Prime
Mobetto: Haachwi mtu nyuma, nasepa

Muktasari:
- Mrembo huyo na Aziz Ki walioana miezi kadhaa iliyopita wakati akiichezea Yanga ambayo ni bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Bara inaoyongoza msimamo wa ligi kwa pointi 73.
SAA kadhaa baada ya mumewe, Stephanie Aziz KI kuondoka nchini kwenda kujiunga na klabu ya Wydad Casablanca ya Morocco, Hamisa Mobetto amefunguka.
Mrembo huyo na Aziz Ki walioana miezi kadhaa iliyopita wakati akiichezea Yanga ambayo ni bingwa mtetezi wa Ligi Kuu Bara inaoyongoza msimamo wa ligi kwa pointi 73.
Mobetto ameliambia Mwanaspoti jijini Dar es Salaam kuwa hakuna kinachomzuia kwenda kuungana na mumewe nchini Morocco na kusisitiza kwamba haachwi mtu nyuma.

Kumekuwa na maswali miongoni mwa mashabiki wa soka na sanaa kama endapo ataenda mlimbwende huyo na mumewe atahamishia maisha Morocco au ataendelea kubaki Tanzania.
Mobetto amesisitiza kuwa atakuwa bega kwa bega na mumewe kwani ni halali yake na haachwi mtu kwani wameshakuwa mwili mmoja.
"Weee....haachwi mtu hapa nitabanana na mume wangu hadi mwisho. Nitaondoka naye popote atakapoenda nchini na Morocco tutakuwa wote," amesisitiza Mobetto na kukiri kwamba hakuondoka naye Mei 19 usiku kwani bado yupo Tanzania akijiandaa kwenda muda si mrefu.

"Sijaondoka bado nipo, ila muda siyo mrefu nitamfuata alipo mume wangu kwa sababu nina haki zote za kuwa naye karibu, popote atakapokuwa na haachwi mtu kama baadhi ya watu wanavyosema.
"Naona kwenye mitandao kila mmoja anasema lake, mara ndoa itavunjika mara nimeachwa. Kwa nini watu wasifanye mambo yao na wakaniachia ndoa yangu? Niwaambie tu watasubiri sana kwangu."
Mwanaspoti ilitaka kujua ni namna gani atafanya kazi zake akiwa ni balozi wa kampuni nyingi hapa nchini, ambapo amesema hakuna kizuizi chochote kitakachomzuia kwani dunia yote kwa sasa ipo kiganjani.

"Kuwa Balozi siyo ishu mbona wapo watu ni balozi Tanzania na hawaishi Tanzania? Hivyo hata mimi naweza kufanya kazi zangu kama kawaida na kwenda nchi nyingine siyo kikwazo cha kampuni ninazofanyia kazi au biashara zangu zishindwe kuendelea," amesisitiza Hamisa.