Tuliwachukulia Tunisia kama Malawi?

Friday November 20 2020
uchambuzi pic

BAADA ya matokeo ya mechi mbili za timu ya Taifa ‘Taifa Stars’ za kuwania kufuzu Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) zitakazofanyika 2022 huko Cameroon, maoni na mijadala imekuwa mingi na tofauti kutoka kwa wadau na mashabiki wa mpira wa miguu Tanzania.

Kundi kubwa limekuwa likiliangushia lawama benchi la ufundi la Taifa Stars chini ya Etienne Ndayiragije kuwa ndio chanzo cha timu hiyo kuvuna pointi moja katika mechi mbili za nyumbani na ugenini ilizocheza dhidi ya Tunisia, ikifungwa bao 1-0 ugenini na kisa kutoka sare ya bao 1-1 nyumbani.

Etienne analaumiwa kuwa mbinu alizoingia nazo kuikabili Tunisia hazikuwa sahihi kwani Taifa Stars muda mwingi ilikuwa inajilinda na mpira ulimilikiwa zaidi na Tunisia jambo ambalo liliwapa wakati mgumu Stars kutengeneza mashambulizi lakini wanaamini kama timu yetu ya Taifa ingeamua kufunguka, pengine ingepata matokeo mazuri zaidi ya hayo.

Inawezekana kweli Etienne na benchi lake la ufundi wana mapungufu yao lakini hoja ya kuwalaumu kwa timu kuingia na mbinu ya kujilinda dhidi ya Tunisia sidhani kama ina mashiko na ni kutowatendea haki Ndayiragije na wenzake.

Ilikuwa ni lazima kwa Stars kutumia ile kukabiliana na Tunisia tofauti na kile ambacho baadhi ya wadau na mashabiki walitegemea ikifanye kwa kulazimisha kumiliki mpira na kucheza kwa kupishana na timu hiyo ambayo inatoka katika ukanda ambao umepiga hatua kubwa kisoka barani Afrika.

Tunisia ni Taifa ambalo limeizidi Tanzania kisoka katika kila eneo kuanzia mafanikio, uwekezaji, uzoefu na hata ubora wa mchezaji mmojammoja hivyo tulipaswa kuingia kwa nidhamu kubwa ya mbinu, ufundi na ile ya kawaida.

Advertisement

Ukianzia kwenye mafanikio kisoka, kuna pengo kubwa kupitiliza baina ya Tunisia na Tanzania kuanzia katika mataji hata ushiriki katika mashindano ya kimataifa.

Wakati Tanzania ikiwa haijawahi kutwaa hata kufika angalau hatua ya robo fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika, Tunisia yenyewe ina taji moja la Afcon ambalo ililichukua mwaka 2004 wakati walipoandaa fainali za mashindano hayo.

Hawajaishia kutwaa taji hilo tu bali pia Tunisia ndio timu iliyoweka rekodi ya kushiriki Afcon mara nyingi mfululizo ambapo imefanya hivyo mara 15 na mara nyingi kati ya hizo, wamekuwa wakifika hatua za juu zaidi kama vile fainali, nusu fainali na robo fainali.

Ikumbukwe kuwa Tanzania imeshiriki Afcon mara mbili tu ambazo ni 1980 na mwaka jana 2019 ambazo zote iliishia katika hatua ya makundi na kushika mkia.

Achana na Afcon lakini pia timu ya taifa ya Tunisia, imeshiriki Fainali za Kombe la Dunia ambazo Tanzania haijawahi kushirki mara tano ambazo ni mwaka 1978, 1998, 2002, 2006 na 2018.

Ni nchi ambayo klabu zake za soka zimekuwa zikipata mafanikio makubwa katika mashindano ya klabu marani Afrika tofauti na Tanzania ambayo mafanikio makubwa kwa klabu zetu kwa miaka mingi ya hivi karibuni yamekuwa ni kushiriki hatua ya makundi ya mashindano ya klabu Afrika.

Tunisia ni timu ambayo ingeweza kutumia kundi kubwa la wachezaji wanaocheza soka la kulipwa katika klabu za kwao kama Esperance, Etoile Du Sahel, CS Sfaxien, Stade Tunisien, Club Africain na wakatusumbua vipi wakiwa na kundi kubwa la wachezaji wanaocheza soka la kulipwa barani Ulaya tena wengine wakiwa wamezaliwa na kukulia huko.

Wahbi Khazri, Nabil Makni, Naim Sliti, Ellyes Skhiri, Saif-Eddine Khaoiu na Dylan Bronn wote wamezaliwa Ufaransa, Mohamed Drager na Marc Lamti wamezaliwa na kukulia Ujerumani, Ayman Ben Mohamed (England) wakati Anis Slimane yeye akiwa ni mzaliwa wa England.

Wakati Tunisia wakiwa na nyota hao na wengine wanaocheza soka la kulipwa Qatar, Italia, Ufaransa, Ugiriki, Uturuki, Ujerumani na kadhalika, Stars yenyewe ilianza na Saimon Msuva na Himid Mao wanaocheza soka la kulipwa nje ya nchi tena katika klabu za daraja la kati katika ligi za Misri na Morocco.

Katika mazingira kama hayo, ilikuwa ni bora kuwaheshimu Tunisia badala ya kutaka kujilinganisha kwani vinginevyo wangeweza kutufunga kwa aibu.

Pengine mbinu hiyo ndio imefanya wengi wadhani Tunisia ni timu ya kawaida lakini kiuhalisia, walionyesha utofauti wa daraja baina yetu na wao kwani walifanya kila kitu ndani ya uwanja na kama sio uhodari wa safu yetu ya ulinzi, hali ingeweza kuwa mbaya.

Vipo vya kumlaumu Etienne lakini sio kile cha timu yetu kujilinda dhidi ya Tunisia. Tungeweza kufanya hivyo na kushangaa iwapo tungekuwa tumekutana na timu kama Malawi, Botswana, Swaziland na Lesotho lakini sio Tunisia.

___________________________________________________________

By CHARLES ABEL

Advertisement