P Diddy ana balaa, 120 wapya wajitokeza kesi yake

Muktasari:
- Rapa huyo, ambaye jina lake halisi Sean Combs, anakabiliwa na shutuma hizo kutoka kwa watu zaidi ya 100, huku wengi wao ni watoto, akifichua mwanasheria wa Texas, Tony Buzbee alipozungumza kwenye mkutano wa waandishi juzi Jumanne.
LOS ANGELES, MAREKANI: WATU wengine 120 wamejitokeza na tuhuma za kufanyiwa unyanyasaji wa kingono na rapa P Diddy, mwanasheria amefichua.
Rapa huyo, ambaye jina lake halisi Sean Combs, anakabiliwa na shutuma hizo kutoka kwa watu zaidi ya 100, huku wengi wao ni watoto, akifichua mwanasheria wa Texas, Tony Buzbee alipozungumza kwenye mkutano wa waandishi juzi Jumanne.
Alisema watu 25 miongoni mwao walikuwa watoto wakati wanadai walipofanyiwa unyanyasaji huo, akiwamo mtoto wa miaka tisa.
“Hili suala limezidi kuwa zito,” alisema Buzbee.
Mwanasheria huyo alisema yeye na timu yake watahakikisha wanatafuta ushahidi wote wa kutosha na hawataacha kitu juu ya shutuma hizo, ambazo Diddy amekana kufanya kosa lolote la kijinai.
Hata hivyo, timu ya wanasheria wa Diddy imezungumza na kukanusha madai ya Buzbee. Mwanasheria wake Diddy, Erica Wolff aliiambia Daily Mail: “Mr Combs amesisitiza na kukanusha taarifa hizo za uongo zilizolenga kumchafua kwamba hakumfanyia unyanyasaji wa kingono yeyote, ikiwamo watoto. Anasubiri kuwathibitishia kwamba hana hatia na kupanda mahakamani ambapo ukweli wote utathibitika, sio huu uvumi.”
Vijana wadogo zaidi wanaodaiwa kufanyiwa huo unyanyaji umri wao ulikuwa wa miaka 9, 14 na 15 wakati tukio hilo linafanyika. Mwanasheria, Buzbee alisema: “Kuna kijana mmoja alifanyiwa unyanyasaji na Sean Combs na watu wengine kadhaa kwenye studio kwa ahadi waliyopewa wazazi wake na mtoto mwenyewe kwamba anapata dili la kurekodi.”
Buzbee alidai kwamba kulikuwa na vijana wengine kwenye usaili na mmoja wao alikuwa mdogo zaidi, ambaye pia alikuwa kwenye mchakato huo wa kutafuta dili la kurekodi kwenye studio za Bad Boy Records, ambayo ilikuwa na wasanii kibao wenye majina makubwa akiwamo Notorious B.I.G., French Montana na Machine Gun Kelly. Kwa mujibu wa Buzbee, mtoto mmoja aliambiwa na Combs kwamba atamfanya kuwa staa mkubwa na kumtaka aende kwake akiwa pekee yake na kumlazimisha mtoto huyo kufanya naye ngono ya mdomo.
Mwathirika mwingine, ambaye alidaiwa kuwa na umri wa miaka 15 wakati anafanyiwa unyanyasaji huo, alisafiri hadi New York City kwenda kushiriki kwenye matamasha ya Diddy ambapo alipewa dawa za kulevya na kuingizwa kwenye chumba cha Mr Combs mahali ambako binti huyo akiwa mdogo alibakwa kabla ya wengine nao kumfanyia vitendo hivyo. Kwa mujibu wa Daily Mail, Buzbee alisema taarifa za vipimo zilionyesha wamepewa dawa za kulevya na kubakwa.