HADITHI: Zindiko (sehemu ya 9)

Muktasari:
- Huu ni mwendelezo wa hadithi tamu ya Zindiko iliyojaa visa na mikasa ya kimaisha kutoka mtunzi mahiri wa riwaya SULTAN TAMBA. Twende naye...
PUNDE mlango ukafunguliwa, wanawake wawili wakatoka ndani. Mama Zimataa – mke wa Mzee Zimataa - akaacha kutwanga dawa, akawafuata wanawake hao. Nyuma yao Mzee Zimataa alikuwa akitoka pia. Mkononi alikuwa ameshika ungo uliojaa majani kadhaa ya dawa na mtungi mdogo.
Zimataa akamwangalia mkewe ambaye naye alisimama katika hali ya kusubiri maelekezo, maana hata wale kinadada wawili hawakuondoka, walikuwa wamesimama hapohapo ikiashiria kwamba kuna maelekezo ya ziada.
“Mke wangu, kawaogeshe zile dawa zao nilizokupa. Dawa nyingine ndio ziko humu nakwenda Zindikoni, wanisubiri, nitawaletea. Nazipeleka kwanza.”
“Sawa mume wangu.”
Mama Zimataa akawapokea wanawake hao na kusogea nao pembeni, akawakaribisha wengine waingie ndani, kwa sababu Zimataa anapoondoka, yeye huendelea na kazi ya kuwasikiliza wagonjwa wake.
Zimataa akaondoka na mtungi wake.
Mama Zimataa akarudi haraka ndani kuwasikiliza wateja hao. Miaka ishirini ya kumsaidia mumewe, ilitosha kumfanya ajue dawa nyingi na shida nyingi zinazowakuta watu wanaokuja pale na utatuzi wake.
Kwa mganga huwa ni tofauti na hospitalini. Kwa sababu mtu anayekwenda hospitalini kumuona daktari, mara zote huwa anaumwa sehemu fulani ya mwili wake. Pengine kichwa na sehemu zake, kifua, tumbo, mikono ama miguu. Lakini kwa mganga ni tofauti. Sio kila mtu anayekwenda kwa mganga huwa anaumwa mwili. Wengine wanaumwa akili, wengine wana changamoto mbalimbali za maisha, wengine wana shida ambazo inawezekana hata haziwahusu wao. Labda ni ndugu zao, jirani zao au kuna mambo fulani wanayataka yawatokee kwenye maisha yao. Kwa maana hiyo tiba za mambo haya wakati mwingine ni ufahamu tu wa saikolojia ya mtu mwenyewe.
Hilo ndilo lililomsaidia mama Zimataa katika kutibu wanaokuja pale kwa niaba ya mume wake. Mtu anayekwenda kwa mganga, kama haumwi chochote huwa na imani ya kurogwa, kwa hiyo ni rahisi kutumia saikolojia hiyo kumtibia kuanzia kwenye akili yake na kufanikisha kwa dawa iliyo ndani ya uwezo wao. Kwa hiyo mama Zimataa alikuwa ni msaada mzuri sana kwa mumewe.
Geti la jengo la Zindiko huwa liko wazi saa zote! Halifungwi na halijawahi kufungwa! Mazingira haya yalikuwa kama mtego kwa yeyote mwenye tamaa ya kulisogelea jengo hili kwa sababu situ geti kuwa wazi, ila hata uzio uliozunguka jengo lenyewe ni mfupi!
Mfupi kiasi cha mtu anayeamua kuingia kwa kuuruka hawezi kutumia nguvu wala akili nyingi. Ni rahisi tu.
Na ndiyo mtego huo uliopoteza maisha ya wengi!
Waliothubutu kuruka au kupitia getini walishtukia wanatazamana na joka la zindiko linalotoka kwenye mtungi ulio kwenye kona ya nyumba. Huwa ni kitendo cha kufumba na kufumbua kwa sababu Joka la Zindiko lina nguvu za umeme! Umeme wa gridi ya taifa!
Unapokanyaga ndani ya uzio wa jengo hilo, ni kama umewasha swichi ya taa! Ukiwasha na taa inawaka. Ukikanyaga, joka limefika mbele yako hata usijue limetoka saa ngapi kwenye mtungi hadi kukufikia. Kwa hiyo hakuna mtu mwenye historia ya kupona kwa waliojaribu kuvuka uzio huo.
Kasoro huyu!
Mzee Zimataa!
Hata sasa, alipita kwenye geti hili akiwa na ungo wake ulio na majani ya dawa na mtungi.
Aliingia kwenye uzio huo na kulifuata jengo kwa mwendo wa nidhamu! Mwendo wa mtu anayeliheshimu eneo hili! Eneo lililomchagua yeye kuwa mtu pekee wa kuingia hapo!
Mzee Zimataa akafika mbele ya mtungi, akainama kidogo, akauelekeza mtungi juu ya mdomo wa mtungi, akazungumza kwa nidhamu pia.
“Kwa idhini yako Joka la Zindiko, kwa nguvu za Jiwe Jekundu zilizokuleta hapa, naleta dawa hizi za wagonjwa saba waliokuja jana. Nataka baraka zako.”
Baada ya kusema maneno hayo ambayo ameyakariri kwa miaka yote ishirini ya kazi hiyo, akarudi kinyumenyume na kusubiri baraka za Joka la Zindiko.
Kilichotokea ni kilekile kinachotokea siku zote.
Mtungi ulitingishika kidogo! Kisha Joka kubwa likatoka kwenye mtungi na kutambaa chini likimzunguka!
Kadiri lilivyotoka na kuongezeka urefu, lakini halikumalizika kutoka!
Na ndivyo lilivyo!
Tangu Mzee Zimataa aanze ile kazi, hajawahi kuliona Joka la Zindiko likitoka lote na kumalizika kiasi cha kujua urefu wake kamili ni kiasi gani!
Hiyo haijawahi kutokea!
Hakuna ajuaye urefu wa Joka la Zindiko kwa sababu linapokuwa linatoka kwenye mtungi halimaliziki. Huendelea kutoka hata kwa urefu wa kiasi gani, lakini daima hubakia ndani ya mtungi kwa sehemu yake ya mwili iliyobakia.
Mzee Zimataa alikuwa amelizoea jambo hili.
Akatulia kimya wakati joka likimzunguka.
Kisha baada ya muda mchache, joka lilirudi kinyumenyume mtungini na kumalizika! Likatoweka! Ikawa kama hakuna chochote! Joka limerudi mtungini.
Mzee Zimataa akageuka na kuondoka zake!
Kazi yake imekwisha!
Kazi ya kuzithibitisha dawa zake alizooteshwa na zindiko kwa wagonjwa aliowakusudia ikawa imekamilika. Kazi hiyo ambayo ameifanya kwa miaka yote ya kazi yake hiyo, ilikuwa imemjengea heshima kubwa na kuogopwa pia.
Kimsingi, pale kijijini na miji mingine ya jirani na ya mbali walikosikia sifa zake, hakuna mtu ambaye alikuwa hamfahamu.
Kwa kijijini kwao pekee, watu karibu wote walishapata huduma kutoka kwake! Iwe moja kwa moja au familia zao. Wote walishaguswa naye! Dawa ambazo huwa anazithibitisha hapo, zilikuwa na nguvu thabiti na ziliweza kutibu ugonjwa wowote. Si ugonjwa tu, shida zote za binadamu waliokwenda kwake zilikwisha!
Kwa upande mwingine Zimataa alikuwa ni mtu mwaminifu sana, kwa sababu hajawahi hata siku moja kumpa mgonjwa dawa ambayo hajaipeleka pale na ikathibitishwa. Hata kama ugonjwa wa mtu aliyekuja, au jambo analotaka kusaidiwa naye analijua na pengine aliwahi kumtibia mtu mwingine au watu wengine, lakini bado aliweka nidhamu ya kuhakikisha dawa hizo zinakwenda kuthibitishwa na joka la zindiko, pale kwenye jengo la zindiko!
Na ndicho kilichosaidia sana katika kumwongezea nguvu na uaminifu kwa kila mgonjwa au mtu mwenye jambo lake aliyekuwa amekwenda kwake.
* * * * * * *
Katika mida hii ya mchana, Zaka na rafiki yake Kazumba walikuwa kazini kwao! Kazi ya udalali!
Muda huu walikuwa wakishuhudia tukio la utiaji saini mkataba wa mpangaji na mwenye nyumba! Walishuhudia kwa sababu mpangaji huyu walikuwa wamemleta wao kwenye hiyo nyumba.
Na hiyo ndiyo ilikuwa kawaida yao, mteja anaposaini mkataba lazima watakuwepo wote au mmoja wao kuthibitisha. Jambo hilo huwa linaenda sambamba na wao kupata bakshishi yao kwa kazi waliyoifanya!
Kwamba licha ya kwamba Zaka na Kazumba hufanya kazi za mheshimiwa mbunge, lakini pia huwa wanafanya kazi zao mtaani kwa kupangisha watu mbalimbali – na kuwatafutia wateja wenye nyumba ambao wanakuwa na nyumba za kupangisha.
Baada ya mpangaji kumaliza kuweka saini na kumkabidhi karatasi ya mkataba mwenye nyumba, kazi ikawa imekamilika!
Zaka akatabasamu!
Kisha mama mwenye nyumba, mwanamke mnene wa sheria yake akakusanya makaratasi yake na wote wakainuka. Mwenye nyumba akampa mkono Zaka. Kisha mpangaji pia wanapeana naye mikono.
Zaka akawa mwenye furaha. “Hii nyumba ni nzuri. Kamwe huwa siwatafutii wateja wangu nyumba zisizoeleweka. Utaishi hapa hadi utakapochoka mwenyewe. Mwenye nyumba ukishamlipa tu hana shida na wewe.”
Mpangaji akatabasamu na kukubali kwa kichwa. Mwenye nyumba pia akatabasamu na kukubali kwa ishara.
Inaendelea...