wakati nyumbani ilishinda 4.
Simba ilifanya vizuri nyumbani kwa kushinda mechi sita, hali ikawa mbaya ugenini ikishinda moja tu.
DIARRA, CAMARA NGOMA DROO
Hapa Simba imepigwa bao na Yanga kwani imeambulia clean sheet sita ikimtumia kipa mmoja pekee kwenye michuano hiyo ambaye ni Moussa Camara, wakati Yanga iliyokusanya clean sheet saba, ikiwatumia Djigui Diarra na Metacha Mnata. Diarra alimaliza na clean sheet sita, Metacha moja.
Kitendo cha Diarra na Camara kukusanya clean sheet sita kila mmoja, maana yake wametoka ngoma droo ingawa Diarra alicheza mechi chache ambazo ni 13, Camara 14.
USHAMBULIAJI / ULINZI
Hapa pia Yanga ilifanya vizuri kuliko Simba. Takwimu zinaonyesha kwamba Simba katika mechi 14 ilizocheza, imefunga mabao 15 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 10, huku Yanga ikifunga 18 na kuruhusu saba.

Katika mabao 15 ya Simba, kinara wake ni Kibu Denis aliyefunga manne, akifuatiwa na Leonel Ateba na Jean Charles Ahoua ambao kila mmoja alipachika matatu. Wengine ni Edwin Balua (1), Mohamed Hussein (1), Elie Mpanzu (1), Steven Mukwala (1) na Joshua Mutale (1).
Kwa upande wa Yanga, mabao 18 yaliyofungwa, saba yalitoka kwa Fiston Mayele ambaye aliibuka mfungaji bora wa michuano hiyo. Mengine yalifungwa na Kennedy Musonda (3), Stephane Aziz Ki (2), Mudathir Yahya (1), Tuisila Kisinda (1), Jesus Moloko (1), Farid Mussa (1), Bernard Morrison (1) na Djuma Shaban (1).
VINARA WA MABAO
Msimu huu 2024-2025, kinara wa mabao wa Kombe la Shirikisho ni Oussama Lamlioui wa RS Berkane aliyefunga matano sawa na Ismail Belkacemi wa USM Alger. Lamlioui ametwaa tuzo hiyo kufuatia kuwa na mchango wa kubeba ubingwa wakati Balkacemi akiishia robo fainali.
Msimu wa 2022-23, mfungaji bora alikuwa Fiston Mayele aliyefunga mabao saba.
KUNA KITU NDANI YAKE
Ukiweka kando takwimu hizo za kila mmoja, upande mwingine kwa kile ilichofanya Simba na Yanga ndani ya misimu mitatu ya karibuni kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika, inaonekana soka la Tanzania linazidi kupiga hatua huku ikibaki hatua chache kubeba ubingwa.

Kocha wa zamani na aliyekuwa nyota wa Simba, Abdallah ‘King’ Kibadeni amesema kwa sasa soka la Tanzania limekua ukilinganisha na wakati wao walipokuwa wakicheza.
“Zamani ilikuwa ni ndoto kucheza mechi za kimataifa na kufika hatua kubwa kama ya fainali, lakini kwa sasa imekuwa sio tatizo tena.
“Kwa sasa Simba na Yanga zinawazia kuwa mabingwa kwani hatua zote walishavuka na kinachotakiwa ni kushinda kabisa ili kuweka heshima.
“Kitendo cha Simba kushindwa kubeba ubingwa msimu huu ni kama historia imejirudia japo maumivu ni makubwa, nimeumia sana nikakumbuka fainali za kipindi hicho, kama wamenitonesha kidonda.”
Staa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Zamoyoni Mogella, amesema: “Klabu zinazopata nafasi za kucheza michuano ya CAF zinatakiwa kusajili wachezaji wenye uwezo mkubwa wa kuamua matokeo, hicho ndicho kilichoiangusha Simba.
“Mfano mchezaji wa RS Berkane aliyesawazisha bao alijitoa, kwa mchezaji mvivu asingefunga katika eneo lile.
“Simba na Yanga zikijiandaa kulingana na ukubwa wa michuano hiyo kwa msimu ujao, mojawapo itanyakua taji, zisiwe na wachezaji wababaifu.”

Mchezaji mwingine wa zamani wa Yanga, Willy Mtendamema, amesema: “Timu zisajili wachezaji wenye viwango vya kimataifa watakaokuwa na uwezo wa kuamua matokeo, mfano wa kina Fiston Mayele, Simba walikuwapo kina Meddie Kagere, Luis Miquissone, kiukweli soka linahitaji uwekezaji, maana wachezaji wenye viwango vikubwa lazima timu ziingie gharama.”