Mauaji ya Tupac #2: Kwanini imechukua miaka 27 mtuhumiwa kukamatwa

JANA tulianza kusimulia kukamatwa kwa Duane “Keffe D” Davis anayetuhumiwa kwa mauaji ya Tupac Shakur mwaka 1996 na leo tunamalizia sehemu ya pili ya kisanga hicho kwa kutazama ni kwa namna gani anahusika, kwanini pekee ndiye amekamatwa? Na kwanini imechukua muda mrefu? Miaka 27?! Endelea...!
SEPTEMBA 12, 1997 mama mzazi wa Tupac, Afeni Shakur alifungua kesi akidai kuwa, Orlando ‘Baby Lane’ Anderson ambaye ni mpwa wa Davis alihusika na kifo cha mtoto wake, lakini Anderson alikana kuhusika na tukio hilo.
Ila kwa mujibu wa Los Angeles Times, siku chache kabla, Anderson alifungua kesi akidai alishambuliwa na Tupac na wanachama kadhaa wa Death Row Records kwenye ukumbi wa Hoteli ya MGM Grand saa chache kabla ya kifo cha rapa huyo.
Hata hivyo, miaka miwili kabla ya kifo chake, Tupac alijeruhiwa kwa kupigwa risasi wakati wa tukio la wizi katika hoteli ya katikati ya jiji la Manhattan Novemba 1994, huku akipoteza Dola 40,000, takribani Sh100 milioni kwa sasa.
Aliwashtumu waziwazi marapa wenzake, Christopher Wallace ‘The Notorious B.I.G’ na Sean Combs ‘Diddy’ kuwa walihusika na tukio hilo, ingawa wote wawili walikanusha vikali, jambo hilo lilileta mzozo na mgawanyiko mkubwa katika jamii ya Hip Hop.
Ikumbukwe miezi sita baada ya kifo cha Tupac, hasimu wake kimuziki, B.I.G naye aliuawa kwa kupigwa risasi Machi 9, 1997, wote walikuwa katika vita vilivyokuwa vinaendelea katika ulimwengu wa Hip Hop kati ya East Coast na West Coast.
Tupac mzaliwa wa New York aliwakilisha East Coast baada ya kusaini Death Row Records yenye makao yake Los Angeles, mara nyingi alirushiana maneno na wenyeji wa New York, B.I.G na Diddy kutoka West Coast akiwakilisha Bad Boy Records yenye makao New York.
Vita vya maneno katika nyimbo zao vilichukua nafasi na kufikia hatua mbaya, Tupac alitoa wimbo wake, ‘Hit ‘Em Up’ ambao ulimlenga B.I.G ambaye alijibu mapigo kwa kuachia ngoma, ‘Who Shot Ya?’ uliokuwa na maneno mengi ya dhihaka, ingawa alikanusha kumlenga Tupac.
Akizungumza na wanahabari wiki iliyopita, Luten Johansson kutoka Idara ya Uchunguzi ya Polisi, huko Las Vegas alisema polisi kwa muda mrefu walikuwa wanajua muhtasari wa matukio hayo, lakini walikosa ushahidi wa kutosha kufungua kesi kuhusu mauaji ya Tupac.
Watu wengine waliohusishwa na uhalifu huo wameshafariki, akiwemo Anderson ambaye alikanusha kuhusika kwake akiongea na CNN kabla ya kifo chake katika shambulizi lilohusiana na magenge ya uhalifu mwaka 1998.
Julai 18 mwaka huu, polisi walipopekua nyumba ya mke wa Davis huko Henderson walichukua nakala ya kumbukumbu ya kitabu kilichoandikwa na Davis mwenyewe, Compton Street Legend (2019) ambacho kinaelezea maisha ya magenge ya mitaani na mauaji ya Tupac.
Davis katika kitabu hicho anajieleza kuwa mmoja wa mashahidi wawili tu, walio hai wa tukio la kupigwa risasi Tupac, mwingine wa pili aliye hai ni Knight ambaye kwa sasa anatumikia kifungo jela kwa kuua bila kukusudia katika kesi isiyohusiana na hiyo.
Kwa mujibu wa dibaji ya kitabu hicho kinachopatikana katika mtandao wa Amazon, Davis alikuwa mpiga risasi wa zamani wa genge la Southside Compton Crips na Mkuu wa Operesheni ya Dawa za Kulevya zenye thamani ya mamilioni ya dola.
Katika kitabu hicho, Davis akiita tukio hilo ‘makabiliano makali’, ndiyo yalisababisha vifo vya mastaa wawili wakubwa wa Hip-Hop duniani, Tupac Shakur na Christopher Wallace ‘The Notorious B.I.G.’ na kubadilisha historia ya Hip Hop milele.
Kulingana na Shirika Huru la Habari (AP), vitu vilivyopatikana katika nyumba hiyo ni simu ya mkononi, kompyuta ndogo, gari, picha, jarida la Vibe lililoangazia maisha ya Tupac, risasi 40 na nakala ya kitabu hicho cha ‘Compton Street Legend’ ambacho ndicho kimechochea pia kukamatwa kwake.
Hata hivyo, hapo awali polisi kutoka kitengo cha upelelezi, Greg Kading ambaye alikuwa anachunguza kesi hiyo, alisema Davis alikuwa amekiri uhalifu huo mbele ya polisi mwaka 2009 lakini taarifa hizo hazikuweza kutumika.
“Tulimkalisha chini mnamo 2009, na alikiri uhusika wake katika mauaji pamoja na washiriki wengine, lakini Davis alikuwa na makubaliano (proffer) nasi, kwa hivyo hatukuweza kutumia habari ambayo aliitoa dhidi yake,” Kading aliiambia CNN.
Ikumbukwe ‘Proffer’ ni makubaliano ambayo mshukiwa anakubali kutoa taarifa inayoweza kuwa muhimu katika uchunguzi, hata hivyo, taarifa zinazotolewa kwa ujumla haziwezi kutumika kama ushahidi dhidi ya mshukiwa.
Kaka wa kambo wa Tupac, Mopreme Shakur ambaye pia ni mwanamuziki wa Hip Hop, alisema habari za kukamatwa kwa Davis zina ‘utamu na uchungu ndani yake na kuhoji kwanini iwe sasa.
“Tumepitia miongo kadhaa ya maumivu, wanajua kuhusu mtu huyu ambaye amekuwa akizungumza hilo kwa kinywa chake kwa miaka mingi, kwa nini sasa? Kwetu hili halijaisha, tunataka kujua ni kwa nini, na kama kulikuwa na washiriki wengine wowote,” alisema Mopreme.
Jumatano ya wiki hii, Oktoba 4 Davis alifikishwa mbele ya mahakama kwa mara ya kwanza na kesi hiyo inatarajiwa kutajwa tena Oktoba 19 mwaka huu, huku akiendelea kusota rumande. Mamlaka zinasema Davis anashtakiwa kwa maneno ya kinywa chake mwenyewe na ndiye mtuhumiwa pekee ambaye yupo hai hadi sasa.