Mastaa walioanza kibabe mwaka na hitsongs

LEO ni Februari 13, 2024 lakini tayari mambo yamekuwa mengi unaweza kusema ni Septemba kutokana na namna mwaka huu ulivyoanza kwa kuchangamka kwenye kila eneo kuanzia maisha ya kila siku, siasa, michezo na burudani.
Ni kawaida ya Januari na Februari kuwa hivi. Wapo wanaelewa kutokana na mambo yao mengi kunyooka lakini wengine wanaona ni miezi dume kwani mambo hayaendi na yakienda ni ile kibishi bishi.
Sahau kuhusu nadharia hizo za Januari na Februari kwa mtu mmoja mmoja. Rejea kwenye tasnia ya muziki.
Mwaka huu ni kama wasanii wamepania hivi! Hadi sasa walio wengi wameachia ngoma mpya na hawataki kulaza damu kabisa kwani siku zinazidi kusonga.
Mwanaspoti kupitia makala haya linakuletea baadhi ya wasanii waliofungua mwaka huu kwa kutoa nyimbo ambazo moja kwa moja zimewafikia watu wengi na kupendwa zikiombwa sana redioni, kwenye runinga na mitandaoni huku mtaani zikipigwa kila kona ‘Hitsongs’. Tiririka;
MBOSSO- UMECHELEWA
BAADA ya kumaliza mwaka 2023 kwa ukubwa wa aina yake akifunga na ngoma zilizopendwa zaidi kama Sele na amepotea, mkali huyu kutoka lebo ya Wasafi Classic Baby (WCB) mwaka huu ameendelea alipoishia baada ya kutoka ngoma iitwayo ‘Umechelewa’.
Mbosso ambaye jina linalosomeka kwenye cheti chake cha kuzaliwa ni Mbwana Yusuph Kilungi katika ngoma yake hiyo ya ‘Umechelewa’ ameimba mahadhi ya mahaba na wimbo huo umesambaa sana na kusikilizwa mara nyingi kwenye mitandao ya kusambazia miziki huku Youtube ikitazamwa na watu zaidi ya milioni moja.

MARIOO-AWAY
Mwaka jana ulikuwa wa baraka sana kwa Marioo na alikiri aliingiza mkwanja mrefu zaidi tangu ameanza muziki miaka kadhaa nyuma.
Hiyo ni kutokana na kutoa ngoma nyingi ambazo zilipendwa, pia kufanya kolabo kibao ambazo zilifungua milango kwa wasanii wapya ikiwemo Chinno Kid anayefanya vyema kwa sasa.
Bia tamu, Shisha, Love Song, Tomorrow, Lonely na anisamehe ni miongoni mwa mikwaju ya Marioo iliyofanya vyema mwaka jana.
Mwaka huu ameanzia alipoishia baada ya kumshirikisha kwa mara ya pili mkali, Harmonize kwenye ngoma inayoitwa ‘Away’ na hadi sasa ukitaja ngoma tano zinazofanya vizuri utapigwa usipoitaja.
Naogopa ni jina la ngoma ya kwanza kwa Marioo kumpa shavu Harmonize. Marioo jina lake kamili ni Omary Mwanga.

NANDY-DAH!
Faustina Charles Mfinanga ‘Nandy’ ni miongoni mwa kinadada waliofanya poa kwenye muziki mwaka jana akiachia nyimbo nyingi zilifuatiliwa sana na kukonga mioyo ya mashabiki ikiwemo Falling, Follow na Kwamanati.
Mwaka huu kaufungua na ngoma kali aliyoipa jina la Dah!. Ngoma hiyo aliitunga ikiwa mahsusi kwa wapendanao Haji Manara na Zaylissa lakini ghafla imebadilika na kuwa ya wapenda burudani wote.
Siku chache baadae akaitoa ngoma hiyo kamili akiwa amemshirikisha Mfalme wa Bongo Fleva, Alikiba. Kwa sasa ni miongoni mwa ngoma tatu za juu kwenye chati za muziki Bongo.

ROMA-NASIKIA HARUFU
Mkali huyu wa Hiphop yupo zake Marekani lakini akitoa ngoma zinatrend Bongo kama vile yupo zake Buza kwa Mama Kibonge au Mbezi kwa Msuguri.
Baada ya kuufunga mwaka jana na ngoma ya ‘Nipeni Maua Yangu’, mwaka huu aliuanza kwa kushika namba moja karibu kwenye kila mtandao wa kuuzia nyimbo na ngoma yake iitwayo ‘Nasikia Harufu’ aliyomshirikisha Lejendi wa muziki, Chid Benz.
Ngoma hiyo imepenya kila kona na watu wameipokea kwa ukubwa zaidi huku wengi wakifurahia unyama mwingi alioufanya Chid humo baada ya kimya cha muda mrefu na sasa kwenye Youtube imetazamwa na zaidi ya watu 1 milioni. Jina la kamili la Roma ni Ibrahim Mussa.
DULLA MAKABILA-FURAHI
Mkali huyu wa nyimbo za singeli naye hajalaza damu kwani Januari alitoa ngoma iitwayo ‘Furahi’ na inafanya vyema kwenye mitandao ya kuuzia muziki ikiwa kwenye chati za juu karibu kwenye kila mtandao alipoipakia huku mtani ikiwa miongoni mwa mada kuu.
Makabila ambaye hufahamika kwa jina lake halisi la, Abdallah Ahmed mwaka jana alitamba na ngoma kibao ila zilizoushika mtaa zaidi ni Pita Huku, Tabata, Kumbe kweli na Nije ama nisije.
Ngoma hiyo ya Furahi hadi sasa Youtube imetazamwa na watu zaidi ya laki nane na huku mtaani kwa sasa inapigwa karibu kila kona.

DIAMOND-MAPOZ
Supasataa wa muziki nchini, Naseeb Abdul ‘Diamond’ naye hajapoa kwani ameanza mwaka kwa kishindo akiachia ngoma iitwayo ‘Mapoz’, aliyowashirikisha wakali, Mr Blue na Jay Melody.
Ngoma hiyo imekuwa pendwa sana ikiwa na mahadhi ya mapenzi ambapo vesi ya kwanza ameimba Jay Melody, ya pili akaimba Mondi na ya tatu akamaliza Mr Blue huku kiitikio wakiimba pamoja.
Ngoma hiyo ambayo pia video yake imetoka ipo kwenye nafasi mbili za juu katika chati za kusikiliza na kutazama muziki Bongo.

HARMONIZE-I MADE IT
Konde Boy naye tayari ameuanza mwaka kwa kuachia mkwaju mmoja wa kimataifa unaoitwa ‘I Made It’. Humo ndani amemshirikisha mkali kutoka Kenya, Bien anayeunda kundi la Saut Soul na rapa Bobby Shmurda kutoka Marekani. Ngoma hiyo imeenda sana hususan Marekani na Kenya kutokana na nguvu waliyonayo Shmurda na Bien nchini humo na hadi sasa wimbo huo kwenye mtandao wa Youtube licha ya kuwa video ya maneno (Lyrics video) ila imetazamwa na watu zaidi ya milioni moja.

DAYOO-HUU MWAKA
Miongoni mwa ngoma zinazosikilizwa zaidi nchini mwaka huu ni pamoja na ‘Huu Mwaka’ kutoka kwa Dayoo akiwa amempa shavu Rayvanny.
Ngoma hii inayoshawishi upambanaji zaidi kwa mwaka huu, imekuwa ikipendwa na wengi kutokana na mahadhi yake kugusa maisha ya watu wengi na mipango yao.
Hadi sasa ngoma hii Youtube imetazamwa na watu zaidi ya milioni mbili na bado ipo kwenye namba za juu katika chati za mitandao mbalimbali ya kuuzia muziki.

KUSAH-MUNGU TU
Mkali huyu wa Bongo Fleva ameanza mwaka huu kwa kuachia ngoma inayoitwa ‘Mungu Tu’ ambayo kwa kasi imepenya kwenye spika nyingi kitaa huku mahadhi yake ikiwa ni kujipa/kuwapa moyo wapambanaji wote.
Jina kamili la Kusah ni Salmin Issa na amekuwa bora kwenye kutunga nyimbo zinazoenda mbali hususani zenye mahadhi ya mapenzi lakini mwaka huu ameona aanze na hiyo ya Mungu tu na kwa namna flana imepenya.
Kabla ya hiyo ngoma Kusah ambaye pia amekuwa akiandikia wasanii wengi, aliwahi kutamba na nyimbo kama I wish, This Love, Mama Lao, I dont Care, Utaniua, On Fire na nyingine kibao.