Nandy kanufaika na vingi vya Jay Melody!

Muktasari:
- Jay Melody akiwa miongoni mwa wasanii wa Bongofleva wanaosikilizwa zaidi mtandaoni tayari ameshinda tuzo, ametoa albamu pamoja na kuandika na kutengeneza nyimbo zake kubwa na za wasanii wengine. Fahamu zaidi.
ALIYEKUWA msimamizi wake kimuziki pale Tanzania House of Talent (THT), Ruge Mutahaba ndiye alimpa jina la Jay Melody likisadifu umahiri wake katika uimbaji, kazi iliyompatia umaarufu, mashabiki na fedha.
Jay Melody akiwa miongoni mwa wasanii wa Bongofleva wanaosikilizwa zaidi mtandaoni tayari ameshinda tuzo, ametoa albamu pamoja na kuandika na kutengeneza nyimbo zake kubwa na za wasanii wengine. Fahamu zaidi.
1. Tangu ameanza muziki Jay Melody ameshinda tuzo moja ya muziki Tanzania (TMA) katika kipengele cha Wimbo Bora wa Mwaka 2023 (Nakupenda), huku akitoa albamu moja 'Therapy' (2024) yenye nyimbo 12.
2. Jay Melody alitumia dakika 10 tu kurekodi wimbo 'Manu' (2023) alioshirikishwa na Phina ambaye ni mshindi wa Bongo Star Search (BSS) 2018 na mshindi tuzo nne za TMA kwa misimu miwili iliyopita.
3. Hadi sasa wimbo wa Jay Melody, Nakupenda (2022) ndiyo pekee wa Bongofleva ambao lyric video yake imesikilizwa zaidi YouTube kwa muda wote ikiwa na 'views' zaidi ya milioni 33.
4. Jay Melody ni msanii wa 13 Tanzania kufikisha wafuasi (subscribers) zaidi ya milioni moja YouTube akiwa ni mmoja wa wasanii wachache waliofika namba hizo ndani ya muda mfupi akiwa amejiunga na mtandao huo Desemba 9, 2017.
5. Diamond Platnumz ndiye msanii wa kwanza kupata wafuasi milioni moja YouTube kisha akafuata Harmonize, Rayvanny, Mbosso, Zuchu, Alikiba, Lava Lava, Nandy, Marioo, Aslay, Rose Muhando, Jux na Jay Melody. Utakumbuka Diamond ndiye mwanamuziki anayeongoza kwa kuwa na wafuasi wengi YouTube Afrika akiwa nao milioni 9.2, huku akiwa wa pili kwa kutazamwa ambapo ametanguliwa na Burna Boy wa Nigeria.
6. Mnamo Septemba 2023, Jay Melody aliandika rekodi kama msanii wa kwanza Afrika Mashariki kufikisha 'streams' milioni 200 katika jukwaa la Boomplay Music bila kutoa albamu wala EP. Wasanii wote wa Bongofleva wenye 'streams' zaidi ya milioni 200 Boomplay ambao ni Diamond, Rayvanny, Harmonize, Mbosso na Zuchu walishawahi kutoa albamu au EP, ila Jay Melody alifika huko bila vitu hivyo viwili.
7. Billnass alishinda tuzo yake ya kwanza ya TMA baada ya kutoa wimbo wake, Puuh (2022) akimshirikisha Jay Melody ambao ulimwezesha kushinda kipengele cha Msanii Bora wa Kiume wa Hip Hop 2022.
8. Hadi sasa wimbo huo ambao amemshirikisha Jay Melody ndiyo pekee wa Billnass uliosikilizwa zaidi Boomplay ukiwa na 'streams' milioni 53.7. Pia ndiyo wimbo wake uliotazamwa zaidi YouTube kwa muda wote ukiwa na 'views' milioni 14.
9. Wimbo wa Jay Melody, Nakupenda (2022) ndiyo pekee wa Bongofleva uliosikilizwa zaidi Boomplay kwa muda wote ukiwa na 'streams' zaidi ya milioni 83 huku msanii huyo akiwa na jumla ya 'streams' milioni 300 katika jukwaa hilo.
10. Hadi sasa Jay Melody ndiye msanii aliyemwandikia Nandy nyimbo nyingi na zote zikafanya vizuri. Jay kamwandikia nyimbo nne ambazo ni Kivuruge (2017), Njiwa (2018) ft. Willy Paul, Hallelujah (2019) ft. Willy Paul na Do Me (2020) ft. Billnass. Ikumbukwe wasanii wengine waliomwandikia Nandy ni pamoja na mumewe Billnass - Bugana (2019), New Couple (2021) na Dah! (2024). Pia kuna Marioo - Wasikundanganye (2017), Kusah - Nibakishie (2020) ft. Alikiba na Lody Music - Napona (2022) ft. Oxlade.
WIKI IJAYO > Msanii anayefuata ni Kajala Masanja