Mambo matano ziara ya Barka Hispania

YULE kijana wa Kitanzania ambaye alijipatia umaarufu mkubwa nchini baada ya kufanya vizuri huko Uholanzi kwenye klabu ya Ajax, Barka Mpanda amekwea pipa na kwenda Hispania kwa ajili ya kushiriki programu maalum za zaidi ya wiki mbili zenye lengo la kuendeleza kipaji chake.
Mwishoni mwa mwaka jana Barka alikuwa Amsterdam, Uholanzi kwenye kliniki za miamba ya soka nchini humo, Ajax kwa vijana wadogo na kufanya vizuri kiasi cha kutwaa tuzo zaidi ya tatu, ikiwemo kuwa mchezaji bora wa walioalikwa mwaka huo.
Kituo cha kulea vipaji cha Valencia SPF ndicho kilichomtumia mualiko Barka kwenda Hispania ambako amefuatana na baba yake, Seif Mpanda.
Akiwa Hispania Barka, amesherehekea kutimiza miaka minane (8), na Mwanaspoti ilizungumza kwa dakika 30 na Barka moja kwa moja kutokea Hispania hadi Tanzania kwa njia ya mtandao na kujua kila kinachoendelea nchini humo.
Leo, Jumatatu kwenye safu hii, tunakuletea mambo matano ambayo yametokea huko Hispania, miongoni mwayo ni pamoja na kipaji cha Barka kuwashangaza wenyeji wao kiasi cha kumfananisha na aliyekuwa supastaa wa Barcelona, Lionel Messi, alivyokuwa udogoni wakati akiibuka.
AKUTANA NA KAKA ZAKE
Kwa mara nyingine tena, Barka alipata nafasi ya kukutana na kaka zake wa damu, Tariq na Jabir ambao wapo Hispania kwenye kituo hicho cha Valencia SPF.
“Nimefurahi kukutana na kaka zangu na jambo zuri ni kwamba nimewakuta wakiendelea vizuri, ni muda mrefu sijaonana nao,” anasema Barka.
Baba yake na Barka, Seif anasema: “Kuja kwangu Hispania mbali na kumleta Barka kwa program alizonazo nililenga kuja kuwaona watoto wangu, Tariq na Jabir. Kwangu nimefurahi kuona maendeleo yao ni mazuri, inatia moyo.”
VALENCIA SPF WAKUBALI
Inaelezwa kwamba kiwango cha Barka kimewastajabisha makocha mbalimbali wa kituo hicho na kusema kuwa kijana huyo anaweza kuwa tishio kwa miaka ya baadaye.
Licha ya kuwa na umri mdogo, Barka alionyesha kuwa na uwezo mzuri wa kuuchezea mpira kitu ambacho kiliwafanya makocha wa kituo hicho kuvutiwa naye.
Ikumbukwe ya kuwa wakati akiwa Uholanzi, alipewa tuzo ya kuwa mjuzi bora wa wiki, ikiwa na maana kuwa ni mchezaji aliyekuwa na mbinu nyingi (skills” kiasi cha kuwazidi wenzake ujanja pindi walipokuwa wakicheza pamoja.
“Inanitia moyo kama mzazi na kunifanya kuona kuwa ninachokifanya kwa watoto wangu kumbe sipotezi muda, kuna siku matokeo yake nitayaona,” anasema Seif.
BARCELONA MARCET WAMTOLEA MACHO
Mbali na kupewa mualiko kwenye kituo cha Valencia SPF, atatakiwa pia kuhudhuria program za kituo kingine cha Barcelona Marcet hapohapo Hispania.
“Nao wamependa kijana wangu ashiriki nao program mbalimbali za mazoezi, ni jambo zuri na naamini kuwa litamjenga kuwa bora zaidi. Unajua huu ndio umri wa mtoto kujengewa uwezo zaidi. Wamevutiwa na Barka ndio maana wamependa kuwa naye, sijaona tatizo kwa upande wangu,” anasema Seif.
UTALII WA DUNIA
Wikiendi iliyopita baada ya program mbalimbali za mazoezi za vijana wake wote watatu, Seif aliamua kutoka nao kwa ajili ya kwenda kwenye maonyesho ya Utalii ya Dunia nzima ambayo yalifanyika kwenye jiji la Madrid.
Seif anasimulia jinsi ilivyokuwa: “Tulitembelea banda letu la Tanzania, lililoandaliwa na Bodi ya Utalii Tanzania, ni zuri sana na nimejifunza vitu vingi sana. Kwanza nimegundua kuwa Tanzania inapendwa sana,”
“Unajua kwa nini?” Anaendelea kwa kusema: “Niliona watu wengi kutoka mataifa mbalimbali wakivutiwa na maonyesho ya Tanzania maana pale kulikuwa na luninga kubwa ambayo ilikuwa ikionyesha vivutio vyetu, ikiwemo mbuga za wanyama.
“Tuliongea mengi na Amos Tengu ni mtu mzuri sana huyu ambaye nilionana naye akiwa na maofisa wengine wa Bodi ya Utalii Tanzania, TTB huko Hispania. vijana wangu walifurahia sana huo mtoko maana tulitembelea pia vivutio vya mataifa mengine.”
NDOTO YACHOCHEA
Kitendo cha Barka kupata nafasi nyingi za kushiriki program mbalimbali za mazoezi, Seif amekitafsiri ni kama kichocheo cha hamasa katika kutimiza ndoto za mtoto wake.
“Shauku ya kijana wangu kufika mbali naona inazidi kukua kadri siku zinavyosogea, amekuwa akinieleza vile ambavyo anapenda kuwa mchezaji mkubwa ambaye ataipeperusha bendera ya Tanzania barani Ulaya,” anasema baba huyo na kuongeza:
“Nimekuwa mtu wa kumpa moyo na kumweleza kuwa hakuna jambo ambalo linashindikana, kikubwa ni kuwa na nidhamu na kuweka juhudi kwenye mazoezi kila siku.”