Binti Msumi ‘wa Kombolela’ anayepitia changamoto za vibenten

Muktasari:
- Huyu ni Amina Kombo ‘Binti Msumi’. Wengi wanamfananisha uigizaji wake na mwonekano kama mkongwe Bi Mwendaikiwamo nafasi anazopewa ikiwamo ya ‘mama mchawi’.
NI mmoja wa nyota wa Bongo Movvie walioteka hadhira kubwa. Amejipatia jina hasa kutokana na kuigiza kama mke wa Mzee Kikala katika Tamthilia ya Kombolela.
Huyu ni Amina Kombo ‘Binti Msumi’. Wengi wanamfananisha uigizaji wake na mwonekano kama mkongwe Bi Mwendaikiwamo nafasi anazopewa ikiwamo ya ‘mama mchawi’.
Mwanaspoti kupitia ukurasa huu wa Dakika 5 Na... lilikutana naye maeneo ya Temeke Mtoni kwa Aziz Ally, jijini Dar es Salaam walipokuwa wakiandaa tamthilia ya Kombolela.
Katika mahojiano maalum, Binti Msumi amefunguka mengi kuhusu maisha yake na sanaa kwa ujumla.

Mwanaspoti: Una muda gani tangu uanze sanaa na imekunufaisha vipi?
Binti Msumi: Nimeanza sanaa ya uigizaji mwaka 1999 na kusema kweli imeninufaisha sana, nimesomesha na kujulikana na watu wengi.
Nilianza kwenye vikundi mbalimbali, hadi nilipoingia mkataba na kampuni ya Bichwa Production na nimeigiza tamthilia nne ambazo zipo YouTube na ndipo hapo mwandaaji wa tamthiliya ya Kombolela, Abdull Usanga aliponiona na kuniomba kuingia.

Mwanaspoti: Uliwahi kuigiza unapenda vibenten, vipi kwenye maisha ya kawaida?
Binti Msumi: Kwenye maisha ya kawaida mimi sipo hivyo ila kwa jinsi nilivyoigiza nilipata usumbufu wa wavulana wadogo wengi wakidhani ndiyo nilivyo.
Tamthilia ilikuwa inaitwa Vibenten, basi hivyo Vibenten vinanisumbua sana, yaani sijui kwa nini. Unakuta kijana kidogo kinakuja huku linang’ata ng’ata mdomo, mie naomba wanikome tu.

Mwanaspoti: Kwa sasa kwenye Kombolela unaigiza mwanamke mchawi, changamoto gani unakumbana nayo?
Binti Msumi: Kwa nafasi ya kuigiza uchawi kwangu imekaa vizuri kabisa na ndiyo nafasi niliyopangiwa na mwongozaji wangu, Abdull, ila siyo mambo yangu ya uchawi, hata nilipokuwa naigiza kwenye kampuni ya Bichwa production nilianza kucheza nafasi ya uchawi kwenye familia ya mzee kicheche na nikaja kucheza uchawi kwenye Sahani na sasa kwenye Kombolela. Ukweli napata changamoto nyingi sana kwenye hii nafasi, unajua siyo kazi rahisi kutembea mtaani wengine wanasema mimi mchawi. Kazi ya uchawi siyo kazi rahisi kwa kweli, ila ndio hivyo ni kazi.

Mwanaspoti: Watu wengi wanakufananisha na Bi Mwenda, wewe unajisikiaje?
Binti Msumi: Ni kweli huwa nafananishwa na Bi Mwenda ila sina undugu naye, na huwa nafurahi tu kufananishwa na mtu ambaye amenitangulia kwenye sanaa na amefanya mambo makubwa kwenye sanaa.
Mwanaspoti: Mashabiki wamekupokeaje mtaani
Binti Msumi: Wanajua binti Msumi mchawi na wengine wanajua na igizo ila pia wamenipokea vizuri kwani wengi ninaokutana nao hunipa hongera ya kazi ninayofanya.

Mwanaspoti: Kwa nini wasanii wengi wa filamu wanapenda maisha ya kujikweza kwa kujiona matajiri wakati siyo?
Binti Msumi: Nahisi filamu kwa kiasi kikubwa zinachangia hilo, maana mtu anaweza kuwa na maisha ya kawaida lakini akacheza tajiri na mwishowe maisha hayo ya kitajiri akahamishia kiuhalisia.
Mwanaspoti: Msanii gani una mkubali na amesababisha ujiingize kwenye sanaa?
Binti Msumi: Mimi najikubali mwenyewe tu.
Mwanaspoti: Vipi kuhusu familia, una watoto wangapi?
Binti Msumi: Nina watoto watatu, wajukuu tisa na nina mume, naishi Chamanzi, jijini Dar es Salaam.