Chid Benz, Mwasiti katika ubora wa muda wote

Muktasari:
- Licha ya mengi yaliyotokea na yanayoendelea kumhusu, hakuna ubishi Chid Benzi ametengeneza muziki mzuri na kushiki kuinua wasanii wengi kupitia kolabo nyingi alizofanya miaka ya nyuma. Songa nayo.
Haikuwa kazi rahisi kwa Chid Benzi kutoka kuwa msaidizi wa Professor Jay jukwaani hadi kuishika Bongo Fleva kwa wakati wake na kuwakilisha vizuri kule anapotokea kupitia muziki wake wa Hip Hop ingawa mwazo alianza kwa kuimba.
Licha ya mengi yaliyotokea na yanayoendelea kumhusu, hakuna ubishi Chid Benzi ametengeneza muziki mzuri na kushiki kuinua wasanii wengi kupitia kolabo nyingi alizofanya miaka ya nyuma. Songa nayo.
1. Kwa mara ya kwanza Chid Benzi alishinda Tuzo za Muziki (TMA) 2006 kama Msanii Bora wa Hip Hop baada ya kufanya vizuri na wimbo wake ‘Naitwa Nani’ akimshirikisha K-Lynn, Miss Tanzania 2000 na mwimbaji wa zamani wa Tanzanites Band.
K-Lynn ambaye aliachana na muziki baada ya kutoa wimbo, She Ain’t a flirt (2009), alianza muziki mwaka 1997 katika bendi hiyo, aliimba hapo kama msanii na mmoja wa viongozi kwa kipindi cha takribani miaka miwili na nusu.
2. Moja ya nyimbo kubwa kutoka kwa Chid Benzi ni Dar es Salaam Stand Up (2011), huu ulitengenezwa katika studio ya Dully Sykes, Studio 4.12 na Prodyuza Pancho Latino kabla ya kutimkia Bxtra Records, zamani B’Hits Music Group yake Hermy B.
3. Kipindi Danny Msimamo anarekodi wimbo wake, Siku Nzuri (2004) pale Aigies Records kwa Complex, alikutana na Chid Benzi ambaye alikuwa anatafuta nafasi ya kutoka, kipindi hicho Chid anaimba na sio kurap kama alivyokuja kutambulika.
4. Mtayarishaji Allan Mapigo na Ruge Mutahaba ndio walimtafuta Chid Benzi na kumuomba kushiriki katika wimbo wake Marlaw, Bado Umenuna (2007), hiyo ni baada ya Ruge kuona uwezo mkubwa wa mwimbaji hiyo baada ya kufanya mazoezi pale THT.
Wakati huo tayari Marlaw alishafanya vizuri na wimbo wake, Bembeleza (2006) aliourekodi akiwa kidato cha sita mkoani Njombe na wimbo huo ndio ulimtangaza zaidi mtayarishaji muziki, Tuddy Thomas.
5. Kipindi Soggy Doggy anasaini makubaliano ya kununua gari lake la kwanza ambalo alitafutiwa na Mwana FA baada ya kupokea Sh6 milioni kama malipo ya mauzo ya albamu yake chini ya Bongo Records, Chid Benz ndiye alikuwa shahidi.
6. Professor Jay ndiye aliombwa kushiriki katika wimbo wa Tundaman, Neila (2006) ila akampendekeza Chid Benzi ambaye alikuwa na ukaribu naye, basi Chid akakubali na kuibuka Baucha Records na Bob Manecky alikuwa anafanya kazi wakati huo.
7. Basi alipoweka vesi yake tu katika wimbo huo ukafanya vizuri na kumtoa kimuziki, baadaye Tundaman akajiunga na kundi la Chid, Lafamilia kisha kutimkia Tip Top Connection baada ya kupewa ofa nzuri.
Na wimbo huo ndio ulibeba jina la albamu ya kwanza ya Tundaman, Neilah (2007) kisha ya pili, Nipe Ripoti (2009) na ndio uliompa show ya kwanza kulipwa fedha nyingi akichukua Sh400,000.
8. Chid Benzi ni miongoni mwa wasanii wachache Bongo walioushirikishwa katika nyimbo za mahasimu wawili kimuziki, Diamond Platnumz (Nalia na Mengi) na Alikiba (Far Away), na ni kabla wasanii hao kuwa na majina makubwa kama ilivyo sasa.
9. Katika wimbo wake, Pisha (2009), Chid Benzi anajitambulisha kama Busta Rhymes wa Tanzania, wakati Gigy Money katika wimbo, Good Time (2018) aliyoshirikishwa na RJ The DJ anajitambulisha kama Cardi B wa Tanzania.
10. Kolabo bora ya Chid Benzi kwa muda wote ni yake na Mwasiti, Hao (2007) iliyotengenezwa na Lamar wa Fishcrub lakini Ruge aliyekuwa anamsimamia Mwasiti hakuikubali, hivyo ilikaa sana ndani ila ilipokuja kutoka ulifanya vizuri sana.
Ikumbukwe Mwasiti amekuwa kipenzi cha muziki wa Hip Hop, miongoni mwa wasanii wa Rap aliowahi kuwashirikisha kwenye nyimbo zake Quick Rocka (Sio Kisa Pombe), Godzilla (Soldier & Leo), Billnass (Bado) na Roma (Fall in Love).