Rekodi za Zuchu miezi 10 WCB zinavyosisimua

Hakuna ubishi mwimbaji wa mwisho kusainiwa na WCB Wasafi, Zuchu amepata mafanikio makubwa ya kimuziki kwa kipindi kifupi ukilinganisha na wasanii wengine wa lebo hiyo.

Ikumbukwe WCB ilianza kusaini wasanii mwaka 2012 na msanii wa kwanza alikuwa ni Harmonize ambaye kwa sasa amejitoa kwenye lebo hiyo na kuanzisha ya kwake, Konde Music Worldwide.

Zuchu alitangazwa kuwa chini ya WCB Aprili 8, 2020 na kufanya lebo hiyo kuwa na jumla ya wasanii wawili wa kike baada ya Queen Darleen. WCB ilikuwa hajamsaini msanii mpya toka Januari 28, 2018 na walimsaini Mbosso aliyetamba vilivyo akiwa na Yamoto Band.

Mmiliki wa lebo hiyo, Diamond Platnumz alieleza, Zuchu alisubiri kwa kipindi cha miaka minne ndipo wakaamua kumtoa kwa sababu walitaka aelewe kwanza maisha ya kisanaa yalivyo.

“Alikuwa kwanza band vocalist wangu yeye na Lava Lava, akatoka Lava Lava nikawa naangalia. Kwa hiyo amekaa na kumjenga hadi sasa amekuwa mwanamuziki, WCB hadi utoke lazima uwe mkali,” alisema Diamond.

Diamond alitoa kauli hiyo usiku wa Aprili 12, 2020 ma ulifanyika utambulisho wa Extended Playlist (EP) ya Zuchu inayokwenda kwa jina la I Am Zuchu ambayo ina nyimbo tano. Wimbo wa kwanza kuachia ni Wana ambao ulitoka kabla ya EP hiyo, video yake iliweza kutazamwa (views) zaidi mara Milioni 1 kwenye mtandao wa YouTube ndani ya siku mbili.

Ikumbukwe ilimchukua wiki moja pekee kuweza kufikisha wafuatiliaji (subscribers) 100,000 kwenye mtandao wa YouTube. Kwa mujibu wa Diamond, Zuchu ndiye msanii wa kwanza wa kike Afrika kuweza kufikia mafanikio hayo.

Alipotoa EP yake, I Am Zuchu ndani ya siku 26 pekee katika mtandao wa Audiomack ilisikilizwa (streams) zaidi ya mara 1,000,000 kwa kipindi hicho. Kufikia Agusti 5, 2020, Zuchu aliweka rekodi ya kuwa msanii wa kwanza Tanzania kufikisha wasikilizaji Milioni 3 kupitia EP hiyo ndani ya mtandao wa Boomplay.

Kutokana na mafaniko hayo, Zuchu ilimchukua miezi mitano tu hadi kufanikiwa kufikisha wafuasi (followers) Milioni 1 kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram ambapo hadi sasa anafuatiliwa na watu zaidi ya Milioni 2.

Ukuaji wake wa haraka katika muziki na umaarufu katika mitandao ya kijamii, Julai 29, 2020 Meneja wa WCB, Sallam SK alitangaza kuwa thamani ya Zuchu ni Sh20 milioni kwa atakayemuhitaji kwenye show yake.

Kauli hiyo ilikuja ikiwa ni wiki moja baada ya msanii huyo kuandaa show ya shukurani ‘I Am Zuchu’ iliyofanyika ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam na kupata mapokezi makubwa hadi Diamond kumzawadia gari jipya aina ya Toyota Vanguard.

Show hiyo iliyofanyika Julai 18, 2020 viingilio vilikuwa si bei chee, kiingilio cha chini kabisa ilikuwa Sh50,000, VIP walilipa Sh100,000, pia kulikua na meza ambazo bei yake ni kuanzia Sh1 milioni hadi 5. Uzuri ni tiketi zote ziliisha (sold out) takribani saa saba kabla ya show kuanza.

Kufikia November 6, 2020 Zuchu aliweka rekodi ya kuwa msanii wa kike Afrika Mashariki mwenye wafuatiliaji wengi (subsribers) kwenye mtandao wa YouTube.

Hiyo ni baada ya kufanikiwa kuwa na wafuatiliaji 547,000 akiwa amempiku Nandy aliyekuwa akiongoza kwa wafuatiliaji 546,000 kwa wakati huo. Hadi sasa Zuchu amefikisha wafuatiliaji zaidi ya 746,000 huku Nandy akiwa na 651,000.

Mwanzoni mwa Desemba 2020 waandaji wa tuzo za Grammy waliripoti Zuchu kufanikiwa kuingia kwenye hatua ya kujadiliwa (Consideration) kwa ajili ya kuwania tuzo hizo kama Mwanamuziki Bora Chipukizi.

Ingawa hakufanikiwa upande wa Grammy, takribani siku 24 nyumba Zuchu alishinda tuzo kutoka African Muzik Magazine Awards (AFRIMMA) kutokea Marekani kama Msanii Bora anayechipukia.

Januari mwaka huu BBC Swahili walimtaja Zuchu kama msanii wa kwanza miongoni mwa wasanii 10 kutokea Afrika ambao wanapaswa kutazama zaidi kwa mwaka 2021. Wengine ni Fik Fameica (Uganda), KiDi (Ghana), Omah Lay (Nigeria), Sha Sha (Zimbabwe), Soraia Ramos (Cape Verde), Tems (Nigeria) na Elaine (South Africa).

Kweli Zuchu akaufungua mwaka vizuri kwa kuachia wimbo Sukari uliotoka Januari 19, 2021, video ya wimbo huu imeweza kutazamwa (views) zaidi mara Milioni 1 ndani ya 22 katika mtandao wa YouTube na kuwa msanii wa kwanza wa kike Tanzania kuweka rekodi hiyo.

Ikumbukwe mtoto huyu wa Malkia wa Taarabu nchini, Khadija Kopa anaweka rekodi hizo zote ikiwa ni takribani miezi 10 tangu atangazwe kuwa chini ya WCB Wasafi.


Imeandikwa na Peter Akaro