Zuchu atisha, atazamwa na Watanzania 'wote'

SUPASTAA wa Bongo Fleva kutoka Lebo ya Wasafi (WCB), Zuhura Othman Soud maarufu Zuchu ameweka rekodi mpya baada ya video ya wimbo wake wa Sukari kutazamwa na zaidi ya watazamaji 'Viewers' 100 milioni kwenye mtandao wa Youtube ikiwa ni miaka mitatu tangu aipandishe kwenye mtandao huo.

Kutokana na idadi hiyo ya watu walioitazama katika mtandao huo ina maana kwamba wimbo huo umeangaliwa na karibu Watanzania wote milioni 61 (kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022) pamoja na watu wa nchi mbili za Afrika Mashariki za Uganda na Rwanda.

Hiyo ni mara ya kwanza kwa Msanii wa kike kutoka Afrika Mashariki kufikisha idadi hiyo ya watazamaji katika mtandao huo kwa wimbo mmoja.

Vilevile Zuchu amekuwa msanii wa kwanza kufikisha idadi hiyo ya viewers kwenye wimbo wa Kiswahili ulioimbwa na msanii mmoja bila kushirikisha mtu mwingine.

Msanii huyo ameungana na Diamond Platinumz na Harmonize kugonga views milioni 100 kwenye mtandao huo ambapo Diamond amefanya hivyo mara tatu kwa nyimbo alizowashirikisha wWakongomani tofauti, huku Harmonize akifanya mara moja kwa video ya ngoma ya Kwangwaru aliyomshirikisha Diamond miaka mitano iliyopita ambayo hadi sasa ina viewers zaidi ya milioni 111.

Ngoma za Diamond zilizogonga milioni 100 ni video za Yope Remix aliyoshirikishwa na Innos B miaka minne nyuma, lakini akaichapisha kwenye ukurasa wake na hadi sasa ina zaidi ya viewers 225, ikifuatiwa na Waah aliyomshirikisha Koffi Olomide miaka mitatu iliyopita ikiwa na zaidi ya viewers milioni 154 kisha Inama aliyomshirikisha Fally Ipupa miaka minne iliyopita inayosoma zaidi ya viewers milioni 134.