MOALLIN: Tunajenga timu mpya, furaha

MOALLIN: Tunajenga timu mpya, furaha

EL GOUNA. IKIWA katika wiki ya pili ya kambi ya wiki tatu mjini El Gouna, Misri, Azam FC wako ‘bize’ kuziba kila mwanya unaoweza kuwaharibia mipango yao msimu ujao.

Baada ya usajili mzuri uliofanyika, sasa kazi ipo kwa benchi la ufundi kuunganisha timu ili Chamazi isiwe sehemu salama kwa wageni.

Kocha Mkuu wa Azam, Abdihamid Moallin anawaambia wachezaji wake mara kwa mara kwamba hawakuja El Gouna kwenye mapumziko, bali kujiandaa na msimu mpya.

“Tumekuja hapa kuteseka ili tufurahi baadaye. Tumekuja hapa kuisoma ramani ya kupita baadaye. Tumekuja hapa kutafuta furaha ya mashabiki wetu,” Moallin.

Moallin anasema yeye na benchi lake lote la ufundi lengo lao namba moja ni kubadili ‘mentality’ za wachezaji wake.

“Wanatakiwa kujua kwamba wanaochezea timu kubwa. Najua wanajua hilo na ndiyo maana walikubali kuja hapa, lakini wanatakiwa kuliweka hilo kwa vitendo siyo kwa maneno.”

Katika vitu vinavyomtesa Moallin ni tabia ya timu yake msimu uliopita kushindwa kupata ushindi katika mechi za mfululizo.

“Tangu tushinde mechi tatu mfululizo Januari, hatukushinda tena mfululizo hadi Juni. Haipaswi kuwa hivyo tena msimu huu. Sifa ya timu kubwa ni kushinda mfululizo.”

Katika kuhakikisha hilo linawezekana, Moallin anatumia kila silaha aliyonayo kuitengeneza timu yake sasa lakini hataki kujipa presha ya ubingwa.

“Ona, hii timu haijachukua ubingwa kwa muda mrefu. Kwa hiyo kitu cha kwanza ni kujenga ‘mentality’ za wachezaji huku tukiimarisha uwezo wao uwanjani. Hilo likikamalika ndiyo tunaweza kuanza kuzungumzia ubingwa, lakini haliwezi kuwa la ghafla, linaweza kuchukua misimu miwili hadi minne,” anasema.

“Timu inayojengwa kwa muda mrefu hutawala kwa muda mrefu pia. Napenda sana kumtolea mfano Jurgen Klopp wa Liverpool, aliijenga timu yake kwa miaka minne, unaoionaje sasa?”

Azam ina wachezaji wengi wenye umri mdogo ambao watacheza kwa muda mrefu sana endapo watatunzwa vizuri.

Wastani wa umri wao ni miaka 24, hii ina maana Azam ina timu ya kukaa pamoja kwa zaidi ya miaka mitano mbele.

“Najua mashabiki wanahitaji sana mafanikio, lakini haiwezi kuwa ghafla. Acha tujenge kwanza timu lakini picha kubwa tutalipata baada ya haya maandalizi.

“Kutengeneza muunganiko siyo kitu rahisi. Wachezaji wanatakiwa kufahamiana sana. Muunganiko siyo tu dakika 90, bali maisha yao kama yote kwa ujumla.

“Je, wanasalimiana wakiwa majumbani kwao? Wanapigiana simu kujuliana hali? Hayo yakitokea ndiyo huhamia ndani ya uwanja na timu huimarika.”

Moallin anasema daraja ambalo Simba na Yanga wapo ni la juu na kama kocha anatakiwa aipandishe timu yake kufikia hapo au kuzidi. “Wewe (ananiambia mimi) upo nchi hii miaka mingi kuliko mimi, labda unajua zaidi.”

Ni lini Simba ilifika robo fainali tatu za CAF ndani ya miaka 5 tu? Ni lini Yanga walikuwa mabingwa bila kupoteza?” anahoji.

“Hii ina maana hizi timu zimekuwa bora sana, nasi tunatakiwa kufika huko na kuwazidi. Bila hivyo hatutafanikiwa malengo yetu. Lakini hatuwezi kuwazidi ndani ya msimu mmoja...ni mpango wa muda mrefu kidogo.”

Moallin anaamini anao ubora wa kutosha ndani ya timu katika nafasi zote, kuanzia langoni hadi mwisho, lakini anasema hiyo haitoshi.

“Unapokuwa na kikosi cha namna hii ni jambo zuri, lakini jambo zuri ni kuwa na wachezaji wenye njaa na kiu cha mafanikio.

“Kwanza watake kufanikiwa wao wenyewe kwa kujituma ili wafike mbali. Walifanya hivyo maana yake klabu pia itafanikiwa.”

Nahodha Aggrey Morris anasema wao kama wachezaji inawatesa kukosa mafanikio kwa sababu ndicho kitu kitakachowapa faraja watakapostaafu.

“Miaka mingi baadaye watu hawakumbuki nani alimfunga nani, wanakumbuka bingwa alikuwa nani.

“Kwa hiyo kukosa ubingwa kunatutesa sana kwa sababu hatutakumbukwa tukishastaafu. Tunatakiwa kujituma na kufuata maelekezo ya walimu wetu ili kupata mafanikio,” anasema.

“Msimu huu utakuwa tofauti sana kwetu. Mimi nipo timu hii muda mrefu lakini safari naona kabisa viongozi wameamua kwa hiyo na sisi lazima tuwaunge mkono. Azam itakuwa hapa El Gouna hadi Agosti 11 ndipo itarudi nyumbani kwa ajili ya kumalizia maandalizi kabla ya kuanza msimu mpya.”