Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

SPOTIDOKTA: Shabiki afariki dunia La Liga, refa ajeruhiwa Uturuki

KWENYE medani ya soka katika vyombo vya habari na mitandao ya kijamii kuna matukio mawili yaliyojiri wiki hii ikiwamo mwamuzi wa Ligi Kuu Uturuki kujeruhiwa na shabiki wa soka kufariki dunia uwanjani.

Tukio la shabiki kufariki lilitokea Jumapili iliyopita, Hispania katika mchezo wa Ligi Kuu nchini humo (La Liga) kati ya Granada na Athletic Club kwenye Uwanja wa Los Carmenes.

Tukio hilo lililotokea dakika ya 17 kipindi cha kwanza lilisababisha mchezo huo kusimama na hapo baadaye iliamuliwa uahirishwe kutokana na makubalianao ya timu hizo mbili. Awali wakati mchezo huo ukiendelea shabiki mwanaume - mtu mzima alianguka ghafla akiwa anatazama mechi hiyo. Watu wa huduma ya kwanza walifika kumhudumia na kukimbizwa hospitali.

Alipelekwa katika huduma za afya za juu, lakini baada ya saa moja ilithibitishwa kuwa tayari ameshafariki dunia. Chanzo cha kifo kilielezwa ni mshtuko wa moyo, kitabibu hujulikana kama Cardiac Arrest.

Tukio la pili ni kujeruhiwa kwa Refa Halil Umur Meler nchini Uturuki, Jumatatu wiki hii katika mchezo wa Ligi Kuu ambapo alipigwa ngumi na rais wa klabu ya Ankaragucu, Faruk Koca baada ya mchezo kumalizika kwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Rizespor.

Lilikuwa ni moja ya matukio mabaya kuonekana katika medani ya soka la kimataifa, kwani siyo tu alipigwa ngumi, bali alipigwa na teke kichwani akiwa chini - sakafuni. Viongozi na wasaidizi wake waliokuwa jirani walijitahidi kumzuia rais huyo ambaye alishuka ghafla kutoka jukwaa la watu mashuhuri na kumvamia kwa shambulizi la kustukiza. Refa alikumbana na kipigo hicho wakati wanatoka uwanjani alijeruhiwa zaidi kichwani katika eneo la jicho la kushoto likioneka kuvimba na kuvulia damu.

Tukio hili limesababisha rais wa Chama cha Soka nchini humo kusimamisha ligi zote.

Jicho la tatu la kitabibu linayatama matukio haya kama moja ya matukio ambayo yanaweza kutupa funzo na pia kutupa ufahamu katika eneo la magonjwa ya moyo na majeraha ya mwili.


MSHTUKO WA MOYO

Cardiac Arrest ni mstuko wa moyo au moyo kusimama ghafla kufanya kazi au mshtuko. Mara nyingi chanzo ni hitilafu ya umeme wa moyo ambao ndio unaowezesha misuli ya moyo kutoa mapigo.

Ikitokea hivyo utendaji wa moyo wa kutoa mapigo na kusukuma damu huenda mrama na kusimama ghafla hatimaye kushindwa kusukuma damu maeneo nyeti ikiwamo Ubongo, mapafu na ogani nyingine.

Mwathirika huweza kupoteza fahamu huku unepaji wa mishipa ya damu hupotea na ndani ya dakika chache anaweza kupoteza maisha kama hatua za haraka na uhakika hazitachukuliwa.

Kwa kawaida tatizo hilo hutokea bila kuwa na dalili au viashiria vya kuonya na mara nyingi huchochewa na matatizo ya mfumo wa umeme wa moyo baada ya kupata hitilafu na kusababisha mapigo yasiyo na mpangilio.

Dalili za awali zinazoweza kujitokeza ni pumzi kukatika, kuhisi kuishiwa nguvu au kuchoka, kuona ghafla mawimbi au giza, maumivu ya kifua na mgongo na kichefuhefu au kutapika.

Mara nyingi cardiac arrest ni tatizo ambalo linaweza kutokea na kusahihishwa na kurudi katika hali ya kawaida kama awali.

Nchi zilizoendelea ambazo ndizo zenye idadi kubwa ya watu wanaopata tatizo hilo hutumia huduma ya usingaji wa kifua na kuongezewa hewa ya oksijeni ili kuwaokoa wahusika.

Katika tukio hilo watoa huduma ya kwanza pale uwanjani walifanya huduma ya usingaji wa moyo ambayo ni moja ya huduma za msingi kwa mtu ambaye anadondoka ghafla na moyo kusimama.

Ufahamu wa huduma hiyo umekuwa ukifundishwa kuanzia katika shule za msingi na watoa huduma hasa wa serikali na wale wa Shirika la Msalaba Mwekundu duniani. Inafundishwa hivyo kutokana na umuhimu wake kwa ajili ya kiungo nyeti cha mwili hatimaye kupata usaidizi pale moyo unaposimama. Ni huduma ambayo imekuwa ikiokoa waathirika pasipo uwepo wa daktari.

Tatizo la moyo kusimama ghafla linasababishwa na magonjwa ya moyo hasa yale yanayoathiri mapigo ya moyo ikiwamo mfumo wa umeme wa moyo.

Magonjwa hayo ya moyo ni pamoja na shinikizo la juu la damu, tatizo la mapigo ya moyo kwenda bila mpangilio, moyo kutanuka, kuwa na kiwango kikubwa cha lehemu mbaya.

Vihatarishi vya tatizo hilo ni pamoja na unene, uvutaji tumbaku, unywaji pombe, utumiaji dawa za kulevya, kuugua magonjwa ya moyo, kutoka katika familia yenye historia ya magonjwa ya moyo au mstuko wa moyo na upungufu wa madini mwilini.

Ili kujikinga na tatizo hili inatakiwa kuepukana na vihatarishi vilivyotajwa pamoja hapo juu, fanya kazi za kushughulisha mwili au mazoezi mepesi angalau kwa siku dakika 30-60 katika siku tano za wiki.

Zingatia kanuni za afya kwa ulaji bora wa vyakula ikiwamo mbogamboga za majani na matunda, ulaji wa protini rafiki kama samaki na jamii ya kunde.

Dhibiti sukari, shinikizo la juu na lehemu mbaya (Cholesterol)kwa kushikamana na ushauri na matibabu ya wataalam wa afya. Angalau chunguza afya yako mara moja kwa miezi 6.


MAJERAHA YA REFA NI HATARI

Mara baada ya kupigwa ngumi iliyotua eneo la usoni karibu na jicho na kusababisha refa huyo kuanguka ambapo akiwa chini alipigwa teke kichwani kabla ya watu waliokuwa jirani kumzuia rais huyo, kwa jicho la kitabibu upigaji huo ulikuwa ni hatari kwani eneo la kichwa ni  nyeti la mwili ambalo linapopata mtikisiko wowote linaweza kujeruhi ubongo.

Ngumi ya binadamu na uzito pamoja na ugumu wa mfupa ni sawa na kupigwa na kitu kizito ndio maana ngumi ya rais huyo ilimdondosha chini mwamuzi.

Hii ingeweza kusababisha jeraha baya la ubongo ambalo linaweza kumpa ulemavu wa kudumu ikiwamo kupooza viungo, kifafa au kifo cha mapema kutokana na kuvuja damu katika ubongo.

Ndio maana ilikuwa ni lazima, refa huyo kuwa chini ya uangalizi wa madaktari muda wa 24-72 kuona kama shambulizi hilo linaweza kumletea madhara ya baadaye.

Refa naye ni binadamu kitendo alichofanyiwa si cha kiungwana katika tasnia ya soka.

Ulinzi kwa marefa ni muhimu hasa pale panapokuwa na tishio au utata wa kimaamuzi, kama wana usalama wa uwanja wangelikuwa makini refa huyo usingeweza kuvamiwa na kujeruhiwa.


CHUKUA HII

Magonjwa ya moyo ndio yanaongoza duniani kwa kusababisha vifo vingi, hakikisha unashikamana na njia zote za kujikinga ikiwamo kufanya mazoezi na kuwa na mienendo na mitindo bora ya kimaisha.

Soka ni burudani na ni chanzo kikubwa cha mapato. Vitendo vya vurugu ikiwamo kupigana au kushambuliana havitakiwi kupewa nafasi katika medani.