Sukari ya Zuchu, ina utamu na uchungu!

Mapema wiki hii Staa wa Bongo Fleva, Zuchu aliandika rekodi kama msanii wa kwanza Afrika Mashariki kwa wimbo wake (Sukari) kufikisha ‘views’ milioni 100 katika mtandao wa YouTube ikiwa ni miaka minne tangu ametoka kimuziki.
Zuchu anakuwa wa kwanza kwa wimbo huo ambao hajamshirikisha msanii yeyote tofauti na ilivyokuwa kwa Diamond Platnumz na Harmonize ambao baadhi ya nyimbo zao zilipata namba hizo ila zilikuwa za ushirikiano.
Wimbo huo wa Zuchu wenye mahadhi ya Afro Pop, ulitoka rasmi Februari 19, 2021 ukiwa umetayarishwa na vichwa viwili, Trone na Lizer Classic ambaye ametengeneza nyimbo nyingi kubwa za WCB Wasafi kwa miaka zaidi ya saba.
Hadi sasa video za Bongo Fleva zenye ‘views’ zaidi ya milioni 100 YouTube, ni Yope Remix (2019) Diamond ft. Innoss’B, Inama (2019) Diamond ft. Fally Ipupa, Waah! (2020) Diamond ft. Koffi Olomide, Kwangwaru (2018) Harmonize ft. Diamond na Sukari (2021) Zuchu. Lakini rekodi hii ya Zuchu ambaye alitoka rasmi kimuziki mwaka 2020 baada ya kutambulishwa na WCB Wasafi akiwa ni msanii wa wa saba katika lebo hiyo, ina utamu na uchungu ndani yake.
Utamu ulianza 2021 pale video ya Sukari ilipoandika rekodi ya kutazamwa zaidi YouTube barani Afrika ukimaliza mwaka huo ikiwa na ‘views’ zaidi ya milioni 60, huku ukifuatiwa na ‘Essence’ ya Wizkid wa Nigeria iliyokuwa na ‘views’ milioni 53.
Hata hivyo, mwaka 2022 rekodi ya Zuchu ilivunjwa na Staa wa Nigeria, Rema kupitia video ya wimbo wake ‘Calm Down’ uliyomaliza mwaka ikiwa na ‘views’ zaidi ya milioni 300, huu remix yake akiwa na Selena Gomez ikipata ‘views’ milioni 190.
Zuchu alikuwa msanii wa pili wa WCB Wasafi na Afrika Mashariki kwa video yake kuongoza kutazamwa Afrika ndani ya mwaka mmoja baada ya Diamond kufanya hivyo na wimbo wake ‘Jeje’ uliotoka Februari 26, 2020 ukitengenezwa Kelpvibe wa Nigeria.
Ikumbukwe video ya Jeje ilimaliza mwaka 2020 ikiwa na ‘views’ zaidi ya milioni 40 na kuongoza Afrika, huku ikifuatiwa na video ya wimbo wa Staa wa Nigeria, Simi ‘Duduke’ iliyopata ‘views’ zaidi ya milioni 28.
Na kwa kuongezea tu, video ya Jeje iliyoongozwa na Director Kenny, inatazamiwa kuwa video ya kwanza ya wimbo wa Diamond aliyofanya pekee yake (bila kolabo) kufikisha ‘views’ milioni 100 ambapo kwa sasa ina milioni 94.
Rekodi ya Zuchu ina utamu Afrika Mashariki ila kwa Afrika nzima, ina uchungu kwake na mashabiki wake maana kuna nyimbo zimetoka hivi karibuni na video zake zimefikisha ‘views’ milioni 100 kwa miezi michache tu wakati ‘Sukari’ akichukua miaka mitatu!. Mathalani, video ya Tyla, Water (2023) ilichukua miezi mitatu tu kufikisha ‘views’ milioni 100, video ya Rema, Calm Down (2022) ilichukua miezi mitano ikiwa ni sawa na video ya Ayra Starr, Rush (2022).
Na ukumbuke video hiyo ya Rema ‘Calm Down’ hadi sasa ina ‘views’ milioni 580 ikiwa ndio video ya muziki kutoka kwa msanii solo (bila kolano) iliyotazamwa zaidi YouTube kwa muda wote barani Afrika.
Kwa ujumla inashika nafasi ya tatu, ikiwa imetanguliwa na ile ya Master KG, Jerusalema (2019) yenye ‘views’ 602, huku remix ya wimbo wake, ‘Calm Down’ ambao Rema kashirikiana na Staa wa Pop Marekani, Selena Gomez ikishika namba moja kwa ‘views’ milioni 833.
Uchungu mwingine katika rekodi ya Zuchu ni kwamba licha ya wimbo huo (Sukari) kufikia namba hizo, haujawahi kushinda tuzo yoyote ya kimataifa na hata zile za ndani kama Tanzania Music Awards (TMA)!.
Hiyo ni tofauti kwa nyimbo za wasanii wengine Afrika ambazo zimepata namba kama hizo, mfano ‘Water’ wake Tyla wa Afrika Kusini ulishinda tuzo ya Grammy 2024 ukiwa ni wimbo wa kwanza kushinda katika kipengele cha Best African Music Performance.
Utakumbuka wimbo huo wa Tyla uliingia chati za Billboard Hot 100 na kupanda hadi nafasi ya 21 na kumfanya Tyla kuwa msanii mdogo zaidi na wa pili nchini Afrika Kusini kuingia katika chati hizo baada ya miaka 55.
Nao ‘Calm Down’ wake Rema ambao una rekodi kama wimbo wa kwanza Afrika kupata ‘streams’ bilioni 1 katika mtandao wa Spotify, ulishinda tuzo ya MTV Video Music Awards 2023 nchini Marekani kama Best Afrobeats.
Ikumbukwe Rema aliyeanza muziki katika makanisani ya Alpha P, alianza kuipata umaarufu na wimbo wake, Dumebi (2019), na baadaye D’Prince alimsaini katika lebo ya Jonzing World ambayo ni kampuni tanzu ya Mavin Records inayomilikiwa na Don Jazzy.