Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

LINEX: Muziki una mambo mazito

LINEX Pict

Muktasari:

  • Katika mahojiano na Mwanaspoti, anaeleza ukimya wake unatokana na kuandaa mradi mkubwa anaotarajia kuuachia mwaka huu.

MSANII wa Bongo Fleva, Sunday Mangu ‘Linex Sunday Mjeda’ amesema kuna mambo mengi yanaendelea katika maisha ya wasanii.

Katika mahojiano na Mwanaspoti, anaeleza ukimya wake unatokana na kuandaa mradi mkubwa anaotarajia kuuachia mwaka huu.

Anasema hana presha na ushindani sokoni, aina ya muziki anaoufanya ni kuhakikisha ndani yake unabeba ujumbe utakaocha funzo, faraja na burudani kwa shabiki.

Mbali na hilo anafafanua maana halisi ya majina yake la Sunday likitokana na kuzaliwa siku ya Jumapili, Mjeda aliwahi kujifunza kozi za kijeshi ingawa hakufanyia kazi badala yake aliweka nguvu katika muziki.

“Nyuma ya majina kuna uhalisia mkubwa anaokuwa anaubeba mhusika, kama ilivyo langu la  Sunday napenda sana kusoma Biblia na kusali, kuna haja wazazi kuzingatia hilo, wasiwape majina watoto wao kisa wamemsikia mtu maarufu ambaye hawajui maagano yake,” anasema.

LINE 01

SIKUWAHI KUSHANGAA KUWA MAARUFU

Anasema hakuna kilichobadilika katika maisha yake, kwani hakuwahi kushangaa kuwa maarufu, ni kitu alichokitengeneza, ndiyo maana hana skendo badala yake aliwekeza nguvu katika muziki unaoishi.

“Umarufu wangu ulitokana na kalamu, karatasi na kukesha usiku nikitunga nyimbo ambazo ni funzo katika jamii, zikipigwa zinaacha ujumbe kwa msikilizaji, zipo zinazoshauri ndoa, maisha ya upambanaji kama vijana,” anasema na kuongeza;

“Kipindi hiki nina maisha mazuri kwa maana ya watoto, mke na nimepata marafiki wengi ambao tunabadilishana mawazo ya kimaisha, huku nikiendelea na kazi zangu za muziki bila kushindana na mtu, ninachozingatia ni kuandika mashairi  yatakayosema na shabiki yangu.

“Mfano wimbo wa Moyo Wa Subira ulitokana na uchunguzi wa sababu za ndoa nyingi kuvunjika, kuna mstari niliusoma katika Biblia uliyosema mwanamke mpumbavu hubomoa ndoa kwa mikono yake mwenyewe, ingawa pia kuna wanaume wa aina hiyo, kisha nikaomba Mungu anipe maarifa zaidi ya kufafanya katika wimbo ambao niliuita Moyo wa Subira.”

Anatambua waliopandishwa juu na kupata umaarufu kupitia vipaji vyao kama mpira wa miguu, filamu, muziki wakishindwa kujiwekeza nje na kazi zao, majina yao yanaposhuka kila kitu kinashuka na kujikuta wanapata msongo wa maisha na wanakuwa hawajiamini wakihisi jamii haiwaelewi. 

“Wengi wanakumbana na changamoto ya afya ya akili inatokana waliishi maisha ya juu wakati wanatajwa kila sehemu baada ya umaarufu kushuka na kufilisika wanakuwa hawakubali uhalisia wao na kushindwa kuishi kwa kujiamini,” anasema na kuongeza;

“Nina mfano wa marafiki zangu wawili waliokuwa matajiri, wote walifilisika ila mmoja akakubali hali akawa anapanda daladala, anatembea kwa miguu huku akiwa anajitafuta upya na akarejea katika hali yake ya mwanzo,  wa pili akawa anaishi maisha feki hadi sasa ana msongo wa mawazo na hali yake mbaya kiuchumi, nashauri watu waishi uhalisia wao.”

LINE 03

CHIPUKIZI

Anasema wasanii chipukizi wanapaswa kutambua uwekezaji hauwezi kumaliza kila kitu na kipaji hakiwezi kujitosheleza, inahitajika nidhamu, bidii, muda wa kutosha, kuheshimu watu na pesa.

“Ndiyo maana kuna wasanii wamekuwa wakubwa baada ya kuonekana mitandaoni na hawana kitu, kuna wengine watu wamewekeza mamilioni ya pesa ila hawajui kuimba, nasisitiza kipaji kizingatie vitu nilivyovitaja,” anasema na kuongeza;

“Muziki ni mpana ukiachana na wasanii, kuna mameneja, wapiga picha, watayarihishaji (producer), waongozaji (direct), warembo wanaotumika katika video (video queen, video king), wanenguaji kuna watu wengi, ambao wanajipatia kipato cha kuzisaidia familia zao, hivyo lazima uheshimike kama kazi.”

Anasema habagui msanii wa kumsikiliza isipokuwa anavutwa na uandishi wenye tija ambao atajifunza kitu cha tofauti;

“Nawasikiliza wasanii wa sasa na zamani, studio tunakutana na wasanii wa kike wengi bado jamii haijawasikia, ila wana vipaji vikubwa, sauti zao za vibwagizo zinasikika katika nyimbo nyingi za wasanii wakubwa.”

LINE 02

FAMILIA WAIMBAJI

“Familia nzima ni waimbaji, wapo wadogo zangu ni wachungaji, mama zangu wote wanaimba, mdogo wangu anaitwa David anaimba nyimbo za dini, nikiwa  mdogo nikiumwa mama alikuwa ananiombea napona, hivyo na watoto wangu wote wanaimba,” anasema Linex anayeutaja wimbo  wa Kesho Yangu kuhusu maisha yake halisi, alipitia kipindi ambacho alikuwa na watu ila hawakuweza kutatua changamoto zake, alijihisi kama yupo msituni peke yake.


MUZIKI NA USHETANI

Kuna kipindi msanii wa kike na mtangazaji Vanessa Mdee, aliwahi kutamba na nyimbo kama Niroge, Moyo, Come Over, Hawajui moja ya mahojiano yake alikiri kupumzika kazi hiyo kutokana mambo ya kishirikina wanayofanya wanamuziki wengi ili wafanikiwe, jambo hilo analiunga mkono Linex.

“Alichosema Vanessa ni kweli kabisa kuna mambo ya kutisha tunayoyasikia wanayoyafanya baadhi ya wasanii, ngumu kuona uhalisia wa hilo ukiwa nje ya kazi hiyo ila vipo na ni halisi kwa wahusika na wana ulimwengu wao tofauti na tunavyodhani,” anasema na kuongeza:

“Wasanii wenzangu wajue muziki ni kazi kama kazi nyingine, anayepaswa kuabudiwa ni Mungu peke yake ndiyo maana kuna wakati naimba nyimbo za dini kama muumini wa kawaida na sikuyataka makubwa ili wasanii wamenipokea na wanasikiliza nyimbo zangu hiyo inatosha.”

LINE 04

BABA LEVO

Anasema anaishi naye kama familia ingawa hawawasiliani mara kwa mara kutokana na harakati za kutafuta ili familia zao ziishi maisha mazuri.

“Baba Levo ni familia ila harakati zetu wanaume huwezi ukawa unapigiana simu mara kwa mara kama hakuna ishu ya maana, ila akisikia nina changamoto anafika kwa haraka vivyo hivyo kwangu, namna anavyoonekana katika mitandao ya kijamii ni tofauti na maisha yake halisi ni mtu smati na mkweli, asiyependa kupindisha jambo,” anasema.


SHOO ZAKE

Anasema kwa sasa kuna wakati anakuwa anaimba live bendi za wasanii wenzake  Christian Bella na Barnaba Classic, kuimba katika matukio mbalimbali ya kitaifa ambayo yanamuingizia pesa.

“Kuna wakati nakodisha vyombo vya kupigia live nakuwa naimba kwa kifupi hizo ndiyo shoo ambazo nazifanya kwa sasa, ingawa wakati mwingine naalikwa nchi jirani katika matukio tofauti,” anasema.

LINE 05

SHABIKI WA YANGA

Anasema kwa Bongo anaishabikia Yanga na anatamani kumuona mshambuliaji Clement Mzize mwenye mabao 13 awe mchezaji bora wa msimu huu (MVP): “Akikosa sawa haikuwa bahati yake, ila kama mzawa anapambana na anaonyesha ubora katikakati ya wageni.”