Quick Rocka akabidhiwa mshindi wa BSS 2019, Ritha aomba radhi

Muktasari:
Zawadi alizokuwa apewe mshindi Meshack Fukuta ni Sh30 milioni na kati ya hizo Sh20 milioni zilipangwa kuwekezwa katika muziki wake ikiwemo kumuingiza studio na kumtafutia menejimenti ambayo itamsimamia mwaka mzima.
Msanii wa Bongo Fleva, Quick Rocka ametangazwa rasmi kuwa meneja mshindi wa shindano la Bongo Star Search (BSS) 2019, Meshack Fukuta.
Hilo limeelezwa jana Jumapili Agosti 16, 2020 na Mkurugenzi wa BSS, Ritha Paulsen katika uzinduzi wa shindano hilo msimu wa 11 uliofanyika Jijini Dar es Salaam.
Pamoja na mambo mengine, Mkurugenzi wa mashindano hayo, Ritha Paulsen, amesema tayari wamemalizana na msanii huyo kuhusu zawadi pamoja na kumtafutia menejimenti ya kumsimamia kazi zake kama walivyoahidi.
Akizungumzia kuhusu hatua hiyo, Meshack amesema amefurahi kumpata meneja ambaye ni mtu sahihi katika soko la muziki kwa sasa.
"Unaweza kuwa msanii mzuri,lakini mwisho wa siku ukatunga nyimbo zako na kuzirekodi ukabaki nazo ndani kama huna mtu wa kukushika mkono.
"Kwangu kaka yangu Quick Rocka ni mtu sahihi,nina imani kwa ushirikiano wetu nitaweza kufika ndoto zangu za kuwa msanii mkubwa na hatimaye kuibua wengine kama nilivyoinuliwa mimi,"amesema.
Kwa upande wake Quick Rocka au Switcherbaba amesema tayari msanii huyo amemaliza kurekodi baadhi ya nyimbo na hivi karibuni anajipanga kuachia EP yake.
Ritha pia alimuomba msamaha Fukuta kwa kitendo cha kuchelewesha zawadi zake.
Katika sakata hilo Mshindi Meshack Fukuta, kutoka mkoani Mbeya, Aprili mwaka 2020 aliibua gumzo baada ya kufikisha malalamiko yake serikalini ya kutokabidhiwa zawadi yake ambapo alieleza kila alipokuwa akifuatilia alikuwa akipigwa danadana.
Jambo hilo lilimuibua Naibu Waziri wa habari,Utamaduni ,Sanaa na Michezo, Juliana Shonza kuingilia kati na kutoa maagizo kwa waandaaji ambao ni kampuni ya Benchmark Production kuhakikisha wanampatia mshindi huyo zawadi yake .
Zawadi alizokuwa apewe Meshack ni Sh30 milioni na kati ya hizo Sh20 milioni zilipangwa kuwekezwa katika muziki wake ikiwemo kumuingiza studio na kumtafutia menejimenti ambayo itamsimamia mwaka mzima.
Akizungumzia hilo, Ritha amekiri kuwa ni kweli ilitokea sintofahamu lakini wanashukuru wamelimaliza na kutumia nafasi hiyo kuomba radhi huku akiahidi kuwa halitajirudia.
"Hata sisi sio kwamba tulipenda kuchelewesha zawadi ya mshindi huyo,lakini kwa kuwa ilikuwa nje ya uwezo wetu hatukuwa na namna.
"Ni kutokana na changamoto hiyo tumejifunza mengi na tunaahidi halitajirudia tena,kwani maandalizi ya sasa tumejipanga vilivyo,"amesema.
Wakati kuhusu mashindano la mwaka huu ambayo kaulimbiu yake ni 'Mpya kubwa,na nusu' kaulimbiu, amesema litaanza kutimua vumbi Septemba kwa kusaka vipaji katika mikoa mitano.
Aliitaja mikoa hiyo kuwa ni Mbeya, Mwanza, Dodoma, Arusha na Dar es Salaam.
Akielezea mafanikio tangu kuanzia kwa mashindano hayo,amesema wameweza kuwafikia Vijana zaidi ya 50,000 na kubadili maisha ya vijana zaidi ya 200.
"Naomba serikali ituunge mkono katikankupata wadhamini,ili tuweze kufika maeneo mengi na kuwafikia vijana wengi zaidi na wadau kuungana nasi kuendeleza vipaji ambavyo tumeviibua badala ya kuona kuwa ni wasanii wa BSS.