Whozu, Billnass na Mbosso wafungiwa na Basata

Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limemfungia kujihusisha na sanaa msanii Whozu na kumtaka kushusha mara moja video ya wimbo wake wa ‘Ameyatimba’ kwenye digital platform zote kutokana na maudhui yalipo ndani yake.
Whozu amefungiwa kujihusisha na kazi za sanaa miezi sita na kutozwa faini ya Sh3 milioni kuanzia leo Novemba 4, 2023.
Basata imesema Whozu alichapisha video ya wimbo huo Novemba 2, 2023 akiwashirikisha wasanii wenzake Billnass na Mbosso ambao pia wametozwa faini ya Sh3 millioni na kutojihusisha na sanaa kwa miezi mitatu kila mmoja.
Wasanii hao wamekumbana na adhabu hizo baada ya wimbo huo kuwa na maudhui yanayokiuka kanuni za maadili kutokana na kuwepo ishara ya vitendo vinavyoashiria matusi kinyume na Kanuni ya 25(6) (j) pamoja na vitendo ya unyanyasaji, ukatili na udhalilisha wa utu wa mwanamke kinyume na Kanuni ya 25(6)-(f).
“Msanii huyu (Whozu) ameshaonywa mara mbili na kutozwa faini mara moja huko nyuma kwa kukiuka taratibu za kuzingatia maadili katika kazi za sanaa lakini bado ameendelea kupuuza,” imesema sehemu taarifa hiyo.