Kuna tofauti ndogo kati ya Mondi na Jay Z!

Muktasari:
- Ni Jay Z ambaye mwaka 2019, Jarida la Forbes lilimtambua kama msanii wa kwanza wa Hip Hop duniani kufikia hadhi ya ubilionea akiwa na utajiri wa Dola 1 bilioni na sasa umeongezeka na kufikia Dola2.5 bilioni.
STAA wa Bongo Fleva, Diamond Platnumz amewahi kumtaja rapa wa Marekani, Jay Z kama kielelezo kizuri kwake (role model) upande wa biashara na amekuwa akivutiwa na mtindo wake wa maisha wa kutengeneza fursa na fedha nyingi nje ya muziki.
Ni Jay Z ambaye mwaka 2019, Jarida la Forbes lilimtambua kama msanii wa kwanza wa Hip Hop duniani kufikia hadhi ya ubilionea akiwa na utajiri wa Dola 1 bilioni na sasa umeongezeka na kufikia Dola2.5 bilioni.
Kwa Tanzania, Diamond anatajwa kama mwanamuziki mwenye mafanikio zaidi kimuziki na kibiashara, ingawa hajawahi kuweka wazi utajiri wake ni kiasi gani ila tunaweza kupata picha mara baada ya kuikata ripoti iliyodai utajiri wake ni Dola 5.1 milioni.
Licha ya mafanikio ya wanamuziki wao kimuziki, kibiashara na nguvu ya ushawishi walionayo katika mataifa yao, kuna eneo moja dogo ambalo wanatofauti ingawa historia ya maisha yao ya awali kama inataka kufanana.
Rapa Jay Z, mshindi wa Grammy 25, alizaliwa Desemba 4, 1969 huko Brookly, Marekani, katika maisha yake alipitia changomoto nyingi akiwa mdogo hasa pale baba yake mzazi, Adnis Reeves alipoachana na mama yake, Gloria Carter.

Kwa mujibu wa CBS News, nyumba za Marcy Project ambazo familia masikini zilikuwa zikiishi ndani ya Brooklyn na ndipo Jay Z alikulia, zilikuwa kwenye maeneo hatari na yenye uhalifu wa kutisha.
Hata hivyo, Jay Z baadaye alikuja kukutana tena na baba yake baada ya kufanikiwa kwenye muziki akiwa ametoa albamu, Reasonable Doubt (1996), walirejesha uhusiano wao kabla ya kufariki dunia mwaka 2003.
Ila haikuwa rahisi kutoka kimuziki, ilimbidi Jay Z kupambana huku na kule hadi kufanya kazi kwenye mgahawa ili kukusanya fedha za kurekodi na baadaye alifanikiwa kutoa albamu hiyo ambayo kwenye wiki yake ya kwanza sokoni uliuza nakala 500,000.
Wakati Jay Z anafikisha umri wa miaka 20, ndipo Diamond alizaliwa, hiyo ilikuwa Oktoba 2, 1989 katika Hospitali ya Amana, Dar es Salaam. Yaliyotokea kati ya Adnis na mkewe Gloria Carter, tunaweza kusema yanafanana yale ya familia ya Diamond kwa sehemu.

Akiwa mdogo wazazi wake (Abdul Juma na Sanura Kassim) walitengana, huku yakiwepo madai kuwa alitelekezwa na baba yake bila msaada. Hata hivyo, baada ya miaka mingi, Mama wa Diamond akaja kudai mzee Abdul sio baba mzazi wa Diamond bali ni baba mlezi tu!.
Baada ya kuhitimu Sekondari 2006, Diamond alijikita rasmi katika muziki ili kujaribu kutimiza ndoto zake. Ili kuhakikisha anafikia ndoto yake alifanya kazi mbalimbali ikiwepo kuuza mitumba, petrol station, kupiga picha na nyinginezo ili kupata fedha za kurekodi.
Hatimaye mwaka 2009, Diamond alitoa wimbo wake ‘Kamwambie’ ambao ulimtoa kimuziki na tangu wakati amekuwa akifanya vizuri. Mwaka 2010 alipata ziara (tour) ya kwanza kwenda Uingereza na ndio ukawa mwanzo wa mafanikio yake kimuziki na kiuchumi hadi sasa.

Baada ya miaka mitano ya kufanya vizuri, Diamond alianzisha rekodi lebo yake, WCB Wasafi ambayo imeshawasimamia wasanii kama Harmonize, Rayvanny, Rich Mavoko, Queen Darleen, Lava Lava, Mbosso, Zuchu na D Voice.
Mnamo Juni 2018, Harmonize kabla ya kujitoa WCB Wasafi aliandaa show yake ‘Kus Night’ na kusindikizwa na wasanii kadhaa wa Bongofleva akiwemo Ben Pol, Queen Darleen, Chin Bees, Nyandu Tozzy, Country Wizzy n.k
Wakati Harmonize akielekea kumaliza kutumbuiza, Diamond aliibuka kwenye show hiyo na kupanda jukwaani na kuanza kuimba pamoja nyimbo zao mbili, Bado (2016) na Kwangwaru (2018).
Sasa Diamond alipokaribia kumaliza shughuli yake jukwaani, alivua tisheti aliyokuwa amevaa na kuwarushia mashabiki wake kitu kilicholeta purukushani kutokana kila mmoja alitamani kuondoka na nguo ya staa huyo.

Kitendo cha kuwarushia mashabiki tisheti ndicho kinaleta utoafuti kati ya Diamond na Jay Z. Kivipi?. Januari 2009, Jay Z alitumbuiza kwenye tamasha la siku ya Ukimwi ikiwa ni pamoja na kuhadhimisha miaka 30 ya mfuko wa Healthcare Foundation (AHF).
Kabla ya Jay Z kupanda jukwaani, mwimbaji mwenye sauti ya aina yake, Alicia Keys, mshindi wa Gramm 17, alitangulia na kuanza kuwapa mashabiki burudani kwa kipiga kinanda pekee yake na kuimba live kama kawaida yake.
Baada ya dakika kadhaa, Jay Z alijumuika na Alicia Keys jukwaani na kuanza kutumbuiza pamoja wimbo wao maarufu ‘Empire State of Mind’ kutoka katika ya 11 yake Jay Z, The Blueprint 3 (2009) chini ya Roc Nation na Atlantic Records.
Mara baada ya Jay Z kumaliza kuimba vesi zake mbili za wimbo huo, aliamua kuvua koti lake na kumkabidhi mtu aliyekuwa pale jukwaani, hakuwarushia mashabiki wake kama alivyofanya Diamond ingawa anauza nguo. Na hiyo ndio tofauti yao!.
Ikumbukwe Jay Z akiwa na mwanzilishi mwenza wa Roc-A-Fella, Damon Dash walianzisha chapa ya mavazi, Roc-A-Wear mnamo 1999 ila 2007 waliiuza kwa chapa ya Rocawear ya Iconix Brand Group kwa dau la Dola204 milioni.
Hata hivyo, mwaka 2019 Jay Z alinunua tena hakimiliki kwa chapa hiyo kwa Dola15 milioni kama sehemu ya suluhu mgogoro wa kibiashara kati yake na Iconix Brand Group ambayo ni maarufu kwa mavazi ya mitaani kama jeans, jezi, viatu, kofia n.k.