Msafiri Diouf hataki ishu za unga

Muktasari:
- Diouf aliliambia Mwanaspoti, kwa sasa hataki kuzungumzia habari za nyuma kwani huwa anazijutia akizikumbuka kutokana na kupoteza vitu vingi katika maisha binafsi na yale ya muziki.
RAPA wa bendi ya Twanga Pepeta, Msafiri Diouf bado anaumia akikumbuka jinsi dawa za kulevya maarufu kama ngada a.k.a unga zilivyomharibia maisha.
Diouf aliliambia Mwanaspoti, kwa sasa hataki kuzungumzia habari za nyuma kwani huwa anazijutia akizikumbuka kutokana na kupoteza vitu vingi katika maisha binafsi na yale ya muziki.
"Yaani katika maisha yangu ya sasa huwa sipendi kabisa na nakuwa mkali mtu akiniuliza habari zangu za nyuma kuhusu utumiaji wa dawa za kulevya, sipendi na sitaki kukumbuka, maana hadi sasa huwa najutia sana, we acha hizi habari sizitaki kabisa.
“Kitu kikubwa ninashukuru kwa sasa nina maisha mengine kabisa yenye kumpendeza Mungu na niko vyema na familia yangu watoto wangu washakuwa wakubwa na ndiyo sababu mojawapo, pia sitaki vitu vijirudie wakaja kuviweka kichwani pindi watakapoanza kujitegemea," alisema Diouf.
Kwa sasa mwimbaji huyo amerudi Twanga Pepeta baada ya kuachana na bendi ya VDS aliyokuwa ameanzisha miezi michache iliyopita na baada ya miezi mitatu ikasambaratika.