Harmonize atimiza miaka 10 katika muziki

Muktasari:
- Harmonize, mshindi mara nne wa tuzo za AEAUSA Marekani, ndiye msanii wa kwanza kusainiwa na kutambulishwa na WCB Wasafi kisha wakafuata wengine kama Rayvanny, Rich Mavoko, Queen Darleen, Lava Lava, Mbosso, Zuchu na D Voice.
STAA wa Bongofleva kutokea Konde Music, Harmonize mwaka huu atasherehekea kutimiza miaka 10 tangu ametoka kimuziki na kibao chake, Aiyola (2015) chini ya WCB Wasafi, rekodi lebo aliyofanya nayo kazi kwa takribani miaka minne.
Harmonize, mshindi mara nne wa tuzo za AEAUSA Marekani, ndiye msanii wa kwanza kusainiwa na kutambulishwa na WCB Wasafi kisha wakafuata wengine kama Rayvanny, Rich Mavoko, Queen Darleen, Lava Lava, Mbosso, Zuchu na D Voice.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa lebo hiyo, Diamond Platnumz, video ya wimbo huo, Aiyola (2015) iligharimu Sh39 milioni, ila kwa ujumla uwekezaji uliofanyika katika video za nyimbo nne za mwanzo za msanii huyo ulifikia zaidi ya Sh115 milioni.
Na punde tu akawa msanii maarufu akishinda tuzo ya AFRIMMA Marekani 2016 kama Msanii Bora Chipukizi baada ya kufanya hivyo kupitia AEAUSA 2016, kisha kuja kutoa EP, Afro Bongo (2019) akiwa na Diamond, Burna Boy, Yemi Alade na Mr. Eazi.
Kwa ujumla alishirikiana na wasanii wengi wa kimataifa kama Marina (Rwanda), Eddy Kenzo (Uganda), Emma Nyra (Nigeria), Willy Paul (Kenya), IYO (Nigeria), OmoAkin (Nigeria), Korede Bello (Nigeria), Sarkodie (Ghana) n.k.
Lakini baada ya miaka minne ya mafanikio katika muziki na kutambulika na wengi kama chapa yenye ushawishi, mwishoni mwa 2019 Harmonize aliamua kuondoka WCB Wasafi akiwa ni msanii wa pili kufanya hivyo baada ya Rich Mavoko.
Hatua hiyo ilileta mgogoro mkubwa wa kimaslai baina yao, Harmonize alidai alilazimika kulipa Sh600 milioni kama fidia ya kuvunja mkataba wake wa miaka 10 na lebo hiyo na kupata hakimiliki ya kazi zake zote.
Oktoba 2019 Harmonize akatangaza kuanzisha rekodi lebo yake, Konde Music Worldwide ambayo ndani ya muda mfupi iliwasaini wasanii sita ambao ni Ibraah, Country Wizzy, Anjella, Cheed, Killy na Young Skales kutokea Nigeria.
Utakumbuka Ibraah ndiye msanii wa kwanza kutambulishwa na Konde Music kupitia EP yake, Steps (2020) iliyowashirikisha Joeboy, Skibii na Harmonize, na ndiye msanii pekee aliyesalia katika lebo hiyo hadi sasa.
Na mwaka uliofuatia Harmonize akatoa albamu yake ya kwanza, Afro East (2020) chini ya Konde Music ambayo ilizinduliwa na Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete kwenye Ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam.
Albamu hiyo yenye nyimbo 18 iliwashirikisha wasanii wengi wakiwamo Mr. Blue na Lady Jaydee (Tanzania), kundi la Morgan Heritage (Jamaica), Khaligraph Jones (Kenya), Phyno, Young Skales, Yemi Alade, Falz na Burna Boy (Nigeria).
Tangu wakati huo amekuwa akitoa albamu kila mwaka na sasa zinafika tano, kuna Afro East (2020), High School (2021), Made For Us (2022), Visit Bongo (2023) na Muziki wa Samia (2024) ambayo ilizinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan pale pale Mlimani City.
Albamu yake ya nne, Visit Bongo (2023) ilishinda Tuzo za Muziki Tanzania (TMA) 2023 kama Albamu Bora ya Mwaka ikizibwaga ‘5’ ya Abigail Chams, ‘Swahili Kid’ ya D Voice, ‘Most People Want This’ ya Navy Kenzo na ‘Flowers III’ ya Rayvanny.
Ushindi huo ulimfanya kufikisha tuzo sita za TMA, tangu kurejea tuzo hizo msimu wa 2021, Harmonize ni miongoni wasanii walioshinda mara nyingi zaidi, wengine ni Zuchu (7), Alikiba (6), Diamond (5), huku Nandy, Phina, Young Lunya na Marioo wakishinda mara nne.
Desemba 2022 video ya wimbo wake, Kwangwaru (2018) ikawa ya kwanza kwake kutazamwa zaidi ya mara milioni 100 YouTube ikiwa ni ya nne Bongo kufanya hivyo baada ya tatu za Diamond, Yope Remix (2019), Inama (2019) na Waah! (2020).
Utakumbuka baada ya Kwangwaru (2018) aliomshirikisha Diamond, video nyingine Bongo zilizotazamwa zaidi ya mara milioni 100 huko YouTube ni Jeje (2020 na Nana (2015) za Diamond, Sukari (2021) ya Zuchu na Enjoy (2023) ya Jux.
Novemba 2023 Harmonize akawa msanii wa tatu Afrika Mashariki kwa video zake kutazamwa YouTube mara bilioni 1 akiungana na Diamond na Rayvanny ila kwa Afrika nzima tayari alishatanguliwa na Wizkid, Davido, Rema, Ckay, Mr. Flavour, P-Square, Tekno n.k. Ikumbukwe Diamond alifanya hivyo Juni 2020 na kuwa msanii namba moja kusini mwa Jangwa la Sahara kutazamwa YouTube kabla ya kuja kushushwa hadi namba mbili hapo Agosti 2023 na Burna Boy, mshindi wa Grammy 2021 kutokea Nigeria.
Na nje ya WCB Wasafi, Harmonize ameshirikiana na wasanii wa kimataifa kama Ruger (Nigeria), Bruce Melodie (Rwanda), Nkosazana Daughter (Afrika Kusini), Bien (Kenya), KJ Spio (Ghana), Awilo Longomba (DR Congo), Bobby Shmurda (Marekani) n.k.
Kwa upande mwingine Anjella aliyewahi kumsimamia chini ya Konde Music, ndiye msanii wa kike Bongo aliyeshirikiana naye mara nyingi zaidi wakitoa nyimbo tano ambazo ni All Night (2021), Kama (2021), What Do You Miss (2021), Kioo (2022) na Toroka (2022).