Prime
Kwa mastaa hawa, ni Kariakoo Dabi ya kwanza tangu...!

Muktasari:
- Dabi hii inavuta hisia za mashabiki wengi Afrika na kuacha kumbukumbu nyingi lakini itakuwa ya kwanza kwa baadhi ya mastaa wa muziki, mitindo na filamu Bongo wanaoshabikia timu hizo tangu kutokea matukio fulani muhimu kwao kama ifuatavyo.
Hatimaye ile siku ni leo. Haina kipengele. Wababe wa soka la Tanzania, Yanga SC na Simba SC wanakutana katika Dabi ya Kariakoo itakayopigwa dimba la Benjamin Mkapa ukiwa ni mchezo wa mzunguko wa pili Ligi Kuu Bara 2024/25.
Dabi hii inavuta hisia za mashabiki wengi Afrika na kuacha kumbukumbu nyingi lakini itakuwa ya kwanza kwa baadhi ya mastaa wa muziki, mitindo na filamu Bongo wanaoshabikia timu hizo tangu kutokea matukio fulani muhimu kwao kama ifuatavyo.

1. Tangu Hamisa Mobetto (Yanga) ameolewa
Akiwa maarufu katika mitindo na muziki, Hamisa Mobetto alihamia Yanga kama shabiki akitokea Simba, huko alimfuta mpenzi wake, Stephane Aziz Ki ambaye Februari 16 walifunga ndoa na kufuatiwa na sherehe kubwa na ya aina yake.
Hii itakuwa ni dabi ya kwanza tangu wawili hao kufunga ndoa, lakini imekuja kitofauti maana tayari Aziz Ki ameondoka Yanga na kujiunga na miamba ya Morocco, Wydad AC ambayo itashiriki michuano ya Fifa ya Kombe la Dunia la Klabu 2025.

2. Tangu Zuchu (Simba) ametoa albamu
Baada ya Zuchu kutoka tu kimuziki, alijipambanua kama shabiki wa Simba akitumbuiza katika matamasha mawili ya timu hiyo, sasa Novemba mwaka uliopita alitoa albamu yake kwanza, Peace and Money (2024) ikiwa na nyimbo 13 na hadi sasa inafanya vizuri.
Zuchu ambaye amekuwepo WCB Wasafi yake Diamond tangu Aprili 2020 alipotambulishwa rasmi, licha ya Bosi wake huyo kuhamia Yanga, yeye amebaki Simba ambayo sasa inausaka ubingwa kwa nguvu kubwa baada ya kuukosa kwa misimu mitatu mfululizo.

3. Tangu Jux (Yanga) amefunga ndoa
Hii ni mara ya kwanza Jux anashuhudia Yanga yake katika dabi ya Kariakoo akiwa na mwali ndani baada ya hapo Februari 8 kufunga ndoa na mpenzi wake kutokea Nigeria, Priscilla ambaye waliweka wazi uhusiano wao mnamo Julai 2024.
Utakumbuka Jux alishatoa wimbo, Shugga Daddy Yanga (2023) kwa ajili ya timu yake hiyo huku mwaka juzi akitumbuiza katika kilele cha Wiki ya Mwananchi, tamasha linaloandaliwa na Yanga kwa ajili ya kutambulisha wachezaji wa msimu mpya.

4. Tangu Whozu (Simba) kujitoa Too Much Money
Akiwa ametoa nyimbo mbili kwa ajili ya timu yake, Noma (2021) na Simba Yetu (2022), hapo Januari 26, Whozu alitangaza kuachana na Too Much Money, lebo ya muziki ambayo alifanya nayo kazi kwa takribani miaka mitano kwa mafanikio.
Staa huyo aliyeanza muziki akiwa Chuo cha Ushirika Moshi na kuja kuvuma na kibao chake, Huendi Mbinguni (2017), mara kibao ameshatumbuiza Simba Day na sasa analiombea chama lake ushindi akiwa kama msanii huru baada ya kuachana na Too Much Money.

5. Tangu Lady Jaydee (Yanga) kusaini Universal Music
Mwaka huu anaadhimisha miaka yake 25 katika muziki wa Bongo Fleva huku akiitazama dabi kwa mara ya kwanza tangu aliposaini mkataba wa kufanya kazi na lebo kubwa ya muziki duniani, Universal Music hapo Novemba 2024.
Hata hivyo, licha ya Lady Jaydee kutoa albamu 10 na kurekodi nyimbo zaidi ya 250, bado hajatoa wimbo maalum kwa ajili ya Yanga, timu iliyobeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara mara 30 ikiwa ndiyo kinara wa vikombe huku ikifuatiwa na Simba iliyotwaa mara 22.

6. Tangu Joti (Simba) kung'aa TCA
Katika tuzo za ucheshi, Tanzania Comedy Awards (TCA) 2025 zilizofanyika kwa mara ya kwanza, Joti aliyejizolea umaarufu kupitia kundi la Original Comedy, ndiye mchekeshaji pekee mkongwe aliyeng'aa zaidi akishinda tuzo mbili.
Hafla hiyo iliyofanyika katika Ukumbi wa The Superdom Masaki hapo Februari 22 huku Rais Samia Suluhu Hassan akiwa mgeni rasmi, Joti ambaye ni shabiki wa Simba alishinda kama Mchekeshaji Bora wa Mwaka na Mwigizaji Bora Mkongwe wa Mwaka.

7. Tangu Marioo (Yanga) kumheshimisha mwanae
Novemba mwaka uliopita Marioo aliachia albamu ya pili, The God Son (2024) ikiwa na nyimbo 17, ndani ya albamu hii kuna wimbo 'My Daughter' ambao ni maalum kwa ajili ya mtoto wake wa kwanza, Princesss Amarah aliyezaa na Paula.
Ukiachana na hilo, Marioo ambaye ni shabiki wa Yanga akiitolea timu hiyo nyimbo kama Yanga Anthem (2022) na Yanga Mabingwa (2023), hii inakuwa dabi yake ya kwanza tangu mwanae kutambulika kama mtayarishaji mkuu wa albamu hiyo, The God Son (2024).

8. Tangu Aunty Ezekiel (Simba) kupata mtoto wa tatu
Staa huyu wa filamu, Machi mwaka huu yeye na mpenzi wake Kusah ambaye ni mwanamuziki wa Bongo Fleva walijaliwa kupata mtoto wao wa pili ila akiwa wa tatu kwa Aunty Ezekiel ambaye mtoto wake wa kwanza alizaa na dansa wa Diamond, Mose Iyobo.
Aunty Ezekiel ambaye ni shabiki wa Simba na hata na Baba yake mzazi, Ezekiel Grayson 'Jujuma' aliwahi kuichezea timu hiyo miaka 1980 akitokea Yanga, awamu hii dabi ya Kariakoo imemjia kitofauti maana imekumta ndani akipata mtori na supu.

9. Tangu Nandy (Yanga) kushinda Trace
Katika tuzo za Trace 2025 zilizofanyika nchini kwa mara ya kwanza hapo Februari 26, Nandy kutokea The African Princess Label, alishinda kipengele cha Msanii Bora wa Kike Tanzania, huku Jux akishinda kama Msanii Bora wa Kiume.
Hii ni mara ya kwanza Nandy kushinda tuzo hizo kubwa Afrika, ni wazi furaha yake itabaki kuwa salama endapo timu yake ya Yanga ambayo ameshaitungia na wimbo itashinda dabi ya Kariakoo ambayo ni miongoni mwa zile tano maarufu Afrika.

10. Tangu Mbosso (Simba) kuondoka WCB Wasafi
Mwishoni mwa Januari kulikuwa na tetesi za Mbosso kuondoka WCB Wasafi, lebo aliyofanya nayo kazi kwa miaka saba baada ya kuachana na kundi la Yamoto Band ambalo alikuwepo na wenzake watatu, Enock Bella, Beka Flavour na Aslay.
Mbosso ambaye ni shabiki wa Simba baadaye alikuja kuthibitisha jambo hilo, hivyo hii itakuwa dabi yake ya kwanza tangu kuachana na WCB Wasafi ambayo imempa mafanikio makubwa kimuziki akitoa albamu moja, Definition of Love (2021) na EP moja, Khan (2022).