Kevin Hart: Mchekeshaji milionea aliyeanza kwa kuuza viatu

Muktasari:
- Kimo chake ni futi tano tu, lakini kwa sasa ameshakuwa mtu maarufu nchini Marekani na duniani kwa jumla na Jarida la Forbes linamtaja kuwa ni msanii namba sita kwa utajiri katika kundi la waigizaji wa komedi. Huyu ni Kevin Hart. Umeshamfahamu?
BIASHARA yake ya kwanza ilikuwa kuuza viatu, lakini akiwa na elimu kubwa kichwani. Baadaye akajitazama akagundua kuwa umbo lake ni mtaji mkubwa, hivyo akajiingiza katika kikundi cha komedi na tangu hapo akawa mchekeshaji maarufu.
Kimo chake ni futi tano tu, lakini kwa sasa ameshakuwa mtu maarufu nchini Marekani na duniani kwa jumla na Jarida la Forbes linamtaja kuwa ni msanii namba sita kwa utajiri katika kundi la waigizaji wa komedi. Huyu ni Kevin Hart. Umeshamfahamu?
Akitokea katika familia iliyosambaratika, Kevin alizaliwa Julai 6, 1979 huko Philadelphia, Pennsylvania na mama mrembo Nancy na baba Henry. Kwa kuwa baba yake alikuwa ameathiriwa na matumizi ya cocaine na vifungo vya jela mara kwa mara, utotoni mwake Kevin alilelewa na mama yake tu ambaye alipambana kuwatengenezea maisha watoto wake.
Mama huyo hakuwahi kufikiria kwamba kuna siku mtoto wake atakuwa milionea mkubwa. Kevin ana ndugu yake mmoja tu wa kuzaliwa naye, Robert Hart.
Baada ya kubaini kuwa umbo lake ni mtaji na hivyo kuhamia katika komedi, sasa amekuwa mtu maarufu Marekani na kipato chake kinatajwa kuwa Dola 15 milioni.
Kwa mujibu wa Kevin, kati ya asilimia 60 hadi 70 ya mashabiki wake ni watu weusi, jambo ambalo mwenyewe analieleza ndilo linalofifisha kutangazwa sana na vyombo vya habari vya kitaifa.
Alivyopiga pesa
Kitu kilichomfanya Kevin kuwa milionea ni komedi. Kupitia filamu zake za vichekesho zimempa pesa nyingi ikiwamo ya filamu ya ‘Let Me Explain’ ambapo kwenye wiki ya kwanza ya uzinduzi iliingiza Dola 10 milioni.
Hizo ni pesa nyingi kupatikana kwa wiki ya kwanza hasa ukizingatia ilizinduliwa kwenye kumbi 876, ikilinganisha na filamu ya ‘The Lone Ranger’ iliyozinduliwa kwenye kumbi 3,904.
Kwenye wiki yake ya pili tu, filamu hiyo iliingiza Dola 27 milioni na kushika namba nne katika filamu zilizofanya vizuri kwenye wiki ya kwanza huku filamu ya ‘Raw’ ya Eddie Murphy ikishika namba moja kwa kuingiza Dola 50.5 milioni.
Kampuni ya Lionsgate baada ya kuona kasi ya Kevin iliamua kutengeneza naye filamu ya ‘Laugh At My Pain’ na ilizinduliwa kwenye kumbi 98 na kuingiza Dola 2 milioni kwa tukio hilo tu la wikiendi moja.
Kwenye ‘Let Me Explain’, pesa inayotajwa kumfikia moja kwa moja mfukoni ni Dola 4 milioni huku pesa nyingine zikienda kwenye makato mbalimbali.
Umaarufu wake umemfanya kupata dili la kuigiza na waigizaji matata kama vile Ice Cube, Robert de Niro na Sylvester Stallone huku akitamba pia na shoo yake ya televisheni ya ‘Real Husbands of Hollywood’.
Kevin amekuwa pia akishiriki kwenye klabu mbalimbali za komedi ikiwamo The Comedy Store, The Laugh Factory, Stand-Up NY, Carolines na The Boston Comedy ambazo zimekuwa pia sehemu ya kumwingizia kipato.
Kevin alipata dili la kuigiza kwenye filamu za komedi kama ‘Death At A Funeral’ , ‘Along Came Polly’, ‘Barbershop’ na ‘The 40-Year Old Virgin’. Amefanya ziara mbalimbali za kutangaza filamu zake ambapo mauzo ya tiketi yamemwingizia Dola 15 milioni.
Kwenye filamu ya ‘Think Like A Man’, alilipwa Dola 500,000, lakini baada ya filamu kufanya vizuri kampuni ya Screen Gems Pictures iliamua kumkatia Dola 10 milioni na hivyo kwa sasa kuwa kwenye mpango wa kutengeneza ‘Think Like A Man 2’ itakayozinduliwa mwakani.
Kichaa wa magari ya kifahari
Licha ya kwamba hana magari mengi ya thamani kubwa, mchekeshaji huyo amekuwa mtumwa wa kuendesha magari ya kifahari. Staa huyo anamiliki Range Rover Supercharged yenye thamani ya Dola 95,125 na mipango yake ni kuongeza magari mengi zaidi ya gharama kubwa kama hiyo. Kevin pia anapenda kuvaa nguo zenye hadhi kubwa na alionyesha mfano kwa kuvaa jaketi la chui chui lenye thamani ya Dola 1,965.
Maisha ya ndoa
Mwaka 2003 alioana na mrembo Torrei na wawili hao wamefanikiwa kuzaa watoto wawili, Hendrix na Heaven Lee. Lakini, miaka minane baadaye wawili hao waliachana kutokana na sababu mbalimbali ambazo walishindwa kuafikiana.
Kwenye mchakato huo wa talaka, Torrie aliripotiwa kutaka alipwe Dola 90,000 na Kevin kwa ajili ya matunzo ya watoto wao. Baada ya kuachana na Torrei, Kevin amenasa kwenye penzi la mrembo, Enikko Parrish, ambaye hivi karibuni walifanya sherehe ya kutimiza miaka minne ya uhusiano wao wa kimapenzi huko Fiji.