MKOJANI 1 - Kuchekesha barabarani kulivyomtibulia mambo

Thursday February 18 2021
mkojani pic
By Kelvin Kagambo
By Olipa Assa

PICHA linaanza Mkojani kafanikiwa kumuimbisha mtoto mkali, vijana wa mjini wanaita pisi kali, aliyemjaza maneno kuwa yeye ni tajiri aliyenunua mtaa mzima na anataka kufungua sheli (kituo cha mafuta) na miradi kibao ya kibosibosi. Mtoto akaingia kumi na nane, akamwambia Mkojani nisubiri nakuja.

Basi ile mtoto kutoka tu mara akapita kimwana mwingine aliyenona, amejazia, shepu kama lote, Mkojani udenda ukamtoka, akashindwa kujizuia akaona isiwe tabu akavuruga mipango ya yule wa kwanza.

Maneno yakaanza kumtoka maana mrembo huyu wa pili aliyekatisha alikuwa mashallah. “Mbona huu mtihani wa kinabii, mimi Mbongo fleva nitauweza kweli, cheki mtoto alivyonona, cheki mbuga ilivyojaa wanyama, yaani fuso limefungwa turubai lakini mzigo wote uko nje, haki ya mama mimi napenda mademu jamani.”

Basi, Mkojani akaanza kumfuata huyo mwanamke mpaka alipoingia kwenye nyumba moja hivi, lakini kabla naye hajaingia yule mrembo wa kwanza akarudi na kumzuia. Mkojani akamkataa, akajifanya hamjui, hajawahi kumsikia wala kumuona, akili yake ilikuwa kwa yule wa pili; Huyo ndiye Mkojani kwenye moja ya sinema zake za kuchekesha iitwayo Napenda Mademu.

Jamaa ni mpole, ana sura ya aibu, lakini maneno yanayotoka kwenye kinywa chake yanakinzana vikali na muonekano wake. Akianza kuongea unaweza ukadhani ana kitabu kilichojaa maneno ya vichekesho.

Lakini pia ni mkarimu na muumini mzuri wa dini ya Kiislamu na muoga wa kufanya vitu vya hovyo, akihofia kiama.

Advertisement


CHIMBUKO LA MKOJANI

Kama ilivyo ada ya Mwanaspoti kuchimbua historia za maisha ya mastaa ambazo hazijawahi kusikika, leo limeibua mambo mazito ya kusikitisha na kuchekesha ya msanii wa vichekesho nchini, Abdallah Mohamed Nzunda ‘Mkojani’.

Katika mahojiano yake na Mwanaspoti alipotembelewa kijiweni kwake Tabata Segerea, Mkojani anafichua alipoanzia hadi akajulikana na Watanzania wanaopenda kutazama kazi zake na kuzifurahia.

Anasema alifanya komedi za kuigiza barabarani, huku akiwa ameweka kitambi bandia na kujipaka masizi usoni, jambo lililomletea balaa maishani na baadhi ya watu kumkataa, ikiwemo familia yake.

“Nilianza kuigiza komedi za barabarani mwaka 2005, nilijulikana sana huko japokuwa nilianza kwa kujifichaficha ili nisiwe najulikana nafanya kazi gani,” anasema.

Anaeleza kilichomuingiza huko ni rafiki yake mtaani aliyekuwa anaondoka saa 10:00 jioni na kurudi saa 4:00 usiku wakati mwingine saa 5:00 usiku akiwa ana pesa nyingi.

Anasema alipomuuliza dili zinazomfanya awe na kipato kuliko vijana wengi mtaani kwao Manzese, jamaa aliishia kutabasamu na kutojibu swali.

“Kwa sababu nilikuwa namuuliza mara kwa mara, siku moja akaniweka wazi kuwa anafanya komedi za barabarani, nikacheka sana kisha nikamwambia twende wote, akaniuliza unaweza nikamjibu ndio, tukaondoka hapo ndipo ukawa mwanzo wangu,” anasema.

“Siku ya kwanza nilipata Sh50,000 nikaenda kununua mabuti ya Timberland yale tulikuwa tunaita Buyu. Lakini nilijitahidi kuficha pesa ili mzee asinione. Nilipozoea kupata pesa dili likabumburuka.”


BABA ACHEFUKWA

Anasema taarifa mfikia mpaka baba yake mzazi kuwa anaigiza barabarani, alichefukwa sana na kumchukia kipindi hicho kwani alikuwa anapata kila kitu nyumbani.

“Baba yangu hakutaka mambo ya kuigiza hasa kupaka paka masizi na kuweka minguo tumboni, siku ambayo aliambiwa aliniuliza hivi wewe unakosa nini hapa ndani, kinachokufanya uende huko barabarani ukakatikekatike viuno, kwanini unanivua nguo?” Mkojani anamnukuu baba’ke.

“Baba yangu ni muumini wa dini ya Kiislamu, kuna wakati mwingine nilikuwa naalikwa kwenye matamasha, sasa kuna wakati mwingine unachekesha kwa kukata viuno hilo lilikuwa linamchefua, alikuwa ananiambia nisilete mambo ya laana na aibu kwa familia ya Kiislamu.”

Baada ya kuona hali ya hewa nyumbani haipo sawa kati yake na baba aliondoka na kwenda kuishi kwa washikaji zake.

“Baadaye baada ya baba yangu kuona ninachokifanya ni kitu ninachopenda, kinanipa amani na kinaniendeshea maisha akanisamehe na kuelewa kazi yangu, nakumbuka alinifanyia tambiko ili kuondoa maneno ya laana ambayo alinitamkia.”


ALIPIGWA CHINI

Achana na baba yake kuchukizwa na kazi hiyo, balaa lingine lililomkuta Mkojani kutokana na kazi ya kuchekesha na masizi mtaani ilikuwa ni kutemwa na mpenziwe aliyempenda.

Ipo hivi. Mkojani alikuwa anatongoza wanawake bila kuwaambia ukweli wa kazi yake. Aliwaingia kwa gia ya ana mishe mjini ambazo zinamuingizia kipato. Sasa kuna siku alifumwa na demu wake 2006 maeneo ya karibu na Ikulu, Posta jijini Dar es Salaam.

“Mimi na rafiki yangu niliyekuwa nafanya naye kazi tulikuwa na aina ya kuwasiliana tunapoona watu wanaotujua wametugundua hasa mwenye nyumbani na hao mademu, siku ambayo sitakuja kuisahau ni ile ambayo nilifumwa na demu wangu nikifanya komedi Posta,” anasema.

“Rafiki yangu ndiye aliyemuona, akaniambia oyaa mambo yameharibika, nikashituka nikaanza kuangaza angaza macho, si nikamuona bana, kila nikitoa macho huku na kuangalia kule alikuwa ananitazama ili kujua ananifananisha ama ni mimi mw-enyewe, akajua ni mimi akaondoka zake, mimi nikaendelea na kazi zangu.”

Anasema baada ya kumaliza majukumu ambayo wakati mwingine alikuwa anaondoka na Sh50,000 hadi 100,000 kwa siku, alirejea nyumbani na alipomtafuta mpenzi wake kwa simu aliambiwa kuwa ameachwa.

Anasema baada ya hapo alipata funzo, ikawa kama anampenda mwanamke basi humtongoza akiwa kwenye manguo yake ya kazi yaani tumbo na usoni masizi au kama si hivyo huweka wazi kazi anayofanya ili kama anakubaliwa isije ikaleta usumbufu baadae. Ukiachana na changamoto ya mahusiano, cha kuvunja mbavu zaidi ni kwamba Mkojani alikuwa anaficha kazi yake mpaka kwa baba mwenye nyumba, lakini siku alipogundulika ilikuwa noma. Ilikuwaje? ITAENDELEA


Advertisement