Diamond Platnumz: Lavalava yupo huru kuondoka Wasafi

Muktasari:
- Mkali wa muziki wa Bongofleva, Diamond Platnumz amesema Lavalava yuko huru kuondoka WCB
Baada ya kuwapo kwa tetesi kuhusu msanii Lavalava kuondoka katika lebo ya WCB, Diamond Platnumz ameweka wazi akisema msanii huyo yupo huru kuondoka.
Diamond ambaye anamiliki Lebo ya Wasafi, amezungumza na waandashi wa habari leo Mei 21, 2025 akisema, Lavalava bado hajamfuata kumwambia kama anataka kuondoka kwenye lebo, ila amewaambia watu wake kwamba kama atataka kutoka basi awe huru kuondoka na hatamlipisha pesa yeyote.
"Najua watu wengi wanataka kufahamu kuhusu Lavalava kuondoka WCB, labda niwaambie tu Lavalava hakunifuata kusema kama anataka kutoka, ila mimi nilimpigia simu Kim nikamwambia kama Lavalava anaweza kutoka atoke tu yupo huru kuondoka, anaimba vizuri anajituma hajawahi kunivunjia heshima hata siku moja, hata jana nilikuwa naye nyumbani nikamwambia, kama anataka kujisimamia mwenyewe basi aje nitampa pesa kiasi cha kuanzia huko aendako," amesema.
Diamond ameendelea kusema, kuwa hategemei pesa kutoka kwa wasanii wa WCB, hivyo kwa upande wake kama msanii ameishi naye vizuri anaweza kumruhusu aondoke bila kulipa chochote, lakini msanii akimkosea na wakati yeye hajamfanyia baya lolote basi msanii lazima alipe pesa.
"Watu waelewe hili, ukiona mtu nimetoza hela pindi anapotaka kutoka kwenye Lebo yangu, basi jua umenikosea adabu, sababu mimi sitegemei hela ya msanii, kwa sababu nawachukulia kama familia yangu, mfano kama Mbosso nimeishi naye vizuri sana na ana adabu na ndio maana sikutaka kumlipisha pesa yeyote, hebu angalia shoo ya Mbosso kwasasa ni Sh milioni 250, kwanini nisiseme nimkate nichukue milioni 150 kwakuwa nimewekeza pesa nyingi? Ni kuamua tu kuachana nao."
Aidha, Diamond amesema watu wengi wanasema anasaini wasanii ili wamuandikie nyimbo, ila kiuhalisia yeye ameshiriki kuandika nyimbo nyingi za wasanii wa Wasafi na nje ya Wasafi.
"Watu wengi huko nje wana imani nimesaini wasanii ili wanitungine nyimbo, kwa taarifa tu mimi nimetunga nyimbo za wasanii wa WCB wengi sana siwezi tu kuwataja, na wapo wengine wasanii wa nje ya WCB wa hapa Bongo, mimi sio msanii wa kuimbaimba tum watu hawafahamu, mimi nikishika peni naweza kukuandikia wimbo wa aina yeyote ya dansi, mduara, taarab, singeli na bongofleva," amesema.
Lavalava alipozungumza, aliweka wazi kuwa bado yupo Wasafi na kama ataondoka kwenye lebo hiyo, mashabiki zake watafahamu kupitia page zake, ila kwasasa bado yupo Wasafi.
"Mashabiki wangu wafuatilie page zangu, nitawaambia mimi si mtu wa chini, nipo wazi sana," amesema Lavalava.