TUONGEE KISHKAJI: Utabiri wangu kuhusu Tuzo za Wachekeshaji Tanzania

Muktasari:
- Tuzo za wachekeshaji Tanzania zinazoitwa Tanzania Comedy Award zilizinduliwa wiki hii. Tuzo hizo zimeanzishwa na msanii wa Bongo Fleva, Ommy Dimpozi kwa kushirikiana na Basata, Bodi ya Filamu na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na zinatarajiwa kufanyika mapema mwaka huu.
MIMI wala sio mtabiri, lakini natabiri; Tuzo za Vichekesho Tanzania zitajaa lawama kuliko tuzo zote zilizowahi kutolewa tangu tupate uhuru. Nitaeleza kwa nini lakini kwanza tukumbushane…
Tuzo za wachekeshaji Tanzania zinazoitwa Tanzania Comedy Award zilizinduliwa wiki hii. Tuzo hizo zimeanzishwa na msanii wa Bongo Fleva, Ommy Dimpozi kwa kushirikiana na Basata, Bodi ya Filamu na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na zinatarajiwa kufanyika mapema mwaka huu.
Nasema zitakuwa na lawama kwa sababu nyingi lakini hizi ni chache.
ASILI YA KOMEDI
Tanzania haitakuwa ya kwanza kuanzisha tuzo za comedy duniani. Mataifa mengine tena yaliyoendelea na kututangulia kwenye tasnia ya burudani na sanaa yamewahi kuanzisha tuzo za wachekeshaji pia, lakini zote hazikufanikiwa kuendelea, ziliishia njiani huku sababu kubwa ikiwa ni asili ya comedy.
Wazungu wanasema, ‘Comedy is subjective’, yaani mtu ambaye anacheka comedy za Eliudi anaweza kuwa hachekeshwi kabisa na comedy za Leonardo na kinyume chake. Hata kwenye sanaa zingine hali hii ipo, lakini uzuri ni kwa mfano kwenye muziki, wimbo ukiwa hit song ni hit song tu, utapigwa kila redio, utachezwa na kila bodaboda na utadumu muda mrefu sokoni, lakini kichekesho ni tofauti.
Kichekesho kikiwa kikali, kitakuchesha muda huu, utacheka, utaendelea na mambo mengine. Hakitapigwa kwenye redio mwaka mzima, wala hutakizama kwa hata wiki mbili mfululizo.
Kwa hiyo kitakachotokea ni, malalamiko yatakuwa mengi kwa sababu kila mtu ana mchekeshaji wake anayempenda, kila mtu ana aina ya vichekesho anavyovipenda. Matokeo yake ni, kila mtu atadhani anachokipenda ni bora na kinastahili ushindi. Itakuwa malalamiko kulia, kushoto, chini, juu, katikati. Kila upande.
VIPENGELE VYAKE
Baadhi ya vipengele vya tuzo hizi vina ukakasi. Tuanze na Best Chawa of The Year.
Naelewa lengo la waandaji. Waandaji walikuwa wanatamani tuzo iakisi tasnia yao. Wao kazi yao si kuchekesha kwa hiyo wanadhani wanaweza kuwa na vipengele vya mzaha mzaha. Lakini wanachosahau ni, unapotengeneza tuzo unatengeneza msingi wa tasnia, unachora ramani ya uchekeshaji. Sasa Je, kwa kuwa na kipengele cha Best Chawa of The Year huoni kama inadogosha tasnia nzima? Vuta picha wasanii wamefanya utafiti kutafuta na kuandika vichekesho vyao, kisha wanakuja kupata tuzo moja na Mwijaku, mtu ambaye anapata tuzo kwa sababu tu alikuwa anasifia matajiri na viongozi, kweli jamani. Labda wana picha kubwa ambayo hatuioni. Ngoja tusubiri.
Lakini, kipengele kingine chenye ukakasi ni Funny Leader of the Year. Yaani kipengele ambacho kinamtunuku tuzo kiongozi ambaye alikuwa ni mcheshi. Nina maswali mengi. Kwa nini kiongozi? Kwa nini sio mcheza soka mcheshi au kwa nini sio mhasibu mcheshi? Nanusa uchawa kwenye hiki kipengele.
Lakini shida kubwa nyingine ni, waandaaji wa tuzo wanatakiwa watambue kitaalamu mcheshi haina maana wewe ni mchekeshaji. Nadhani kila mtu anaye rafiki yake ambaye ukikaa naye akikupigia stori utacheka balaa, lakini tunakubaliana rafiki yako huyo huyo ukimchukua ukamtupa Cheka Tu au ukamwambia atanegeneza clip hatoboi. Ninachosema ni, inabidi tuilewe sayansi ya ucheshi na tukabilane comedy ni taaluma, sio kuwa mcheshi. Hakuna haja ya kumtunuku kiongozi mcheshi kwenye tuzo za wachekeshaji.
YOTE KWA YOTE
Nadhani ni hatua nzuri. Nawapongeza wanaadaji kwa uthubutu. Tusubiri tuone baada ya tuzo kufanyika itakuwaje lakini huo ndo utabiri wangu. Malalamiko yatakuwa mengi.