NLM ni zaidi ya ndoto kwa Rayvanny

Muktasari:
- Kwa wakati huo Alikiba bado alikuwa hajaanza kusaini wasanii chini ya Kings Music, naye alikuwa chini ya RockStar4000 ambayo sasa inatambulika kama RockStar Africa.
KATIKA wimbo wake, Natafuta Kiki (2016) ndipo kwa mara ya kwanza Rayvanny aligusia kuna siku ataachana na WCB Wasafi na kwenda kujiunga na lebo nyingine, Alikiba ambaye ni mmiliki wa lebo ya Kings Music kwa sasa ndiye aliyetajwa.
Kwa wakati huo Alikiba bado alikuwa hajaanza kusaini wasanii chini ya Kings Music, naye alikuwa chini ya RockStar4000 ambayo sasa inatambulika kama RockStar Africa.
Hata hivyo, bado Alikiba alikuwa ana nafasi ya kumsaini Rayvanny kama kweli angeondoka WCB Wasafi kama alivyoeleza kwani mwaka mmoja baadaye (Julai 2017) Alikiba alitangazwa kuwa miongoni mwa wamiliki wa RockStar Africa Entertainment Co.
Pia alichukua nafasi ya Director of Music and Talents chini ya RockStar Africa, Alikiba akiwa katika nafasi hizo ndipo alipomsaini Ommy Dimpoz kuwa chini ya RockStar Africa na yupo hadi sasa na kina Aslay, Young Lunya na Abigail Chams.
Vilevile Alikiba mwenyewe alionyesha kuupenda wimbo hao hadi kujirekodi video ikionyesha akiusikiliza, Rayvanny aliiambia XXL ya Clouds FM amekuwa akikutana na Alikiba na kumueleza anaupenda muziki wake.
Ikumbukwe video ya wimbo, Natafuta Kiki iliyotoka Agosti 31, 2016 ilishika nafasi ya 12 miongoni mwa video za muziki ilizotazamwa zaidi katika mtandao wa YouTube nchini Tanzania kwa mwaka 2016.
Katika mahojiano na kipindi cha Uhurufleva cha Uhuru FM, Oktoba 2016, Rayvanny alisema anaweza kuanzisha lebo yake akiwa chini ya WCB Wasafi kwani hakuna kizuizi, huku akitolea mfano wa Jay Z na Kanye West.
“Naweza nikawa na WCB na nikawa na lebo yangu lakini lazima niangalie, tunamuona Kanye West yupo kwa Jay Z lakini ana wasanii wake na vyote amefanya kutokana na nafasi yake, kwa hapa nilipo sishindwi kumsimamia msanii,” alisema Rayvanny.
Kwa wakati huo ndio alikuwa anaanza kuonja ladha ya mafanikio katika muziki, anaishi katika nyumba nzuri, huku WCB wakimpatia gari la kutembelea aina ya Toyota Rav4 baada ya kufanya hivyo kwa Harmonize aliyekabidhiwa gari aina ya Toyota Mark X.
Ndoto hiyo ya Rayvanny ilingoja hadi Aprili 2021, ikiwa ni miaka mitano tangu kuonyesha nia yake huyo, ila hakusaini kwa Alikiba bali alikufungua lebo yake, Next Level Music (NLM).
Septemba 2021 Rayvanny alimtambulisha msanii wa kwanza wa NLM ambaye ni Mac Voice, huyu anatambulika kama mjukuu wa Diamond Platnumz kwa sababu Rayvanny alianzisha lebo hiyo akiwa bado chini ya usimamizi wa WCB Wasafi.
Ikumbukwe Mac Voice kabla ya kusaini NLM, tayari alikuwa amesikika kwa kiasi fulani kwenye Bongofleva akiwa chini ya usimamizi wa Chege ambaye ndiye amlishika mkono kwa mara ya kwanza.
Muda mfupi baadaye Mac Voice aliweza kuachia EP yake, My Voice (2021) yenye nyimbo tano ambapo Rayvanny alishirikishwa katika nyimbo mbili, ‘Tamu’ na ‘Pombe’ zilizofanya vizuri zaidi.
EP hiyo ilifanya vizuri upande wa mauzo mtandaoni ambapo kwa kipindi cha mwenzi mmoja alichokuwepo Mac Voice kwenye muziki aliweza kuweka rekodi hizi kama ifuatavyo;
Mosi; kufikisha ‘streams’ milioni 1 kwenye mtandao wa Boomplay Music, pili; kufikisha ‘subscribers’ 100,000 YouTube, tatu; kufikisha ‘views’ milioni 4 YouTube, tano; kufikisha jumla ya ‘streams’ milioni 10 kwenye mitandao ya iTunes, Spotify, Boomplay, Play Music na Audiomack.
Nguvu ya muziki ilisababisha Mac Voice kuchaguliwa kuwania tuzo za African Entertainment Awards USA (AEAUSA) 2021 katika kipengele cha Best New Artist ambacho Rayvanny alikiwania mwaka 2016, na wote hawakufanikiwa kushinda tuzo hizo.
Julai 2022 Rayvanny akatangaza rasmi kuondoka WCB Wasafi na kuwekeza nguvu zake NLM, huyu ni msanii wa kwanza aliyetolewa na Wasafi kushinda tuzo nyingi za kimataifa ambazo ni BET 2017, Zikomo 2022, Afrimma 2022, EAEA 2022, DIAFA 2022 n.k.
Utakumbuka Rayvanny aliyeanzia muziki akiwa na Tip Top Connection kisha WCB Wasafi na sasa Next Level Music (NLM), ni msanii wa pili Afrika Mashariki kufikisha ‘views’ bilioni 1 katika mtandao wa YouTube akiwa ametanguliwa na Diamond, kisha Harmonize.
...