Prime
Mabadiliko makubwa yanukia Msimbazi

Muktasari:
- Kuna kila mabadiliko makubwa yananukia kikosini Msimbazi huku majina kadhaa yakitajwa mpaka sasa.
VIKAO vizito vinaendelea ndani ya Simba kupitia tathimini za mchezaji mmoja mmoja kuona mchango wake kama utaisaidia timu hiyo msimu ujao 2025/26.
Kuna kila mabadiliko makubwa yananukia kikosini Msimbazi huku majina kadhaa yakitajwa mpaka sasa.
Tayari yapo majina ya mastaa wa kigeni waliokaliwa kooni kuhakikisha wanakatwa.
Kati ya mastaa ambao ni 50 kwa 50 kusalia ama kuondoka ni mshambuliaji raia wa Cameroon, Leonel Ateba, kiungo mkabaji Augustine Okajepha aliyetokea Rivers United ya Nigeria na kiungo mshambuliaji Debora Fernandes Mavambo.

Siyo hao tu. Chanzo hicho kilisema tayari Simba imeanza kusaka beki wa kati, akipatikana mchezaji aliye katika mstari wa kuachwa ni Che Malone Fondoh ambaye vigogo wengi wanaona uwezo wake ni wakawaida jambo ambalo linasapotiwa kiufundi pia na namba zake kwenye michezo migumu.
Mwanaspoti lilianza kuripoti kuhusu Simba kuchambua wachezaji wazawa ambao wapo katika mjadala wa kuachana nao ambao ni Hussein Kazi (kamaliza mkataba), Hussein Abel, Edwin Balua (mabao mawili), Aishi Manula(mkataba unaisha) na Valentino Mashaka (mabao mawili).
Chanzo cha taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo, kilisema sababu ya Ateba ambaye hadi sasa ana mabao 12 kupendekezwa na viongozi baadhi akatwe hawajaona uwezo wake wa kuibeba timu nyakati ngumu, hivyo wanahitaji kupata mbadala wake aliye na uwezo mkubwa, huku jina la mshambuliaji wa Singida Black Stars, Jonathan Sowah likitajwa kujadiliwa ili kuongeza nguvu msimu ujao.
"Mipango ya Simba msimu ujao ni mikubwa inahitaji mshambuliaji mwenye uwezo mkubwa wa kufunga, hivyo ni miongoni mwa vitu vilivyotunyima ubingwa wa CAF alikosekana mwenye kufosi mashambulizi," kilisema chanzo hicho na kuongeza;
"Kuhusu Mavambo na Okajepha imekuwa tofauti na walivyotarajiwa wangefanya makubwa yakumpa kocha upana wa kuchagua kikosi, badala yake wamekuwa wakitumika Yusuph Kagoma na Fabrice Ngoma.
"Kuhusu Joshua Mutale anakingiwa kifua na kocha Fadlu Davids anamuona ni mchezaji mwenye bidii ya mazoezi na alikuwa anakikaa naye mara kwa mara ili kujua sababu ya kufanya vibaya wakati wa mechi za mashindano na sasa matunda yake yanayoonekana ligi inapoenda mwishoni."

"Kuna marekebisho makubwa yatafanyika,hao wachezaji ni baadhi kwa sababu huwezi kuondoa mchezaji kabla hujapata mbadala wake," kilisema chanzo hicho.
Pamoja na Simba kujadili wachezaji ambao wanapendekezwa kuwaacha, inafanya juhudi ya kumalizana na wale ambao wamemaliza mikataba yao na wanahitaji kuendelea nao akiwemo nahodha Mohamed Hussein 'Tshabalala."