Huyu ndiye Blue Ivy Carter, kula chuma hicho!

Akiwa na umri wa miaka tisa tu, Blue Ivy Carter alishinda tuzo ya Grammy 2021 kupitia wimbo 'Brown Skin Girl' alioshirikishwa na Mama yake mzazi, Beyonce Knowles, hivyo kuandika rekodi kama mtu mdogo zaidi wa pili duniani kushinda Grammy.
Ikumbukwe Leah Peasall ambaye sasa ana umri wa miaka 30 ndiye anashikilia rekodi ya kuwa mtoto mdogo zaidi duniani kushinda Grammy ambapo mwaka 2002 alishinda akiwa na umri wa miaka minane.
Blue Ivy Carter, 11, ni mtoto wa Beyonce na Jay Z, alizaliwa Januari 7, 2012 New York, Marekani, ni mtoto maarufu zaidi duniani baada ya Prince George kutoka familia ya kifalme Uingereza na North West, mtoto wa Kim Kardashian na Kanye West.
Tangazo la ujauzito wake lilotolewa na Beyonce Agosti 28, 2011 katika tuzo za MTV VMAs wakati akitumbuiza wimbo 'Love on Top', lilivunja rekodi ya duniani (Guinness World Record) katika mtandao wa Twitter kwa kupata 'tweet' 8,860 kila sekunde!.
Muda mfupi baada ya kuzaliwa sauti yake ilisikika kwenye wimbo 'Glory' wa Baba yake, Jay Z ambao uliingia chati za Billboard na kumfanya Blue Ivy kuandika rekodi nyingine ya dunia kama mtu mdogo zaidi kuingia kwenye chati hizo.
Wimbo, Brown Skin Girl kutoka kwenye albamu ya Beyonce, The Lion King: The Gift (2019) akishirikisha wasanii wengine, Saint JHN na Wizkid, ndio umempatia mafanikio makubwa zaidi Blue Ivy.
Kupitia wimbo huo, Blue Ivy ameshinda tuzo 10, kutoka Grammy, MTV VMAs, Shorty, The Daily Califonian, Soul Train (2), NAACP Image (2), Voice Art na BET katika kipengele cha BET HER na kuandika rekodi kama mtu mdogo zaidi kuwahi kushinda BET.
Tuzo ya BET Her ni maalumu kwa nyimbo zinazotia moyo na kuwawezesha wanawake, kwa mara ya kwanza ilitolewa mwaka 2006 ikitambulika kama BET J Cool Like That, hadi sasa Beyonce na Mary J Blige ndio wasanii walioshinda mara nyingi kipengele hicho.
"Ninapomwambia Blue Ivy ninajivunia yeye, ananiambia kuwa anajivunia mimi na kwamba ninafanya kazi nzuri, ni tamu sana," Beyonce aliliambia Jarida la Vogue, Uingereza.
Sio studio tu, Blue Ivy amewahi kutumbuiza mara kadhaa, katika tuzo za Oscars 2022 akiwa na umri wa miaka 10 aliungana na Mama yake, Beyonce kutumbuiza wimbo wake 'Be Alive' uliyotumika katika filamu ya King Richard.
Januari mwaka huu Blue Ivy aliungana tena na Beyonce kutumbuiza huko Dubai katika ufunguzi wa Hoteli ya Atlantis The Royal Resort ambapo walilipwa Dola24 milioni, wastani wa Sh56.3 bilioni kwa shoo hiyo iliyochukua saa moja na nusu!.
Katika video ya wimbo wake, Spirit, Beyonce anaonekana akiwa ameketi pekee yake katikati ya jangwa, ghafla kamera zinamleta Blue Ivy akitazama kwa mbali, huku upepo ukipeperusha nywele zake, kisha anamkaribia Mama yake na kumshika mkono.
Ikumbuke katika video za Beyonce zilizoandaliwa na Disney kutoka kwenye filamu, The Lion King (2019), Blue Ivy ameonekana katika video za nyimbo mbili; Spirit na Bigger na kumfanya kuwa Staa wa video za muziki duniani.
Sauti ya Blue Ivy ndio inasikika ikifanya simulizi katika kitabu cha watoto, Hair Love kilichoandikwa na Matthew A. Cherry ambaye amehusika katika filamu ya uhuishaji inayotokana na kitabu hicho iliyoshinda tuzo ya Oscar 2021 kama filamu Fupi Bora ya Uhuishaji.
Hair Love inasimulia hadithi ya Baba Mweusi ambaye anajifunza jinsi ya kunyoa nywele za binti yake mchanga wakati mke wake akiwa hospitalini.
Blue Ivy anatabiriwa anaweza kuja kufanya masuala ya mitindo na urembo, akiwa na miaka tisa, Februari 2021 alionyesha kuwa ni Mwanamitindo mzuri baada ya kuungana na Beyonce kutangaza chapa mpya ya mavazi ya Adidas, Ivy Park.
Bibi yake Blue Ivy, Tina Knowles (Mama yake Beyonce) ambaye ni Mbunifu wa Mitindo alionyesha Instagram picha aliyopodolewa na Mjukuu wake huyo na kumsifia ni mpambaji mzuri, anajua kucheza na 'makeup' vilivyo.
Jay Z ambaye ndiye msanii wa Hip Hop tajiri zaidi duniani akiwa na utajiri wa Dola2.5 bilioni, wastani wa Sh5.8 trilioni, katika mahojiano na The Sunday Times alizungumzia kuhusu malezi na kile alichojifunza kwa Blue Ivy.
"Unajua kuhisi kupendwa ndilo jambo muhimu zaidi ambalo mtoto anahitaji, sijali ikiwa mtoto wangu hataki kuwa katika muziki au michezo, lakini ilimradi anahisi kuungwa mkono na kupendwa, lolote linaweza kutokea," alisema Jay Z.
Ikumbukwe Blue Ivy Carter ana wadogo zake wawili mapacha, Rumi na Sir Carter waliozaliwa Juni 13, 2017, hawa bado hawajaingia katika muziki kama Dada yao. Beyonce, 41, alianza uhusiano na Jay Z, 53, mwaka 2000 akiwa na umri wa miaka 19 wakati Jay Z akiwa na miaka 30 wakati huo, walifunga ndoa Aprili 2008 kujaliwa watoto mwaka 2012 na 2017.