Mitihani mitano Kamwaga Simba

WIKI iliyopita Simba ilimtangaza, Ezekiel Kamwaga kukaimu nafasi ya Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano kwa miezi miwili kabla ya kutangaza rasmi nafasi za ajira katika eneo hilo.

Kamwaga aliwahi kuhuduma katika klabu hiyo kwenye nafasi aliyokuwepo sasa na aliwahi kuwa Katibu ambaye alisimamia shughuli zote za klabu ambazo zilikuwa zikifanyika kila siku.

Wakati anafanya kazi kwenye nafasi hizo kipindi cha nyuma na sasa ni tofauti kabisa kwani kuna mabadiliko mengi ikiwemo uendeshaji wa klabu ya Simba ambao unatumika kwa wakati huu ni wa kisasa.

Mwanaspoti linakuletea mitihani mitano ambayo Kamwaga anakwenda kukutana nayo ndani ya Simba kulingana na majumu ya nafasi yake kama ambavyo anatakiwa kuyafanyia kazi.


PRESHA

Jambo la kwanza presha ambayo ilikuwepo mwaka 2014, akiwa katika nafasi ya Ukatibu ni tofauti na ambayo anakwenda kukutana nayo wakati huu katika majukumu yake.

Awamu hii Kamwaga atakutana kwanza na presha ya kazi kutoka kwa muajiri wake, Barbara Gonzalez ambaye ni mmoja wa viongozi wasiopenda kupindisha katika wanachosimamia na wanaojali muda.

Presha nyingine ambayo atakwenda kukutana nayo zaidi ya hapo awali ni kutoka kwa mashabiki wa Simba ambao wanaamini kila leo timu yao inastahili kushinda na si kupoteza mechi.

Kama ikitokea Simba wanafanya vibaya, mtu sahihi ambaye atakuwa anaongea na mashabiki ni Kamwaga. Anatakiwa kuwa na utulivu na ushawishi mkubwa ili kushindana na presha hiyo.


WAANDISHI

Ofisa Habari wa aliyeondoka, Haji Manara, mbali na ushawishi mkubwa aliokuwa nao na juhudi kubwa alizokuwa akifanya, lakini alikuwa na mivutano ya hapa na pale na baadhi ya wanahabari.

Kati ya matukio yake ya kukumbukwa katika siku za hivi karibuni, ni pale alipowaita takataka wachambuzi wa michezo ambao aliamini hakuwa na weledi, alivutana na mtangazaji mwanadada Prisca Kishamba katika mkutano na wanahabari ambao ulikuwa ukionyeshwa ‘live’, jambo ambalo lilifanya hadi vyama vya wanahabari kutoa matamko ya kumkosoa Manara, amekuwa akipishana pia na mtangazaji Shafih Dauda wa Clouds na pia Manara amewahi kusuluhishwa tofauti zake na watu wazima kama ambavyo alifanya baba yake mzazi, Sunday Manara wakati alipokuwa na tofauti na Maulid Kitenge.

Kuingia kwa Kamwaga katika nafasi hiyo kwanza anatakiwa kuwaona waandishi wa habari wote ambao anafanya nao kazi wanakuwa na maelewano mazuri pamoja na usawa mmoja.

Isitokee tena kuna baadhi ya waandishi Kamwaga awe anawapatia ushirikiano na wengine anashindwa kuwapa hilo halitakuwa jambo sahihi na anaweza kutengeneza matabaka kama kipindi hajaingia katika nafasi hiyo.


UWEZO

Ni wazi kama Kamwaga alipewa hadi ya nafasi ya Ukatibu klabuni Simba maana yake anauwezo mzuri katika utendaji wa shughuli zake za kila siku.

Kamwaga hata katika gazeti hili kolamu zake nyingi zimekuwa zikionyesha kuwa na uwezo mkubwa wa kufikiria na kuandika maandiko ambayo yalikuwa kama si kujenga basi yanafundisha.

Shida kubwa itakuwa katika kuongea endapo kama atapata nafasi ya kufanya mkutano na waandishi, kwani huko mtaani mashabiki wengi wa soka wanaamini ukiwa katika nafasi hiyo unatakiwa kuwa na uwezo wa kuongea kama Manara au Jerry Muro.

Kamwaga anatakiwa kuishi katika misingi yake na asitake kuonyesha kuwa naye anaweza kuongea kama vile ambavyo mashabiki wa timu hiyo wakuwa wanahitaji au kutamani kutoka kwake.


KIVULI CHA MANARA

Ukweli usiopingika kuna maeneo ambayo Simba wamenufaika kutokana na ushawishi ambao alikuwa nao Manara ndani ya kipindi cha muda wote aliofanya kazi katika kikosi hicho.

Kipindi cha miezi miwili ambacho Kamwaga atakuwa na kivuli cha Manara nyuma yake katika maeneo ambayo amefanya vizuri anatakiwa kuyaboresha zaidi na pale aliposhindwa anatakiwa kupainua.

Kati ya maeneo ambayo Simba na Manara walifanikiwa ni katika ushawishi wa mashabiki wao kujitokeza uwanjani kwa wingi huku wakiwa wanaishaingilia timu hiyo mwanzo mwisho.

Idara hiyo ya habari Simba imefanikiwa kuwa na ushawishi wa kuwatuliza mashabiki wao pindi wanaposhindwa kupata matokeo mazuri kama ilivyokuwa katika mechi dhidi ya Kaizer Chiefs licha ya kufungwa mashabiki waliwapigia makofi wachezaji wao kama wameshinda.


UTANI WA YANGA

Katika eneo jingine ambalo Kamwaga atakuwa anakutana nalo kama changamoto ni utani kutoka kwa mashabiki wa Yanga, ambao mara zote si rahisi kwao kukubali jambo la Simba.

Mashabiki wa Yanga na Simba mara zote huwa hawaangalii mahala pa kutania kama mazoea yao yalivyo iwe katika mitandao ya kijamii, vijiwe vya soka au kwenye maisha ya kawaida.

Kamwaga anatakiwa kulitambua hilo na kutokuwa na hasira wala jazba kati yake dhidi ya utani ambao atakuwa anakutana nao kutoka kwa mashabiki hao wa soka nchini.