Lulu Diva achomoa kesi ya Wema, Whozu

Muktasari:
- Akizungumza na Mwanaspoti, Lulu amesema anachukizwa na watu ambao wameunda kikundi cha kumpa sifa mbaya ili jamii imuone mwanamke wa tofauti.
NYOTA wa muziki anayefanya vizuri katika tamthilia nchini, Lulu Diva ameruka kimanga taarifa kwamba yeye ndiye kidudu mtu kilichosababisha uhusiano wa Wema Sepetu na Whozu kuvunjika kama zilivyosambaa mtandaoni.
Akizungumza na Mwanaspoti, Lulu amesema anachukizwa na watu ambao wameunda kikundi cha kumpa sifa mbaya ili jamii imuone mwanamke wa tofauti.
“Nimeanza kufanya uchunguzi tangu hizi habari zilivyoanza kusambaa kuwa miye ndio chanzo cha Wema na Whozu kugombana, mara mimi natoka na Whozu, mara sipendi Wema awe na Whozu, nimegundua kuna baadhi ya watu wapo kuniharibia,” alisema Lulu na kuongeza;
“Wanaonizushia wanafanya hivyo, ili nionekane nina tabia chafu isiyokubalika na jamii, sasa mimi nawezaje kumuonea wivu yule mwanamke mwenzagu? Yaani watu wapo kuropoka tu, sipendi na nikimaliza uchunguzi nitawaweka wazi wahusika wote.”€
Kwa upande wa Wema alipotafutwa na Mwanaspoti, alisema kugombana kwake na Whozu hakuna mtu baki anayehusika, kwani hayo ni mambo yao wao wenyewe na humalizana wenyewe hivyo penzi lake na Whozu bado lipo kwa sana na hakuna chochote kitakacholisambaratisha.
“Mimi na Whozu tumekuwa na matatizo yetu. Nilianza kufuta picha zake kwenye Instagram yangu na kuandika ujumbe kwenye status ya Instagram kuwa siko na mtu kiuhusiano, lakini tumekaa na kuyamaliza sisi wenyewe, sasa kwa nini watu wamhusishe mtu ambaye hahusiki na ugomvi wetu?” Alisema.
Wema na Whozu; ni mastaa wa Bongo ambao wanazungumzwa zaidi kutokana na penzi lao kuzidi kung’ara kila uchao na wakati huo huo, huku wakidaiwa kuwa ‘kapo’ inayoongoza kwa kuachana na na kurudiana mara kwa mara.
Wiki iliyopita zilienea habari kuwa Wema Sepetu na Whozu wameachana huku akihusishwa Lulu Diva ambaye ni rafiki wa Wema japo hivi karibuni wamekuwa hawana ukaribu kama zamani na huenda ndio chanzo cha madai kwamba hapendezwi Wema na Whozu kuwa wapenzi.
Wema na Whozu hadi kufika sasa wameshachana na kurudiana zaidi ya mara kumi na mbili toka waanze penzi lao mwaka 2022.