Barka aanza maisha mapya Barcelona

KAMA ambavyo ilikuwa kwa mshambuliaji kinda wa Kitanzania, Kelvin John kuanza maisha yake ya soka kwenye kituo cha Brooke House FA huko Uingereza kwa ajili ya kuzoea maisha ya Ulaya kabla ya kutua KRC Genk ndivyo ambavyo inaweza kuwa kwa Barka Seif ambaye amejiunga na MARCET Football University ambayo alipita Ansu Fati akiwa mdogo kabla ya kuibukia Barcelona.
Julai mosi, 2021 baada ya kuonekana ameiva, Kelvin alijiunga rasmi na KRC Genk ya Ubelgiji ambayo ilionyesha kumhitaji angali akiwa na miaka 17 ambapo alikuwa akifanya vizuri na kikosi cha vijana cha timu ya taifa ‘Serengeti Boys’.
Akiwa na Brooke House FA, Kelvin alitajwa kuwa mmoja wa makinda ambayo yanaweza kufanya makubwa miaka ijayo, ni kama nyota njema alianza kuwaka mapema na hatimaye kwa sasa licha ya kuwa na miaka 19 anapambania namba kwenye kikosi cha kwanza cha KRC Genk akiwa na nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta.
Inawezekana Barka licha ya kuwa na umri mdogo zaidi kuliko Kelvin wakati akiingia Ulaya akafuata nyayo za mshambuliaji huyo.
Kwanini? Wiki chache zilizopita Barka alikuwa Uholanzi ambako alienda kwa mara ya pili kwa ajili ya kliniki kwenye klabu ya Ajax ambayo imetoa wachezaji wengi wakubwa ambao kwa sasa wanafanya vizuri Ulaya, akiwa huko yametoka maelekezo ambapo anatakiwa kuanzia MARCET Football University.
MARCET Football University ikoje tutalitazama hilo baadaye. Nje ya Bongo ilifanya mawasiliano na baba wa kijana huyo, Seif Mpanda na hapa anaeleza kuwa tayari mwanaye ameanza maisha mapya nchini Hispania kwenye chuo hicho.
“Kwanza kabisa shukrani kubwa ziende kwa wote ambao wamekuwa sehemu ya mchakato huu kuanzia pale ambapo kijana wangu alipata nafasi ya kwanza kwenda Uholanzi hadi ya pili na sehemu nyingine ambazo na zenyewe tulialikwa.
“Kilikuwa kipindi kizuri ambacho tumejifunza mambo mengi kila sehemu ambayo tulienda. Kwa sasa kijana wangu atakuwa Hispania kwenye chuo cha MARCET Football University, atakuwa hapo akipata elimu ya mpira na kawaida.
“Ilikuwa ngumu kwa sababu bado kijana ni mdogo lakini imebidi nipambane kuhakikisha wepesi unapatikana, tumefuata kila taratibu ambazo zinahitajika na hatimaye zimekamilika hivyo anaweza kurejea nyumbani Tanzania kwa ajili ya kusalimia,” anasema mzazi huyo wa Barka.
Kwa upande wake Barka anasema anajisikia furaha kupata nafasi ya kujiunga na MARCET Football University na anaamini ataendelea kujifunza mambo mengi kwenye chuo hicho. ”Ndoto yangu ni kuwa mchezaji mkubwa kwa miaka ya baadaye, naamini kwenye kujifunza. Nitaendeleza nidhamu ambayo nimekuwa nayo kwenye kila jambo maana nimekuwa nikielezwa kuwa ni msingi wa kila kitu,” anasema Barka.
Twende sawa kuhusu Marcet ni nani huyo?Anaunda Chuo Kikuu cha kwanza ambacho huendeleza mpira wa miguu pekee. Uzoefu wa miaka mingi na uchunguzi ulisababisha, kwa kawaida, kuwa kituo cha kipekee cha elimu ambacho kinaweka Kandanda kwenye kiwango sawa na eneo jingine lolote la kijamii na kuinua kama nafasi ya kukuza taaluma kamili na ya kuridhisha.
Kwa hivyo Chuo Kikuu hiki sio tu kinatayarisha wakufunzi, makocha, wataalamu wa fiziotherapi, wachambuzi na wanasheria, bali pia na wataalamu wengine wanaohusishwa na mpira wa miguu. Mashirikisho na taasisi za mafunzo kutoka kote duniani pia hushirikiana na Marcet ili wanafunzi wao wapate ubora na ufaulu.
Soka ya Akili na Teknolojia
Marcet anaweka akili katikati ya maendeleo ya soka. Kipaji, muda mzuri, bahati nzuri au bidii ni muhimu ikiwa inasimamiwa kwa akili ndani na nje ya uwanja.
Kwa hivyo, taasisi hii imekubali teknolojia mpya kama kipengele muhimu na tofauti katika mipango yote. Data na maarifa ambayo hutoa huruhusu Marcet Lab kufikia maarifa ambayo yanawezesha kutafakari upya elimu ya soka na uundaji wa taasisi kuelekea mifumo na mbinu bora.
Teknolojia mpya pia huwaruhusu wanafunzi na wachangiaji kufikia mafanikio ya mtu binafsi yanayonufaisha pamoja.
Sifa iliyothibitishwa
Ufanisi wa Marcet unathibitishwa na orodha ndefu ya wanafunzi waliofaulu ambao wamefikia wasomi wa ulimwengu wa soka. Wataalamu wa kila aina katika mabara yote wamekuwa mabalozi wa falsafa ya Marcet na kuchangia leo katika maendeleo chanya ya soka na jamii popote pale walipo.
Luis Llopis, kocha wa makipa wa Real Madrid; Carlos Lozano, physiotherapist wa Shanghai Shenhua; Miquel Coldecarrera, akiwa Girona FC; Sebastián Galles, kocha wa pili wa Club Universitario de Chile; Germán Vargas, katika Deportivo Saprissa; Tommy N’Kono, kocha wa makipa wa RCD Español; Guillermo Hoyos, mmoja wa makocha wa thamani zaidi Amerika… Hii ni mifano michache tu ya wanafunzi waliofaulu wa Marcet.
Ushirikiano
Kando na kesi za kibinafsi, Chuo Kikuu hiki pia hushirikiana mara kwa mara na taasisi mbalimbali duniani, pamoja na shule za michezo, vituo vya elimu.
Mashirikisho ya soka kutoka nchi kama vile Peru, Ukraine, Korea Kaskazini, India, Malta au Lebanon yamewasiliana na Marcet katika miaka ya hivi karibuni ili kuzindua mipango mipya, kubadilisha mpango wao wa elimu au kuunganisha miradi iliyopo.