Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

MaDJ wakali Bongo

Muktasari:

  • Kazi ya uchezeshaji muziki inayofanywa na Ma-DJ ni ya heshima na umaarufu mkubwa tangu enzi za ukoloni. Hata hivyo, mpaka leo bado inaendelea kubamba na kufunika upande wa disko, redio na katika runinga huku ikichagizwa na maendeleo ya sayansi na tekonolojia.

UNAWEZA kuwa na nyimbo nzuri na vifaa vizuri vya disko, lakini kitu kimoja tu kinaweza kuharibu mambo yote. Disko likikosa mchezeshaji ‘DJ’ mzuri halitakuwa na mashabiki na kila wimbo utakaopigwa hautawafanya watu wabanduke katika viti vyao.

Kazi ya uchezeshaji muziki inayofanywa na Ma-DJ ni ya heshima na umaarufu mkubwa tangu enzi za ukoloni. Hata hivyo, mpaka leo bado inaendelea kubamba na kufunika upande wa disko, redio na katika runinga huku ikichagizwa na maendeleo ya sayansi na tekonolojia.

Kumekuwa na orodha ndefu sana ya Ma-DJ kila mahala, lakini wapo bora ambao huwezi kuzungumzia tasnia hii chini bila kuwataja. Ukifanya hivyo, wanaoielewa historia ya ladha na utamu wa disco, enzi hizo lilipokuwa disco haswa, watakuona una lako jambo.

Miaka sasa imepita na tasnia hii imezidi kutanuka na kuwavutia vijana wengi, ambao wameamua kuwekeza nguvu zao na akili zao, wakiendelea kubuni na kutia vionjo kwa kadiri miaka inavyosonga na teknolojia kukua.

DJ Bonny Luv

Huwezi kuzungumzia historia ya disco nchini Tanzania na kuacha kumtaja Boniface Kilosa, a.k.a DJ Bonny Love ambaye ni DJ wa madisko. Huyu ni miongoni mwa Ma-DJ wachache ambao kwa miaka mingi wamejizolea sifa za kipekee katika kuhakikisha  mashabiki wa muziki siyo tu kwamba hawabanduki stejini pindi akiingia mitamboni bali pia wanapata ‘raha kamili’.

Hali hiyo ndiyo imesababisha watu wengine wathubutu hata kusema kwamba ikiwa hujawahi kuhudhuria disco au shughuli nyingine yoyote yenye burudani za muziki huku DJ Bonny Luv asipokuwepo, basi huenda ukawa hujapata bado hiyo raha kamili.

 Hata hivyo habari njema ni kwamba hujachelewa kwani Bonny Luv alikuwepo, bado yupo na ataendelea kuwepo pale Mzalendo Pub Millenium Tower jijini.

DJ JD

Anafahamika kama John Dillinga maarufu kama DJ JD, ni kati ya Ma-DJ wakongwe kwani alianza kufanya kazi hiyo mwaka 1988, enzi hizo likiitwa disko la Old School. Wakati huo alikuwa akifanya kazi ya U-DJ katika madisko mbalimbali nchini. Katika miaka ya mwishoni mwa 1990, DJ JD aliingia katika U-DJ kwenye vituo vya redio na hadi sasa anaendelea kukaa katika nafasi ya juu.

DJ JD maarufu sana licha ya ukongwe alionao, kwa sasa anapatikana pale Isumba Lounge zamani iliitwa Jolly Club.

DJ MAJAY

Ni Dj maarufu sana ambaye kwa kipindi kirefu alikuwa akifanya shughuli zake katika redio na alikuwa akipiga katika kipindi cha Kwetu Flava, zaidi Magic FM. Wakati huohuo alikuwa akiendelea na shughuli zake za U-DJ wa disko.

Kazi yake ilijulikana zaidi pale New Maisha Club na jopo lao linalojulikana kama  Xtreme Deejay. Mara nyingi amekuwa wakipiga muziki huku akishirikiana na mpiga drums ndani ya New Maisha Club jijini Dar es Salaam.

Hivi sasa DJ Majay anatajwa kama ndiye mmiliki wa redio mpya ya kisasa liyofunguliwa mwaka huu jijini yenye masafa ya 93.7 fm ambayo bado haijapewa jina, mitambo yake ilifungwa na wataalamu kutoka Ujerumani.

DJ PETER MOE

Ni DJ maarufu sana hasa kwa wapenda burudani, wamekuwa wakiburudika na muziki wake mtamu hasa wanapofika katika Kiota cha Grooveback.

Sehemu hiyo ya burudani ni sehemu iliyowakuza vijana wengi sana ambao leo hii wameweza kufanya vyema katika sekta hiyo wakiwamo kina DJ PQ.

DJ PQ

Ni zao la Grooveback, lakini kwa sasa ni DJ wa redio akiiwakilisha Clouds FM. Dj PQ ambaye alianza kupata mashabiki wengi mwaka 1998 baada ya kushinda kwenye mashindano ya U-DJ na kupewa Taji la Smart Boy DJ, ameshafanikiwa kufanya kazi kadhaa ikiwamo kutoa burudani kwa washiriki wa Jumba la Big Brother.

DJ PQ aliyetoa burudani kwa washiriki hao waliochanganyika kutoka Ruby na Diamond, alijipatia umaarufu mkubwa baada ya mashabiki kumbatiza jina la Peter Quick kutokana kasi yake anapokuwa kazini.

DJ CHOKA

Alianza kama DJ wa Profesa Jay miaka mitano iliyopita, jina lake halisi ni Hugoline Martin, leo hii ni maarufu kwenye matamasha makubwa nchini. Anafahamika sana jukwaani kuliko kwenye kumbi za disko, mwanzoni alikuwa akifahamika kwenye Tamasha la Fiesta, ila kwa sasa anashiriki matamasha mengine yote makubwa yakiwamo yale ya Kili Music Tour.

Alianza kazi hii mwaka 2005, kuna kipindi fulani aliwahi kuweka wazi kwamba anaachana na kazi hiyo kutokana na kuamua kuwekeza nguvu kubwa katika kazi inayomlipa yaani ile ya website yake ya djchoka.com. Lakini baadaye alishawishiwa kuendelea na kazi hiyo kutokana na uzoefu wake jukwaani.

DJ AD

Ni DJ mkali Afrika Mashariki, huyu anapatikana Dodoma katika Klabu ya Usiku ya Maisha yaani Maisha Club Dodoma.

Abdul Mkali, DJ AD, Amekuwa jaji wa Ma-DJ kwa miaka miwili mfululizo katika mashindano ya kutafuta Ma-DJ na wasanii wa muziki wakali wa kutumia mtindo akapela maarufu kama freestyle STR8 MUZIK yanayofanyika kila mwaka.

Katika mashindano hayo, DJ AD  kutoka East Africa Radio ni jaji wa Ma-DJ akishirikiana na DJ Nelly.

DJ OMMY CRAYZ

Kati ya Ma-DJ wakali wanaotikisa Jiji la Dar es Salaam, ni Ommy Crayz. Ameajiriwa na Maisha Club, na kwa sasa ndiye DJ pekee ambaye kila siku za wiki anawarusha mashabiki wa disko katika ukumbi huo uliopo Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Ni DJ kutoka Maisha Club na amekuwa msimamizi wa kazi za mwanamuziki Climax Bibo ambaye ni rapa.

DJ Q

Huyu anapiga jukwaani, ukumbini na redioni, jina lake halisi ni Mohamed Chande, yuko kazini kwa miaka zaidi ya 20 akifanya muziki wa kila aina.

Kwa sasa ni msimamizi wa Top Garage Night Club iliyopo maeneo ya Mbezi Beach jijini Dar es Salaam lakini pia ni mwajiriwa wa Magic FM Radio ambapo hewani anasikika katika kipindi cha Daladala Beat.

Jamaa pia ni mtangazaji na aliwahi kuwa nyota katika kipindi cha Sunrise cha Times FM Radio na alikuwa akishirikiana na Masoud Kipanya kuendesha kipindi hicho akiwa kama DJ na mtangazaji.

DJ ZIRO

Jina lake kamili ni Laurence Daniel maarufu kama DJ Ziro ‘O’. Umri wake kwa sasa ni miaka 26 lakini alianza kazi ya U-DJ mwaka 1999 kama DJ wa mitaani na kwenye camp mbalimbali za uswahilini, watoto wa mjini wanajua ni yale madisko vumbi au pati za uswahilini.

Sehemu alizofanyia kazi ni pamoja na DTV, Channel 10. Maisha Club na sasa yupo Clouds FM na Clouds TV.