Wakongwe wamsubiri Aziz Ki, Lomalisa

Wakongwe wamsubiri Aziz Ki, Lomalisa

NYOTA wapya wa Yanga, Aziz Ki, Gael Bigirimana, Lazarous Kambole, Joyce Lomalisa na Bernard Morrison ndiyo habari ya mjini kuelekea kilele cha Wiki ya Mwananchi.
Nyota hao waliosajiliwa msimu huu wa dirisha kubwa wametajwa na wakongwe wa timu hiyo kuwa ni miongoni mwa watakaokuwa kivutio kwa mashabiki na wapenzi wao.
Tamasha la msimu huu limepokelewa kwa hisia tofauti na nyota wa zamani wa Yanga ambao wanalitazimia kufana zaidi na kushuhudiwa  na maelfu ya mashabiki kulinganisha na mengine matatu yaliyopita.
Tamasha hilo linafikia kilele kesho Jumamosi, kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar es Salaam, huku wanachama na mashabiki wa timu hiyo wakiendelea na shughuli za maadhimisho hayo kwa wiki nzima kuanzia Jumatatu wiki hii.


YUSUPH MACHO
Nyota huyu anasema usajili mpya wa msimu huu umeongeza zaidi hamasa, huku akitamani zaidi kuona viwango vya nyota hao wa kigeni.
“Kuifuatilia Wiki ya Mwananchi kwangu ni lazima na matamanio yangu ni kuwashuhudia nyota wetu wa kigeni, kile tunachokisikia kuhusu soka lao ni chenyewe?
“Aziz Ki amezungumzwa sana, pia kina Lomalisa na wengine, Wiki ya Mwananchi itanipa taswira ya ujio wao kwenye Ligi yetu kama utakuwa na faida na kuwapa changamoto wazawa,” alisema Macho.


SUNDAY MANARA
Mshambuliaji huyu nyota wa zamani Yanga anasema Wiki ya Mwananchi imekuwa ikipata mvuto kila mwaka tangu ilipoanzishwa mwaka 2019.
“Kuna matukio mengi ya kufana, utambulisho wa wachezaji, lakini yote kwa yote, Yanga imekuwa ikitoa fursa kwa wachezaji wake wa zamani, hili ni jambo jema sana hata kama si wote kwa kuwa ni wengi, lakini uwepo wa wachache wanaowakilisha wenzao ni jambo ambalo linaifanya Wiki ya Mwananchi kuongeza mvuto zaidi,” anasema.
Anaongeza msimu huu anaamini itafana zaidi kutokana na hamasa kubwa ya wapenzi na mashabiki ambao wanaendelea kufurahia mafanikio ya klabu yao kwa kutwaa ubingwa wa Ligi na Azam Sports Federation Cup.
“Kama haitoshi, usajili uliofanywa msimu huu ni kivutio ambacho kitanogesha zaidi Wiki ya Mwananchi, matukio ambayo klabu na wapenzi na mashabiki wake imekuwa ikiyafanya pia kwa jamii, hii inadhihirisha Yanga ni Wananchi halisi,” alisema.

Mohammed hussein ‘Mmachinga’
Nguli huyu wa zamani wa Yanga ni miongoni mwa mashabiki ambao wataifuatilia kilele cha Wiki ya Mwananchi kwa karibu, nyota huyo anasema tamasha hilo limekuwa likiiweka Yanga karibu zaidi na wananchi.
“Ratiba ya klabu katika matukio mbalimbali ikiwamo ya kijamii ni jambo kubwa la upekee, hili linaifanya klabu kuwa karibu zaidi na jamii, lakini kama haitoshi kuwashirikisha katika matukio nyota wake wa zamani katika tukio hili ni hamasa kubwa sana.
“Tunatarajia tamasha kubwa zaidi msimu huu kulinganisha na yale yaliyotangulia na huo ndio ukweli kwani tangu limeanza limekuwa likifana kila mwaka,” anasema.