Wameshea love, sasa mashosti

Muktasari:
- Majina yao yamehusishwa na wanawake zaidi ya watano na kuonekana kushea penzi kwa mastaa hao huku kukizuka mtafaruku, lakini baadaye wakawa marafiki.
ACHANA na muziki wao, ni wazi umaarufu wa Diamond Platnumz na Harmonize ulichangiwa pia na uhusiano wao kwa wanawake mbalimbali maarufu kutoka kiwanda cha mitindo, muziki na filamu.
Majina yao yamehusishwa na wanawake zaidi ya watano na kuonekana kushea penzi kwa mastaa hao huku kukizuka mtafaruku, lakini baadaye wakawa marafiki.
Hawa hapa wasanii maarufu walioshea penzi na Diamond au Hamornize na kujenga uadui kabla ya baadaye kuwa marafiki.

Wema Sepetu na Hamisa Mobetto
Wema na Hamisa inadaiwa walishea penzi la Diamond na kusababisha vita baina yao na kushindwa hata kusalimiana wanapokutana sehemu mbalimbali ikiwamo za starehe.
Diamond alianza na Wema kabla ya kuachana naye akajiweka kwa Hamisa na baada ya kuachana ukimya ulitawala baina ya wanawake hao.
Hata hivyo, kwa sasa hawana bifu na ni marafiki huku kila mmoja akiendelea na maisha yake bila Diamond.
Kajala na Wolper
Kajala na Wolper kwa nyakati tofauti wameshawahi kuwa na uhusiano na Harmonize na hilo lilisababisha kuangukia kwenye uadui mkubwa.
Harmonize alianza na Wolper kabla hajaolewa, walipoachana akaja kujihusisha na Kajala.
Asikwambie kitu sasa hivi wamekuwa marafiki kupitiliza, alipo Kajala kwenye sherehe humkosi Wolper wamekaa meza moja.

Tanasha Donna na Hamisa Mobetto
Inafahamika pamoja na wote kuzaa na Diamond, lakini Hamisa na Tanasha ni marafiki ambao wamekuwa wakipeana kampani na kutamani kuwakutanisha watoto wao, Dyllan na Naseeb Junior, Lakini hapo awali hawakuwa na urafiki huo kutokana na kupokonyana tonge mdomoni na Diamond alianza kuwa na Hamisa na kuzaa naye na baadae akawa na Tanasha kabla ya kuachana.

Tanasha Donna na Zari
Tanasha raia wa Kenya na Zari raia wa Uganda wote wamezaa na Diamond na wawili hawa baada ya kujijua wameshea penzi moja la Diamond, hawakuwahi kuwa na ukaribu.
Ndio wanawake wa Diamond walioiteka zaidi mitandao ya kijamii kwa kuzungumziwa baada ya kuzaa naye.
Hata hivyo, mwaka jana 2023, Zari alichapisha picha ya watoto hao watatu wakiwa pamoja na kueleza waziwazi upendo wake mkubwa kwao. Picha hizo ni Latiffa, Nillan ambao amezaa na Diamond na Nasseeb Junior ambaye Tanasha amezaa na Diamond.
Tanasha pia alishiriki picha hiyo na kueleza upendo wake kwa watoto hao kupitia ukurasa wa Instagram wa mtoto wake Naseeb Junior. Pia Zari na Tanasha mwaka jana walionekana pamoja wakiingia kwenye White Part Uganda kitu ambacho kilizua gumzo ya kuwa hawa watu wameelewana hadi kufikia kuwa marafiki wa kualikana kwenye shughuli zao.

Jacline Wolper, Wema Sepetu, Hamisa Mobetto
Hii ni kitambo kabisa kwa msanii wa filamu Bongo na pia mfanyabiashara, Jacline Wolper inadaiwa alikuwa mpenzi wa Diamond lakini waliachana katika mazingira ya kutatanisha.
Inaelezwa jambo hilo lilisababisha Diamond amtungie wimbo kutokana na jinsi alivyoumia.
Lakini kutokana na kutoonyesha na wivu Wolper yupo kiurafiki na Wema na Hamisa ambao waliwahi kuwa na husiano ya mapenzi na Diamond.

Hamisa Mobetto na Jokate Mwegelo
Hamisa na Jokate waliwahi kuripotiwa kipindi cha nyuma kutoelewana baada ya Jokate kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Diamond wakati akijua fika Hamisa na Diamond ni wapenzi.
Si kwamba Hamisa na Jokate walikuwa wanavimbiana tu pindi walipokuwa wanakutana katika ishu zao za urembo, bifu lao lilienda mbali zaidi lakini baadaye walikuja kuwa marafiki na kupeana madili ya urembo.
Jokate aliwahi kuwa na biashara ya nywele zake mpya zinalizofahamika kama Malaika kupitia brand yake ya Kidoti na aliwatumia warembo maarufu akiwemo Hamisa kwa ajili ya kutangaza.