UCHAMBUZI: Afcon Cameroon, darasa tosha la kuiandaa Taifa Stars

Saturday January 15 2022
afcon pic
By Charles Abel

FAINALI za Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) 2021 zinaendelea huko Cameroon ambapo leo mechi za raundi ya pili zitaendelea baada ya kuanza jana.

Jumla ya timu 24 zinashiriki fainali hizo zilizoanza Januari 9 huku zikitarajiwa kumalizika Februari 6 zikiwa zimegawanywa katika makundi sita.

Timu za Cameroon, Morocco, Nigeria, Mali, Gabon, Cape Verde, Senegal na Guinea zilianza vyema mashindano hayo kwa kuibuka na ushindi katika mechi zao za mwanzo na sasa zina kibarua cha kufanya vyema katika michezo iliyobakia ili ziweze kusogea katika hatua zinazofuata.

Wahenga wanasema safari moja huanzisha nyingine na hilo linategemewa kutokea huko Cameroon kwani wakati fainali za awamu hii zikiendelea, Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) litachezesha droo na kupanga ratiba ya mashindano ya kufuzu awamu ijayo ya Afcon itakayochezwa huko Ivory Coast mwaka 2023.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Caf, droo hiyo ya mashindano ya kufuzu Afcon mwaka 2023 itachezeshwa Januari 21 huko Douala, Cameroon .

Mashindano hayo ya kufuzu yataanzia katika raundi ya awali ambayo itakuwa ya mtoano itakayohusisha timu ambazo ziko chini katika viwango vya ubora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA).

Advertisement

Zile zitakazocheza hatua hiyo ya awali, zitatinga katika hatua ya makundi itakayohusisha jumla ya timu 48 zitakazogawanywa katika makundi 12 na baada ya hapo, timu mbili zitakazoongoza kila kundi zitafuzu fainali za Afcon 2023.

Timu ya taifa ya Tanzania ya soka ‘Taifa Stars’ itakuwa miongoni mwa zitakazoshiriki mashindano hayo ya kufuzu ambayo hapana shaka itaanzia moja kwa moja kwenye hatua ya makundi ikiwa inasaka kushiriki fainali zake za tatu za Afcon baada ya kushindwa kufuzu zile za mwaka huu zinazoendelea huko Cameroon ingawa kabla ya hapo ilishiriki mara mbili ambapo ni katika fainali za mwaka 2019 zilizofanyika Misri na za mwaka 1980 zilizoandaliwa huko Nigeria.

Japo Stars haipo kule Cameroon, kuna mambo matatu muhimu ya kufanyia kazi ambayo tunayaona katika fainali za Afcon ambazo zinaendelea yanayoweza kuifanya timu yetu ya taifa iwe inashiriki mara kwa kwa mara na kufanya vyema katika mashindano hayo au mengi itakayokuwa ikishiriki tofauti na ilivyo sasa.

Jambo la kwanza ni kuimarisha ubora wa waamuzi wetu. Tukiwa na waamuzi bora maana yake tutakuwa na ligi bora na yenye ushindani ambayo itasaidia Stars kupata wachezaji bora na washindani ambao watakuwa chachu ya mafanikio.

Kunapokuwa na ligi yenye ushindani na bora, timu zitaandaa vizuri wachezaji wao kimbinu, kiufundi, kisaikolojia na kifizikia hivyo tutakuwa na wachezaji waliokamilika na wenye utimamu wa kimwili na kiakili kuichezea timu ya taifa.

Jambo la pili ni kuandaa idadi kubwa ya makocha wazawa wenye uwezo na ubora wa hali ya juu ambao watafundisha klabu na timu zetu za taifa kwa ngazi tofauti.

Katika fainali zinazoendelea za Afcon huko Cameroon, kati ya timu 24 zinazoshiriki mashindano hayo mwaka huu, ni tisa tu ambazo zina makocha wakuu kutoka nje ya bara la Afrika huku 15 zikinolewa na makocha raia wa nchi za barani humu.

Tukiwa na idadi kubwa ya makocha wazuri humu ndani maana yake tutakuwa na uhakika wa maandalizi bora kwa wachezaji wetu wa ndani ukizingatia Stars kwa muda mrefu imekuwa ikitegemea kwa kiasi kikubwa wachezaji wa klabu za ndani kutokana na uchache wa wale wanaocheza nje ya nchi.

Lakini jambo la tatu ni kuhakikisha tunaimarisha na kuwekeza vilivyo katika soka la vijana zaidi ya kile tunachokifanya kwa sasa.

Idadi kubwa ya timu zinazoshiriki Afcon mwaka huu, zina kundi kubwa la wachezaji vijana ambao hawajafika hapo walipo kwa bahati mbaya.

Wengi wamepita katika misingi sahihi ya soka kuanzia katika umri mdogo jambo lililozivutia timu mbalimbali za Ulaya na Asia kuwasajili na kuwatumia jambo lililofanya waimarike na kupevuka kiasi cha kutosha kuzitumikia timu zao za taifa.

Tumeshakosea kutokwenda Cameroon kwenye Afcon mwaka huu, lakini hatupaswi kukosea kwa kutojifunza yale mazuri yanayoendelea katika fainali hizo za 33 nchini humo.

Advertisement