Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

ASHA BARAKA: Aishtukia hatuchezi ya Yanga, asimulia miaka 30 ya kibabe

ASHA Pict

Muktasari:

  • Mwanamama huyo anajiandaa kuadhimisha miaka 30 ya kuwepo kwake katika shughuli za kimuziki akiwa mmoja ya wamiliki wa bendi ya muziki wa dansi wa kike anayeendelea kukomaa katika fani licha ya anguko kubwa la muziki huo ukilinganisha na ulivyokuwa miaka ya nyuma.

MASHABIKI wa muziki wa dansi wamempachika jina la Iron Lady, lakini jina lake kamili ni Asha Baraka, mwenyekiti wa Bendi wa Twanga Pepeta na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba.

Mwanamama huyo anajiandaa kuadhimisha miaka 30 ya kuwepo kwake katika shughuli za kimuziki akiwa mmoja ya wamiliki wa bendi ya muziki wa dansi wa kike anayeendelea kukomaa katika fani licha ya anguko kubwa la muziki huo ukilinganisha na ulivyokuwa miaka ya nyuma.

Asha Baraka, anasimulia mengi juu ya safari hiyo ya miaka 30 yenye kila aina ya hali kuanzia furaha, misukosuko na changamoto na kufunguka pia nafasi yake ndani ya Simba na na mtazamo wake kuhusu Dabi ya Kariakoo ambayo haijafahamika kama itapigwa au la.

Nyota huyo wa zamani wa kimataifa wa mchezo wa netiboli, anasema licha ya Yanga kutishia kutocheza mechi hiyo ya Juni 15, anaamini watani wanafanya danganya toto na kwamba gemu ipo kama kawaida, huku akitoa sababu sambamba na mambo mengine yahusuyo muziki na soka kwa ujumla.


FURAHA MIAKA 30

Asha anasema anajivunia kutimiza miaka 30 ya kudili ya masuala ya muziki, lakini kubwa kwake ni kuona ameshiriki kuzalisha wanamuziki wengi wa dansi na kuweza kuzalisha bendi kadhaa zilizochangia kuwainua kiuchumi kwa kuwapa ajira.

Anasema ukiziondoa bendi za Msondo Ngoma na Mlimani Park ‘Wana Sikinde’, hakuna bendi hata moja unakosa kuwakuta wanamuziki wanne au watano waliotoka katika bendi ya Twanga Pepeta.

“Kwa hiyo kuna vitu vingi sana ndio maana watu wameona kwamba ndani ya miaka hii 30 ambayo natimiza kwenye shughuli za muziki kifanyike kitu kuhusu mimi, ikiwa bendi inatimiza miaka 28 tangu kuanzishwa kwake,” anasema Asha na kuongeza;

“Hii ina maana kwamba mimi nilianza kujifunza burudani kabla ya Twanga Pepeta haijaanzishwa, na hata ile mikiki mikiki ya Twanga Pepeta iliyokuwa inatokea unakuta niliweza kuihimili kwa sababu nilishaanza kuingia kwenye burudani miaka miwili kabla ya bendi kuanzishwa.”

ASH 01

MIAKA KABLA YA BENDI

“Ndani ya miaka miwili kuna kitu kilitokea ambacho kimenifanya kuwa jasiri, yaani hata zikitokea figisu figisu nakuwa naweza kupambana nazo, kitu hicho ni wakati kina Nyoshi El Saadat ambaye ni mwanamuziki, walichukuliwa na wenzie katika bendi yangu na mtu mmoja alikuwa shabiki sana wa muziki wa dansi akawachukua wote kwenye bendi na kuwapeleka Nairobi, ndio likatokea lile jina ambalo anatuma Nyoshi sasa hivi kwenye bendi ya Bogoss Musica, sema mtu huyo sasa hivi ni marehemu, hivyo yule mtu alipofariki ilibidi kina Nyoshi El Saadat warudi Tanzania,” anasema Asha.


KUPORWA WASANII

Asha anapoulizwa kitu gani anachojutia ndani ya miaka 30 ya shughuli zake za muziki naye anajibu kwa upole;

“Kujutia hakukosekani katika muziki na muziki ni matukio tu, kama hivyo unaweza kuchukuliwa wanamuziki wako, yaani wanaibwa hadi unajuta kwanini imejiingiza kwenye hii biashara, lakini kutokana na ujasiri nilionao napambana nao hadi mwisho.

“Kitu kingine unaweza ukapelekwa polisi tu ukakaa ndani bila sababu kisa bendi anamiliki mwanamke kwanini anakuwa juu, yaani utakuta mtu anafanya figisu anakupa kesi wala sio yako, na akikupa kesi sio yako unaenda polisi na polisi wakija kugundua huna kesi wanakuachia, lakini ndio unakuwa ushalala polisi,” anasema Asha.

ASH 02

MUZIKI BADO

Yapo madai kwamba muziki wa dansi umeshuka, lakini kwa Asha Baraka ni tofauti, mwenyewe anasema muziki bado upo ila promosheni ndio imepungua kwa sababu vituo vya redio vimejikita katika muziki wa kizazi kipya hususani singeli na bongofleva.

“Kwanza muziki wa dansi hauwezi kuporomoka, unaweza ukashuka kidogo kwa asilimia lakini sio asilimia mia, nikisema hivi namaanisha muziki wa dansi kwanza nyimbo zake hazifi, leo hapa Twanga Pepeta wakipiga wimbo wa Kisa cha Mpemba, uliotengenezwa mwaka 1999 ukipigwa ni kama wa juzi tu,” anasema na kuongeza;

“Licha ya kuwa ni wimbo wa albamu ya kwanza ya Twanga Pepeta, lakini unapigwa jukwaani na watu wanacheza hapo ndio uone sasa muziki wa dansi unavyosimama hata nyimbo nyingine kama Jirani, Kuolewa, Aminata, Mtu Pesa, zikipigwa bado watu wanajazana kwenye kumbi wanacheza uzuri ni kwamba na muziki unapigwa live watu wanacheza live.

“Na niseme tu watu walianza kuona muziki wa dansi umeshuka kipindi cha Uviko 19. Baada ya uviko kuisha muziki ukaanza kusimama, nasema hivi kwa sababu wakati huo kulikuwa hakuna misongamano ya watu ili kuepusha lile balaa lililoikuta dunia.

“Kitu kingine ninachoweza kusema, ni mimi kutotengeneza media na TV, lakini nilijaribu ila kuna watu walinikwamisha kitambo sana nilianza kushughulikia ili niwe na media yangu na lengo kubwa ilikuwa ni kusapoti muziki wa dansi, sababu dansi bila media hakuna kitu,” anasema Asha.

Pia amewapa makavu wanamuziki wa dansi kuhusu kutumia mitandao ya kijamii, kwani imechangia kurudisha muziki huo nyuma kulinganisha na wenzao wa miondoko mingine.

“Wanamuziki wa dansi asilimia kubwa hawaitendei haki mitandao ya kijamii kwa ajili ya kusapoti huu muziki wa dansi, ukweli katika hili suala wanahitaji elimu sana ili waweze kupata ufahamu wa faida ya mitandao ya kijamii kwa matumizi ya kazi zao.

“Yaani utakuta mtu hata kuposti kazi zake kwenye mitandao haposti na wengine hadi sasa wala hawana akaunti za mitandao, inatakiwa watambue hakuna kazi isiyoonekana mfano mimi kiongozi wa Twanga Pepeta, Chaz Baba haposti chochote katika mitandao, yaani hii nasema kwa ujumla pia wanamuziki wa dansi wanajiangusha wenyewe.

“Hali ni tofauti na wasanii wa Bongofleva na miondoko mingine, wanachangamkia mitandao sababu wale wanafanya kazi binafsi wanajiajiri wenyewe, lakini muziki wa dansi mfano Twanga Pepeta watamtegemea Asha Baraka au watategemea wataonekana katika akaunti za bendi, lakini hata hawajui kama ipo siku mtu atatoka Twanga Pepeta.

“Leo nikiongozana na mwanamuziki wa dansi barabarani utashangaa naitwa mimi, sasa unajiuliza mimi naimba? Lakini hii inatokana na kazi yangu ya kufanya jitihada, watu wanifahamu” anasema Asha.

ASH 03

USAJILI WA CHOKI

Asha anasema katika miaka yake ya 30 ya kuwa katika muziki, hakuna usajili uliomkuna na kubaki kichwani mwake kama ule ya Ally Choki.

“Katika sajili zote nilizowahi kuzifanya kwenye bendi ya Twanga Pepeta, zote ni nzuri ila kiboko ilikuwa ya mwanamuziki Ally Choki, sababu mimi nilikuwa nasajili wanamuziki na wanaondoka, na wanamuziki wa kwanza kuwasajili walikuwa Luiza Mbutu na Jesca Charles, BanzaStone (sasa marehemu), baada ya Banza Stone kwenda T.O.T, ndio nikafanya usajili wa Ally Choki,” anasema Asha na kuongeza;

“Sasa huu usajili wa Ally Choki tukafanya mpambano wa Twanga Pepeta na T.O.T Band. Hapo Twanga Pepeta tuna Ally Choki na T.O.T wana Banza na hii haitawahi kutokea. Hii tulifanyia kwenye Ukumbi wa Vijana Social Kinondoni. Watu walikuwa wengi sana msafara wa magari kuingia ukumbini ulianzia kituo cha Mwanamboka, huu ndio usajili nilioufurahia sana yaani ulikuwa usajili na kumtoa mwanamuziki tulimuingiza Ally Choki kama mfalme.

“Hapo ndio tukawa tunamuingiza Ally Choki  ukumbini kwa matukio tofauti, mara akiwa kapanda farasi, mara Kijiko kwenye Ukumbi wa Diamondi Jubilee. Zamani kumbi zilikuwa nyingi tofauti na sasa hivi, zamani kulikuwa na Club Maisha, Billicanas, Leaders Club na nyingine na ndio maana watu sasa hivi wanasema muziki wa dansi umeshuka, kumbi ni chache kwa sasa. Dansi siku zile lilianzia Alhamisi, Ijumaa, Jumamosi na Jumapili,” anasema.

ASH 04

WALITOBOA KUPITIA TWANGA

“Kipindi hicho Leaders Club ilikuwa ndio inaongoza kwa kupandisha wasanii, wasanii wengi wa muziki na wa filamu wamepitia jukwaa la Twanga Pepeta, mfano kama Dully Sykes, Mr Nice, Diamond Platnumz walikuwa wanapanda jukwaani kuimba nyimbo zao tulikuwa tunatoka nafasi kwao, hata hii Bongo Movies imenyanyuka kupitia kwenye kumbi za dansi, mfano marehemu Kanumba, Ray Kigosi, Wema Sepetu Steve Nyerere wote hawa walikuwa wanakuja kwenye dansi na tulikuwa tunawapandisha stejini, kwanza mimi huwa nawashangaa watu wanaosema huyu Asha Baraka na Steve Nyerere vipi, yule tumetoka naye mbali kipindi anaanza kuonyesha vile vichekesho vyake pale Mango Garden tulikuwa tunampa nafasi Twanga Pepeta, na alikuwa hadi anaimba nyimbo za Twanga na tulikuwa tunasafiri naye,” anasema Asha .

ASH 05

INGIA TOKA TWANGA

Kumekuwa na wimbi la wanamuziki nyota kuingia na kutoka Twanga Pepeta kwa muda mrefu na hilo Asha analifafanua;

“Mimi nilichojijengea kwa wanamuziki ni uhusiano mzuri nao, na ndio maana mnaona wanamuziki wanaondoka na kurudi, hii ni burudani ambayo haitaki hasira, mwanamuziki anakuja anakaa anaangalia maisha akiona hapamfai anaaga anaondoka na huwa nawapa baraka zote za kuondoka ila nawaambia wakikwama warudi kwani hapa ni nyumbani,” anasema Asha, aliyeamua kumpa maua yake, Ally Choki kwa umahiri na kipaji kikubwa cha muziki alichonacho.

“Ally Choki ni mwanamuziki mzuri, ndiye aliyetunga nyimbo nyingi hapa Twanga Pepeta, hivyo hata akiondoka akirudi unaachaje kumpokea? Choki ni jembe yule sema tu hataki kutulia sehemu moja, na kinachomfanya asitulie ni pesa, anaweza akaja mtu akikwambia tu suala la pesa hivyo anatakiwa kuondoka, basi anapata wenge la kuondoka kumbe huyo mtu kazi yake ni ya muda tu, mwisho wa yote anarudi.

“Habari za kudaiwa kuwa huwa anaondoka sababu hapewi cheo sio kweli, tena hakuna wanamuziki wanaomheshimu Choki kama wa Twanga Pepeta, ila tu kama alitoka amerudi amekuta kuna viongozi wengine huwezi kuwaambia waache kuongoza apewe choki, hayo ni maneno tu ya watu huwa wanamchochea Choki tena hawa ni wanamuziki wenzie wa nje ya bendi, mara wamwambie asirudi kwenye bendi ataonekana siyo, maneno mengi anaambiwa, ila mimi namwambia asisikilize watu kwani Choki amefanya vitu vingi ndani ya Twanga Pepeta ametengeneza vingi hivyo muda wowote akitaka kurudi Twanga milango iko wazi mimi roho yangu nyeupe,” anasema Asha.


SIMBA WAJANJA

Asha anaizungumzia Simba anayoitumikia kama Mjumbe wa Bodi ya Wakurungenzi akisema inaenda na malengo waliyojiwekea kama klabu inayoendeshwa kisasa wakati inaendelea kumtegemea mtu mmoja.

Ukimuuliza ni vipi Mo Dewji mwenye asilimia 49 za umiliki wa klabu ndio aonekane akitoa pesa nyingi kuliko wanachama wenye asilimia 51, Asha anafafanua;

“Mimi ni mjumbe wa bodi ya Simba, na ni mjumbe wa muda mrefu nina miaka saba, ni kati ya wajumbe wa muda mrefu baada ya mabadiliko ya kiuwekezaji. Tukimzungumzia Mo Dewji kwanza ni mwanachama. Watu waelewe hivyo, ni mwanachama wa Simba, ni mtu ambaye anaipenda Simba sana sio yeye tu peke yake hadi familia yake. Kwa uwezo alionao Mo ana sababu zote kuisapoti Simba, kuidhamini na anatupa pesa kupitia brand zake tofauti kila mwaka, na Simba inapata mapato yake mengine kupitia sehemu tofauti sio kwamba Simba imekaa tu kumtegemea mtu mmoja na haiwezi kujitafutia.”


AISHTUKIA YANGA

Yanga imekuwa ikisisitiza kwamba haitacheza Dabi ya Kariakoo iliyokwama kupigwa Machi 8, licha ya Bodi ya Ligi kutangaza mechi itakuwa Juni 15, lakini kwa Asha ana mtazamo tofauti akidai watani wao wanataka kuwacheza shere.

“Nasemaje watacheza bana. Watacheza Yanga watacheza na wito wangu ni watu waende tu uwanjani Juni 15, Yanga na Simba. We unazijua vizuri? Hakuna cha kutoa taarifa wala nini mbona kuna taarifa ngapi mitandaoni huwa zinatolewa unadhani zote ni za ukweli?

“Hawa watacheza tu hatutaki propaganda zao, na hatutaki watukimbie yaani wapende wasipende watacheza, Bodi ya Ligi imetangaza mechi, nani atagoma wanakimbia kufungwa hao maneno mengi na ubingwa tunaubeba msimu huu,” anasema Asha ambaye alianza kuipenda Simba tangu akiwa sekondari hadi wakati akicheza netiboli katika timu ya Shirika la Bima la Taifa.


AHOUA, MPANZU

Asha anasema wachezaji wote waliosajiliwa msimu huu wakiwamo Charles Ahoua, Ellie Mpanzu, Moussa Camara na wengine anawakubali kwa uwezo walionao.

“Mimi naridhika na viwango vya usajili wa wachezaji wote wa Simba, na hata waliopo wenyeji, Simba hii ni bora huoni wachezaji saba wametangazwa kwenda kucheza timu ya Taifa

“Tukija kwa hawa waliosajiliwa, nawakubali sababu kila mchezaji mmoja amesajiliwa aisaidie timu na sio kushindana kumzidi mwenzake.Siwezi sema nani ni bora zaidi ya mwenzake wakati wanacheza nafasi tofauti kwa hawa wageni,” anasema Asha aliyefichua jinsi alivyoanza kuipenda Simba hadi kuja kuwa kiongozi kwa kusema;

“Mimi Simba iko kwenye damu, na nimeingia Simba nikiwa namaliza sekondari, na aliyeniingiza alikuwa Katibu Mkuu Jimmy David Ngonya sasa marehemu, kipindi hicho nacheza sana netiboli ndio alipoamua kuniingiza, akaunda timu ya netiboli, maana tulikuwa tunashinda klabu ya Simba muda wote, tulikuwa tunafanya mazoezi, na wakati huo Shirika la Bima kulikuwa na kitengo cha michezo, basi nimekua nayo, ndio maana huwa naumia sana Simba ikifeli katika michuano yoyote,” anasema Asha.


ANAJIGAWAJE?

Asha ni mama wa familia, kiongozi Simba na bosi wa Twanga Pepeta, alipoulizwa anajigawaje kumudu shughuli hizo zote kwa ufanmisi ikiwamo masuala ya kifamilia anasema;

“Watu wengi hawaelewi, sasa hivi mfumo mpya wa uwekezaji Simba inaendeshwa kama kiofisi, ina menejimenti, hivyo tunakutana miezi mitatu mitatu, na ikitokea mashindano tunapokezana, hawa wanaenda huku wengine huku hivyo napata muda mwingi sana wa kufanya mambo mengine ya familia na shughuli za bendi.”