Nguza: Wasanii wa sasa wanadeka

Friday February 19 2021
nguza pic
By Nasra Abdallah

MWANAMUZIKI mkongwe nchini, Nguza Viking amesema wasanii wa miaka ya karibuni wanadeka katika ufanyaji kazi.

Mkali huyo wa muziki wa dansi anayefahamika zaidi kama Babu Seya ameyasema hayo katika mahojiano maalumu na Mwanaspoti lililotaka kujua namna anavyouona muziki wa sasa akilinganisha na ule wa enzi zao.

Akizungumzia hilo, mwanamuziki huyo alisema wanamuziki wa sasa wanadeka na kufafanua kuwa wamerahisishiwa vitu vingi katika kufanya muziki wao, ikiwemo kutumia asilimia kubwa teknolojia ya kompyuta.

Pia aliongeza kuwa hata katika utungaji wao wa nyimbo ni watu ambao wamekuwa hawakai chini kuumiza vichwa kama enzi zao, badala yake mtu anaweza kutunga wimbo asubuhi kesho yake ukausikia redioni.

“Kwa sisi tuliofanya muziki siku nyingi ili kukamilisha wimbo wako itakuchukua wiki mbili au mwezi kwa kuwa tulikuwa tukifikiria sana tunaimba nini, kwa ajili ya kina nani na kwa nini,” anasema.

“Kitendo hicho kilitufanya tutumie muda mwingi katika kufikiria kutunga tofauti na wasanii wa sasa - wao siku moja ya pili wamekamilisha nyimbo.”

Advertisement

Katika upande wa wa vyombo vya muziki, Nguza anasema ilitakiwa kama ni ngoma ipigwe kweli, tumba ipigwe kweli, lakini hivi sasa vyote hivyo vinapatikana kwenye kompyuta.

Alieleza kuwa licha ya hivyo kukua kwa teknolojia katika tasnia ya muziki kumewarahisishia kazi. Hata hivyo, alisema pamoja na teknolojia hiyo, wasanii bado wanatakiwa kuumiza vichwa kuja na tungo nzuri zinazokuwa na faida kwa jamii na pia zitakazowasaidia kuzifanya ziishi muda mrefu.

“Fikiri kama kibao cha Seya nilichokiimba miaka mingi iliyopita hadi leo nakitumia katika kuniingizia hela, na kikipigwa mahali lazima watu wasimame, sio muziki wa vijana wa sasa, siku mbili watu wameuchoka, wabadilike,” alisema.

Advertisement