Safari ya Joslin na Wakali Kwanza hadi kutusua

Muktasari:
- Nuruel ndiye msanii wa Bongofleva aliyemvutia zaidi Joslin ndipo naye akaingia katika muziki na kuzichanga karata zake, na baada ya miaka kadhaa akawa mmoja wa wasanii wakali wenye mtindo wa tofauti sana. Fahamu zaidi.
MSANII wa Bongofleva Joslin ni miongoni mwa wasanii watatu waliounda kundi la Wakali Kwanza akiwa na wenzake Q Jay na Makamua huku MJ Records wakitoa kazi zao nyingi hapo ambazo ziliwapatia umaarufu mkubwa wakati huo.
Nuruel ndiye msanii wa Bongofleva aliyemvutia zaidi Joslin ndipo naye akaingia katika muziki na kuzichanga karata zake, na baada ya miaka kadhaa akawa mmoja wa wasanii wakali wenye mtindo wa tofauti sana. Fahamu zaidi.
1. Alianza muziki akiwa shule ya msingi Mtendeni, Dar es Salaam, baba yake alimpeleka sehemu atakapojifunza muziki kama kupiga piano kila anaporudi shule jioni ili asipate muda wa kujiunga katika makundi mabaya mtaani.
2. Kabla ya kutoka kimuziki, Joslin alikuwa anakutana na Mr Blue na moja ya mambo aliyomwambia ni kwamba akija kutoka watu lazima watamkubali sana - alipokuja kutoka ndipo mashabiki wakaanza tena kumpambanisha na Mr Blue.
Na wimbo wa Dully Sykes 'Dhahabu' ndio wa kwanza kwa Joslin na Mr Blue kufanya pamoja. Dully Sykes aliwashirikisha maana wote wameishi Kariakoo hivyo unaendana na ujumbe wa wimbo huo uliotengenezwa MJ Records.
3. Jina lake kamili ni Joslin Robert Mchala, ndilo alipewa na wazazi wake, hivyo hakubadili jina alipoingia katika muziki ikiwa ni sawa na Barnaba, Vanessa Mdee na Linah ambao nao hawakubadili majina yao kisa muziki.
4. Mara ya kwanza Joslin kuiingia studio ilikuwa ni kurekodi wimbo 'Ningejua' alioshirikishwa na kundi la Joint Mobb, ila versi aliyoingiza katika wimbo huo hadi leo haipendi kutokana na kwamba hakufanya vizuri kama alivyotaka.
Na mara ya pili kuingia studio ndipo akarekodi wimbo wake wa kwanza kama solo 'Vita vya Kiroho' na hayati DJ Steve B aliposikia wimbo huo alimtafuta Joslin ili waweze kufanya kazi pamoja na ndipo mafanikio yake kimuziki yakaanza.
5. DJ Steve B a.k.a DJ Skills aliyepiga muziki Clouds FM wakati huo ndiye alimpeleka Joslin kurekodi MJ Records kwa mara ya kwanza na albamu mbili za kwanza za msanii huyo 'Perfume' na 'Umewezaje' ndiye alizisimamia.
6. Na huyu DJ Steve B kupitia albamu yake "Pamoja Ndani ya Game" iliyokuwa na nyimbo za wasanii mbalimbali ikiwemo wa Q Jay 'Sifai' uliotengenezwa MJ Records na Master J na Bizman ndio uliomtoa msanii huyo wa kundi la Wakali Kwanza.
Ni wimbo uliompatia Q Jay tuzo yake ya kwanza kutoka Tuzo za Muziki Tanzania (TMA), akishinda katika kipengele cha Wimbo Bora wa RNB 2007.
7. Wazo la kuandika wimbo wake 'Perfume' ambao ndio ulimtoa Joslin kimuziki lilikuja baada ya kutaka kuongelea mtindo wake wa maisha (life style) kwa njia ambayo watu watapenda na kusikiliza. Baada ya Perfume akaachia nyimbo nyingine mbili 'Mshikaji Mmoja' na 'Niite Basi'. Hizo ni miongoni mwa nyimbo ambazo zilichangia kuleta mabadiliko kwa watu kupenda muziki wa kuimba baada ya rap kutawala kwa muda mrefu.
8. Hata hivyo, Joslin aliandika wimbo 'Niite Basi' miaka miwili kabla ya kuurekodi na mara ya kwanza aliurekodi wimbo huo na kumshirikisha Mangwair ila akaja kuurudia tena peke yake na ndio huo uliokuja kushika vilivyo. Pia Joslin ndiye alimuelekeza Master J mdundo wa wimbo wake 'Niite Basi' usikike vipi kwa namna alivyoutunga wimbo huo, kisha Master J na Bizman wakatulia na kutengeneza kitu kizuri.
9. Katika kundi la Wakali Kwanza wimbo wao 'Natamani' uliotengenezwa na Marco Chali ndani ya MJ Records ndio uliowapatia tuzo yao ya kwanza ya TMA ukishinda kipengele cha Wimbo Bora wa RnB 2009.
10. Hapo awali kundi la Wakali Kwanza lilitumia jina la Free Stars ila baada ya kuhamia MJ Records ndipo wakashauriwa kubadili jina hilo maana limekaa Kizungu sana kitu kinachoweza kuwapa ugumu kueleweka, ndipo wakachekecha na kuja na hilo la Wakali Kwanza.