Wema: Tatizo watu hawanielewi

Muktasari:
- Wema ameliambia gazeti hili, watu wameona ametulia na kufanya mambo yake kimya kimya, wanaanza kumchokoza ili aseme maneno aonekane hana adabu.
BAADA ya kudaiwa kwa sasa amefulia ndiyo maana amecharuka kuposti matangazo kwa wingi katika akaunti yake ya Instagram ili apate pesa, msanii wa Bongo Movie, Wema Sepetu amefunguka watu wanaomsema hivyo watakuwa hawamuelewi vizuri.
Wema ameliambia gazeti hili, watu wameona ametulia na kufanya mambo yake kimya kimya, wanaanza kumchokoza ili aseme maneno aonekane hana adabu.
Anasema yeye sio mtu wa kwanza kuposti matangazo na watu wasimpangie cha kufanya katika akaunti yake kwani ana uhuru wa kuposti chochote.
“Naona watu wameanza eee.. wameshaniona nipo kimya nimetulia sasa wanataka niwakosee adabu, hivi mtu kuposti tangazo ndio kufulia au ndio kulipwa? Wanajuaje makubaliano yangu na ninaowapostia tangazo? Hawa wanaosema hivi ni watu ambao hawana shughuli za kufanya kutwa wapo kwenye peji za watu kutukana watu na kuwasema vibaya.
“Labda niwaambie tu, mimi sio mtu wa kwanza kuposti matangazo na nina uhuru wa kuposti chochote kwenye akaunti yangu, naomba uwaambie sitaki mjadala wa ovyo kwenye peji yangu, mwenyewe najua nini ninachofanya,” anasema Wema.
Hata hivyo, anasema hakutaka kuwafafanulia watu kwa kile wanachomsema, ila kaona awafunge midomo tu kuwa asilimia kubwa ya matangazo anayoposti ni sababu ya kupewa ubalozi wa kutangaza biashara za watu, sasa kwa nini asitimize wajibu ikiwa ameonekana?
“Sikutaka kuwafafanulia kwa nini naposti matangazo, mimi ni balozi wa hayo matangazo kwa watu wanaonifatilia wanafahamu hili, sasa mtu napewa heshima ya ubalozi wa kutangaza biashara ya mtu nakataaje sasa? Nitayaposti sana tu ila kama kuna tangazo halipo kwenye ubalozi basi wajue hayo ni maamuzi yangu tu kuposti,” anasema.
Afafanua ishu ya App kupooza
“Nimegundua kitu cha kuwaongezea watu kwenye App yangu, sababu kwa sasa kitu kikubwa kilichopo ni kipindi changu cha mapishi maarufu kama ‘Cook with Wema Sepetu’, kinachopatikana kwenye App na chaneli yake ya YouTube.
“Kitu ambacho nahitaji kukiongeza tutakuwa na ‘content’ mpya ya short films kwenye app, hivyo mashabiki zangu wakae mkao wa kunipokea na kula huku wakiendelea ku-subscribe tu,” anasema.
Huyu ndiye dizaina wake
“Aise mimi bana nafanya kazi na wanamitindo wengi sana ila nikitengenezewa vazi na Martin Kadinda huwa anafunika sana, yaani Martin ni kila kitu kwangu kwenye mambo ya mavazi na hajawahi kukosea, ndio maana akinitengenezea nguo lazima nitrendi sana na hilo vazi na watu wengi kunipongeza kwa kupendeza.”
Vipi kuhusu kupania sherehe
“Naona na kusikia watu husema mimi huwa napania kuvaa kukiwa na sherehe za watu, ukweli sijawahi kupania sherehe ya mtu, huwa inatokea tuu watu kuwa na nyota zetu na mwili wangu una damu ya nguo.”
Rangi ya nguo anayoipenda
“Napenda sana rangi nyeupe, sababu nimeona inanipendeza na kuimudu kwa usafi, mimi ni msafi napenda vitu visafi safi.”
Mwili anaoukubali huu hapa
“Naukubali mwili wa sasa hivi nilionao, sababu najiona ni mwepesi sana, ule mwili wa mwanzo wa unene unipitie mbali tu kwa kweli na wala siutamani.”
Wema wa kuanika kula bata na mpenzi wake hayuko tena
“Nayafurahia sana mapenzi yangu ya sasa ya kuweka ‘private’ matukio tunayoyafanya japo watu wanafahamu niko na Whozu, ila hawamuoni yule Wema wa kipindi cha nyuma, kila kitu anachofanya na mpenzi wake anaweka mitandaoni, kiufupi nimejifunza na kubadilika sana, hata wewe mwenyewe unaniona.”
Hataki urembo huu unamzeesha
“Kutumia vipodozi vikali, kuweka mawigi makubwa makubwa kichwani siyo kabisa, yanatuzeesha tu.”
Wema ni mtu wa namna hii
“Mimi ni mpole sana, halafu mkorofi mtu akinichokoza, pia napenda kupambana kwa kitu chenye malengo, napenda kupendwa na mpenzi wangu.”
Ushauri kwa Mama Samia
“Kwanza nampongeza sana Rais wetu mama Samia Suluhu Hassan, pia namwomba azidi kutupambania wasanii kuweza kufika mbali, niseme tu mama mitano tena.”