Rayvanny, Marioo kuliamsha Kizimkazi

Muktasari:
- Mbali na bendi hizo kongwe na wasanii hao wa Bongo Fleva tamasha hilio litasindikizwa pia na makundi ya taarabu ikiwamo Jahazi Modern Taarabv na Zanzibar One huku Dulla Makabila na Sholo Mwamba watawakilisha singeli, mbali na michezo mbalimbali ikiwamo soka itakayonogesha siku hiyo.
MSIMU mpya wa Tamasha la Kizimkazi unatatarajiwa kufanyika Julai 19, huku wakali wa muziki wa kizazi kipya nchini, Rayvanny na Marioo ni kati ya watakaowasha moto sambamba na bendi kongwe za muziki wa dansi, Msondo Ngoma na Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde’.
Mbali na bendi hizo kongwe na wasanii hao wa Bongo Fleva tamasha hilio litasindikizwa pia na makundi ya taarabu ikiwamo Jahazi Modern Taarabv na Zanzibar One huku Dulla Makabila na Sholo Mwamba watawakilisha singeli, mbali na michezo mbalimbali ikiwamo soka itakayonogesha siku hiyo.
Tamasha hilo linaloenda sanjari na kaulimbiu ya ‘Kizimkazi Kumenoga’ ambalo mgeni rasmi atakuwa Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan lilitafanyika Mkoa wa Kusini kwenye Uwanja Mpya wa Suluhu Academy.
Mwenyekiti wa tamasha hilo, Mahfoudh Said Omar aliliambia Mwanaspoti, mbali na Rais Samia, pia viongozi na wageni mbalimbali mashuhuri na maarufu kutoka ndani na nje ya nchi wataudhuria tamasha hilo litakalopambwa pia na mechi ya mashabiki wa Simba na Yanga.
Omar alisema pia siku hiyo kutakuwa na mbio za ngalawa, baiskeli, bao, karata na zuma, huku kwa burudani ya muziki wapinzani wa jadi, Msondo Ngoma na Sikinde Ngoma ya Ukae zitaonogesha tamasha hilo mbali na muziki wa Bongo Fleva, Singeli na taarabu.
Katibu Mkuu wa tamasha hilo, Ahmed Abdulhamid Hamis alisema miradi ya maendeleo inayofungamana na Kizimkazi Festival itazinduliwa ndani ya siku hizo nane mbali na kongamano la nishati safi ili kuungana na championi wa nishati safi Rais Samia.
Hamis alisema kabla ya tamasha hilo kuanza kutakuwa na mafunzo ya siku sita ya ujasiliamali kwa wavuvi, wasanii, watalii na walimu kuanzia Julai 12.
“Pia kutakuwa na dua maalumu ya kumuombea Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi na Rais Samia itakayofanyika Mnazi mmoja Zanzibar,” alisema katibu huyo, huku muasisi wa tamasha hilio, Said Hamad Ramadhan alisema tamasha limekuwa kichocheo cha maendeleo katika mkoa huo wa Kusini.
“Limeongeza fursa mbalimbali za biashara na hata watalii kuja,” alisema Ramadhan.