Dk Cugat ndiye Messi wa tiba ya wanasoka duniani

Friday January 14 2022
Dokta PIC
By DK. SHITA SAMWEL

NYOTA wa PSG na timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi ni mmoja wa wachezaji bora kuwahi kutokea duniani akiwa na kipaji cha hali ya juu cha kucheza soka na hatimaye kuweza kuibuka Mwanasoka Bora wa Dunia mara 7.

Anachuana vikali la Cristiano Ronaldo anayekupiga kwa sasa Manchester United na timu ya taifa ya Ureno, lakini unaambiwa kwenye upande wa ulimwengu wa tiba za upasuaji wa majeraha ya michezo kuna “Messi wa tiba” toka nchini Hispania akijulikana kama Dk Ramon Cugat Bertomeu.

Huyu jamaa ni daktari bingwa aliyebobea katika upasuaji wa mifupa, majeraha ya michezo, upasuaji wa kisasa wa matundu, bailojia ya seli na ukuaji wa viungo.

Daktari huyu, anayeingia umri wa miaka 72 kwa sasa anatokea katika familia ya wakulima amekuwa ni mwokozi wa maelfu ya wachezaji wanaopata majeraha yatakanayo na michezo.

Maelfu ya wachezaji maarufu duniani husafiri umbali mrefu kwa ajili ya kwenda Hispania kufuata huduma yake ya upasuaji ili kutibiwa majeraha mabaya wanayopata katika soka.

Hata Messi alipoumia goti mwaka juzi alifanyiwa upasuaji wenye mafanikio na Dokta Cugat hatimaye alipona na kurudi katika mchezo akiwa timamu kama hapo awali.

Advertisement

Wanasoka wengine maarufu waliofanyiwa upasuaji na daktari huyu ni pamoja na Luis Suarez akiwa Barcelona, Calum Hudson-Odoi wa Chelsea, John Stone wa Manchester City na Thiago Alacantara wa Liverpool.

Hata kocha wa sasa wa Manchester City Pep Gurdiola akiwa anaichezea klabu ya Barcelona aliwahi kufanyiwa upasuaji uliomfanya kupona na kurudi tena kuitumikia klabu yake.

Pep aliwahi kukaa nje siku 400 bila kucheza mwaka 1997 mpaka 1998, lakini baadaye aliweza kurudi tena uwanjani baada ya kutibiwa na Dk.Cugat.

Miaka 10 baadaye Pep alichaguliwa kuwa kocha mkuu wa Barcelona na kuamua wachezaji wote wanaopata majeraha ya michezo kutibiwa katika kliniki ya Dokta Cugati.

Hata alipotua Manchester City aliingia katika makubaliano ya kikazi na Dk.Cugat kwa kuwatibu wachezaji wake wanapopata majeraha makubwa ya michezo.

Pep anamweleza kuwa ni daktari mahiri namba moja duniani wa upasuaji wamifupa na majeraha ya michezo kuwahi kutokea akimtibu kwa mafanikio wachezaji aliowahi kuwafundisha ikiwamo Xavi na Messi

Nguli huyu ambaye pia ni mtafiti mbobezi tayari ana mbinu yake ya kitiba aliyoibuni ambayo imepata mafanikio inayojulikana kama PRP (Platelet Rich Plasma) ambayo inaongeza kasi ya uponaji wa jeraha.

Mbinu hii inahusisha kuchukua sehemu ya damu yenye chembe sahani toka kwa mchezaji aliyejeruhuwa na huweka katika mashine inayochekecha na kuitenganisha sehemu hiyo ya damu na baadaye huchomwa katika eneo lenye jeraha.

Gharama za uchomaji sindano ina gharimu kiasi cha Paundi 435 sawa na karibu milioni 1.45 za kitanzania. Huduma hii ilipata umarufu na kutangazwa sana nchi Uingereza baada ya mchezaji wa Manchester City John Stones kuchomwa na kumletea uponaji wa haraka wa jeraha.

Klabu ya Barcelona kwa miaka mingi imekuwa ikimtumia Dk.Cugat kuwatibu wachezaji wake, hata miezi michache iliyopita amemfanyia upasuaji wa goti kinda wao Ansu fati baada ya kupata majeraha ya goti.

Umahiri wake si katika kupasua pekee bali pia hapo kuhakikisha wakati wa uuguzi mgonjwa anapata virutubisho maalum ambavyo yeye amevitafiti kusaidia uponaji wa haraka wa majeraha.

Amekuwa pia akifanya tiba ya upandikizaji wa vishina vya seli kwa wachezaji waliopata majeraha mabaya ikiwamo upandikizaji wa vishina vya seli katika magoti kwa wachezaji waliovunjika mifupa plastiki gotini.

Alianza kujulikana nchini Hispania tangu enzi za mashindano ya Olimpiki ya kiangazi yaliyofanyika mwaka 1992 jijini Barcelona akiwa ni mmoja wa madaktari maalum wa upasuaji wa mifupa na majeraha ya michezo. Umaarufu wake duniani ndiyo umechangia kupachikwa jina la “Messi of Medicine” ambalo Pep Gurdiola alikuwa akimwita hivyo mara kwa mara na sasa hata wachezaji wanaotibiwa hapo humtania kwa jina hilo

Timu kubwa zinazoshiriki ligi ya la liga zimewahi kujaribu kutaka kumwajiri lakini alikataa jukumu hilo mwenyewe akipendelea kuhudumu katika kliniki yake.

Daktari huyu alieleza hataki kuajiriwa na kueleza hivi “ninachopenda ni kuwa daktari wa wanasoka wote, nilipo milango iko wazi kwa dunia nzima”.

Dk.Cugat ambaye ni mzaliwa wa Tortosa Hispania ni muda mrefu anaishi na kufanya kazi katika kliniki yake nchini Hispania akiwa na timu yake ya wataalam wa Afya.

Amepata elimu yake toka chuo kikuu cha Barcelona na amewahi kupokea tuzo ya heshima ya “nguli aliyebobea katika upasuaji kwa njia ya matundu” na kuwa mfano wa “uthamani wa taaluma na utafiti wa kitabibu katika jamii”.

Amekuwa na kituo chake cha utafiti wa kitabibu tangu mwaka 2007 kikijulikana kama Garcia Cugat Foundation biomedical Research akifanya kazi kwa miaka 10 na timu za madakatari wa upasuaji wa mifugo, Chuo kikuu cha Barcelona, Valencia, Murcia na Cordoba.

Anaeleza kuwa lengo la kliniki yake ni kutoa matibabu ya kiwango cha juu kwa wagonjwa wake. Na hilo amefanikiwa na ndiyo maana wagonjwa husafiri toka nchi zingine na kumfuata Hispania.

Katika kliniki yake amekuwa akipokea wachezaji kutoka katika ligi kubwa duniani ikiwamo la EPL, Series A, Bundesliga na ligue One ya Ufaransa.

Mahusiano yake mazuri ya muda mrefu na vyama vya soka yamechangia kufanya kazi kwa karibu na FIFA hatimaye kuwafikia na kuwatibu wachezaji wengi wanaopata majeraha ya michezo.

Anaeleza katika kitabu chake cha wasifu kuwa utafiti ni moja ya egemo kuu la taaluma yake kwani ndiyo imemfanya kuweza kufanikiwa katika matibabu anayoyatoa.

Huyu ndiyo Dk. Cugat “Messi wa tiba” anayeishi maisha ya kawaida na kuyatoa maisha yake kwa ajili ya kuwahudumia majeruhi wa soka.

Advertisement