Prime
Fei Toto kwa Aziz KI sawa, ila tusubiri tuone!

Muktasari:
- Na kama mchezaji kwa leo viongozi hawapati kazi kubwa kumshawishi kusajiliwa kwa sababu kuna lundo la mifano kuhusu wachezaji waliotumia daraja hilo kuwavusha na msimu huu tu ameondoka Stephane Aziz Ki.
LIGI yetu ya soka inaendelea kukua na kuvutia wachezaji mbalimbali wenye uwezo mkubwa, wakiamini inaweza kuwa daraja zuri la kuwavusha kwenda katika mafanikio ya maisha.
Na kama mchezaji kwa leo viongozi hawapati kazi kubwa kumshawishi kusajiliwa kwa sababu kuna lundo la mifano kuhusu wachezaji waliotumia daraja hilo kuwavusha na msimu huu tu ameondoka Stephane Aziz Ki.
Huyu ni Mfungaji Bora mwingine wa Ligi Kuu Bara aliyeondoka baada ya George Mpole enzi akiichezea Geita Gold na Fiston Mayele aliyekuwa Yanga. Mpole alienda FC Lupopo ya DR Congo na Mayele anayekipiga kwa sasa Pyramids ya Misri.

Aziz Ki ameondoka Yanga kwenda Wydad Casa-blanca ya Morocco na kwa sasa mabosi wa Jangwani wanataka kutafuta mbadala wake na wanahu-sishwa na kums-hawishi aliyewahi kuwa mch-ezaji wao ambae sasa anahudumu kwenye viunga vya Chamazi, Feisal Salum Abdalah ‘Fei Toto’, huku watani wao Simba nao wakihusishwa na jitihada za kumshawishi atue Msimbazi.
Yes...Feisal Salum anaonekana kama mbadala sahihi kwa Aziz KI kutokana na kile anachoweza kuongeza kwa timu ndani ya kiwanja.
Ni kweli Feisal hawezi kuwa Aziz Ki, ila anaweza kutimiza majukumu ya kimchezo kwa ubora unaohitajika. Faida ya ziada ya Feisal ni matumizi kulingana na muundo wa timu kwa mechi husika, kwani ni kiungo aliyekamilika.

Anaweza kutumika kama kiungo mbunifu eneo la nyuma ya mshambuliaji kama msimu huu anavyocheza pale Azam na akakupatia idadi nzuri ya utengenezaji wa mabao na kufunga.
Kwa sasa Fei Toto ndiye kinara wa asisti akiwa nazo 13, wakati msimu uliopita alicheza kama kiungo mshambuliaji na namba tisa bandia na kumaliza na mabao 19 na asisti saba nyuma ya Aziz Ki aliyefunga mabao 21 na asisti nane katika Ligi Kuu Bara.
Fei Toto pia anaweza kutumika kama mshambuliaji akiwa amefichwa kwenye kiungo (false 9) kama alivyocheza msimu uliopita na kuwa mfungaji namba mbili.

Pia anaweza kutumika kama kiungo wa kuzuia timu ikihitaji kuwa na viungo wawili wa kuzuia, ni kiungo aliyekamilika anaweza kutumika kwa namna yoyote kulingana na mipango ya benchi la ufundi ndio maana sishangai kuhusishwa na watani wa jadi kutoka Kariakoo kila mmoja akihakikisha msimu ujao anakuwa mshindani ndani na Afrika kwa ujumla.
Ila niseme wazi tu, sitoshangaa pia ikiwa atavuka mipaka kwenda kucheza nje kutokana na uwezo alionao.
Ikiwa Yanga itafanikisha itakuwa imefanikiwa kupata mbadala wa Aziz KI kwa daraja lile lile na itawaimarisha kuendea msimu ujao kama kiwango alichonacho kitaendelea kuwepo sababu kiwango hupanda na kushuka ndani ya muda mfupi.

Simba katika ile safari ya kujenga timu itakuwa imeongeza nyenzo muhimu kwenye ujenzi na itamuongezea kocha Fadlu Davids upana wa machaguo eneo la kiungo ambalo ndilo muhimili wa timu.
Faida nyingine, klabu zote zitapata ni kusajili mzawa kwa daraja ambalo ingewalazimu kutumia zile nafasi kumi na mbili za wageni, japo wengine wameanza kuzikwepa kanuni kwa kuwabadilisha uraia, japo hili halipaswi kufumbiwa macho kwani ni uhuni wa kupora nafasi za wazawa.
Hatma ya msimu ujao kwa Feisal ataenda wapi? Azam nayo tayari ina uhakika wa nafasi moja kati ya mbili za uwakilishi kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika hivyo kama inataka kushindana ni lazima kuhakikisha inawabakisha kikosini wachezaji wake bora na kujazia maeneo yenye uhitaji baada ya kutokuwa na msimu mzuri ukilinganisha na mwenendo wa msimu uliopita.

Mchezaji bado ana mkataba na Azam, hivyo klabu hiyo ndio yenye nafasi nzuri ya kumtumia msimu ujao japo historia inaonyesha kuna biashara zimefanyika baina ya Azam na Simba kuliko Yanga na hata ikifanyika huwa ina misukosuko.
Azam kama ina nia ya dhati ya kushindana inapaswa kuacha kuwa malisho ya washindani wake kwa kuwabakiza wachezaji wake bora ili iweze kushindana msimu ujao katika Ligi ya ndani na michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwani ukiitazama michuano hiyo inaonekana kama ndio saizi yetu kwa sasa timu za Tanzania, hivyo Azam ina deni walau kufikia hatua ya makundi.

Matarajio yangu ni kumuona Feisal akicheza michuano ya klabu barani Afrika, ni timu gani? Tuupe muda nafasi yake.