Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Dr Cheni Gara B? Yule mwanafunzi wangu tu

Muktasari:

  • Kwa sasa mbali na uigizaji wa filamu alikofanya vizuri, pia anajihusisha na U-MC (Mshereheshaji) na anakiri huko anapata pesa nyingi zaidi kuliko filamu.

KUNA asiyemjua Dr. Cheni? Inawezakana ila ni wachache sana hasa watoto wa kuania mwaka 2000.

Nyota huyu wa filamu nchini ‘Bongo Movie’, aliwahi kutamba kwenye maigizo akiwa na Kaole Sanaa Group na tamthilia za kundi hilo zilirushwa kwenye kituo cha runinga ITV. Unakumbuka?

Kwa sasa mbali na uigizaji wa filamu alikofanya vizuri, pia anajihusisha na U-MC (Mshereheshaji) na anakiri huko anapata pesa nyingi zaidi kuliko filamu.

Anasema ni kazi hiyo imezidi kumwongezea umaarufu na ni mmoja wa ma mc wanaokubalika kutokana na umahiri wake katika kazi hiyo.

Mwanaspoti lilifika Sinza Makaburini ilipo ofisi yake na kufanya naye mahojiano na haya ndiyo aliyofunguka.


Wengi wanajua ana bifu na MC Gara B, lakini unajua anasemaje kuhusu MC huyu?

Dr Cheni: Nani kasema nina bifu na MC Gara B? Hivi unaweza kumfanyia bifu mwanafunzi wako? Yule kapita mikononi mwangu. Nimemwelekeza jinsi ya kufanya kazi ya u-MC, sasa leo hii niwe na bifu naye, la nini?

Watu wanazungumza tu maneno. Nimeanza kumjua Gara B miaka saba iliyopita, tatizo anapenda sana kuwapangia ma- MC namna ya kuvaa katika kazi zao.

Mimi asinipangie mavazi ya kuvaa. Huwezi kumpangia mtu avae, Mbona Mrisho Mpoto havai viatu na hakupangiwa na mtu, mie naenda pale kuendasha program ya harusi na sio kuonyesha mavazi.


Changamoto kwenye kazi yake ya u-MC zikoje na anazikabili vipi?

Dr Cheni: Kuna kazi moja sitaisahau. Bwana harusi alifuma meseji kwenye simu ya mke wake wakiwa kwenye gari wakiwa wametoka kufunga ndoa.

Yaani shughuli ilitakiwa kuisha hapo hapo na waligoma kuingia ukumbini.

Mwanamke aliachwa kwenye gari ya maharusi, ikabidi watu wa karibu kuingilia kati.

Mimi nilipopata habari hihiyo, kwenye ukumbi ndani ilibidi nitumie akili na kuwaambia waalikuwa gauni  la bibi harusi limeleta shida.

Ilikuwa changamoto sana kwani mwanzo nilisema gari limeharibika baadae gauni. Watu hawakujua chochote ukumbuni. Hata hivyo, sasa wako poa na wana watoto watatu.


Anasemaje kuhusu kufunga ndoa ya pili?

Dr Cheni: Sijawahi kuoa mke wa pili ingwa dini yangu inaniruhusu. Wala sina mtoto nje ya ndoa. Ninachoshukuru mke wangu ni mvumilivu sana kwani anasikia habari nyingi lakini hadi leo nipo naye na tuna miaka 17 na watoto watatu.


Kwa nini haonekani kwenye tamthilia?

Dr Cheni: Sasa mimi utanionaje wakati mimi ni projuza? Kipindi kile watu walikuwa wananiona kwa sababu nilikuwa msanii.

Kwa hiyo huwezi kuniona kwenye filamu ya mtu tu ilimradi umeniona. Wapo wanaonihitaji lakini kiukweli bado sijaamua.

Kuna wakati nitaamua kucheza filamu za wengine lakini kwa sasahivi waniache kidogo.


Kipi kinalipa zaidi, u-mc au filamu?

Dr Cheni: Kwenye u-MC ni asilimia mia. Filamu kwa sasa ni hadi upate fursa ya kuonekana kwenye TV.

Kama huwezi kupata fursa huwezi kupata kituo chochote cha Tv na utaendelea kukaa benchi hadi upate nafasi.

Ndio maana hapa kati nilipata fursa Azam tukaonyesha uwezo wetu na mkataba wetu  umeisha. Tunajipanga, tutarudi kivingine na itakuwa zaidi ya tamthiliya ya Mtaa wa kazamoyo.

Siyo kwamba u-MC unalipa sana, ila watu wanaoana kila siku, hivyo, napata fursa sana za namna hiyo.


Anatengaje muda kwenye kazi ya u-mc na filamu?

Dr. Cheni: Ni rahisi kwa sababu filamu unaweza kushuti hata asubuhi hadi saa moja jioni naingia kwenye u-mc hadi saa sita usiku unamaliza unarudi nyumbani, hivyo muda unapatikana.


Aliingiaje kwenye U-MC?

Dr Cheni: Kilichonifanya niwe MC ni ile hali ya kualikwa tu kwenye sherehe, lakini baadaye niligundua kuna kitu ma-MC wanashindwa kuwapa Watanzania kwenye sherehe zao, ndiyo nikaamua kuingia kwa miguu yote.


Sikia mipango yake ijayo

Dr Cheni: Nimeona ni bora nifungue chaneli yangu, hasa kwenye TV. Kama TCRA wataturuhusu nitaiita Cheni TV.

Hata hivyo, itaanzia kwenye simu kwani sasa hivi tayari tunayo YouTube Channel.

Nataka watuy waipate kwa urahisi kwenye simu ingawa ikiwezekana iwe kwenye TV.

Kuna watu wengi wana vipaji, wanafanya sinema, tamthilia na wana uwezo lakini hawapati nafasi kwenye TV, ndiyo maana nataka niwape fursa kila mwenye uwezo wa kuandika stori au wa kufanya hizo kazi, nitawasaidia hasa kwenye uzalishaji (prodaction).

Wengi wanafeli kwenye uzalishaji kwa kukosa vifaa. Yaani mtu ana stori na wasanii, lakini hana vifaa kwani ni gharama kununua au kukodisha na wengi hawawezi kuimudu.

Hivyo akija nitampa vifaa akafanyie kazi na tutaingia makubaliano, lengo ni kuwasaidia maana sisi tumesaidiwa na wao wasaidiwe.


Hii imekaaje kwa wasanii aliowatoa kisanaa?

Dr Cheni: Kuna  wasanii wengi wa filamu waliopita mikononi mwangu. Nasema hivi nieleweke, siko kwa ajili ya kujigamba au kutaka sifa, ila furaha yangu ni kumwona aliyepitia kwangu anafanya vizuri. Amenitaja au hajanitaja, kwangu siyo ishu kubwa.

Usitegemee kulipwa fadhila, mtu kama atakumbuka kurudisha fadhila sawa asipokumbuka ni sawa pia.

Wengi wamepitia mikononi mwangu na sasa wanajulikana na wengine hawajulikani.

Mfano Mkuu wa Wilaya Rorya, Juma Chikoka ‘Chopa Mchopanga’, mimi ndiye nimemleta kwenye sanaa. Nilimpokea na kumfanyia ‘interview’ lakini  huwezi kumsikia akisema hili kama nimemtoa.

Kuna Rashid Mwinshehe ‘Kingwendu’ hakuna mtu aliyekuwa anamtaka kwenye sanaa.

Alikuwa sokoni Kariakoo na mimi ndiye nilimchukua na kumfanyia interview  na sasa anafanya kazi nzuri, lakini huwezi kumsikia hata siku moja akisema Dr Cheni amenitoa.

Wapo wengi, Dida wa Mchops, Blandina Chagula ‘Johari’ huwa hawasemi, hata marehemu Steven Kanumba.

Ila Lulu peke yake ndiye anayekumbuka kulipa fadhila kwa kukiri kusema nimemtoa kwenye sanaa, yaani yupo wazi  hata asipokupa fedha, lakini akakumbuka kukushukuru, hiyo ni fadhila kubwa.


Anamfahamu vipi  Lulu

Lulu ana uwezo mkubwa kwenye sanaa, pia ana heshima. Hata tulivyomshika kumtoa, nilimchukua akiwa na miaka miwili au mitatu,  nilikuwa namwona anafika mbali.

Lulu tangu akiwa mdogo alikuwa anapenda U-Modo, anajipenda na msafi, ndiyo maana hata fani zake unaona kwenye nguo kama hivyo ana maduka ya nguo, kila ukimwona Lulu amependeza.

Sema tu kwa sasa kwa umri aliofikia wa kuwa na familia yake na watoto  huwa sipendelei sana kuzungumzia habari zake za nyuma juu ya sakata la marehemu Steven Kanumba.

Kikubwa nilishapambana kwa upande wangu imetosha, sina tatizo naye na bado tunawasiliana kama kawaida.


Sanaa imempa faida gani?

Dr Cheni: Sanaa ndio imenitambulisha na kunifikisha hapa. Hivyo hata biashara zangu ninazozianzisha zinakuwa nyepesi kwa sababu watu tayari wanamjua Cheni.

Nina Kampuni yangu inaitwa Cheni Arts Creation Company limited. Kuna vitu vingi nafanya kama kuuza vitu online, kama mtu ana shida ya kitu China tuna mawasiliano mazuri huko, hivyo anakipata kupitia kwetu.

Tunafanya matangazo, kama una biashara yako tunakutembelea tunaipeleka mjini, inaitwa Cheni mtembezi. Pia tuna ‘video prodaction’ inaitwa ‘Sherehe yako’. Tunashuti maharusi na kupiga picha na tunatengeneza kadi za kidigital.


Changamoto gani kapitia kwenye sanaa

Dr Cheni: Sijawahi kupata changamoto katika safari yangu ya sanaa, kwani kila ninachokutana nacho nachukulia ni fursa na kuzifanyia kazi.


Ni kweli Simba ikifungwa anakosa raha?

Dr Cheni:  Mimi ni Mnyama lia lia na nakosa raha Simba inapofungwa na hata sasa nina wakati mgumu kwani Simba ina mwenendo dhaifu katika Ligi Kuu Bara.

 Mohamed Hussen ‘Tshabalala’ na Kibu Denis pamoja na wachezaji vijana wananivutia zaidi kikosini.


Ana mpango wa kuachana na filamu?

Dr Cheni: Nafanya filamu kwa sababu napenda tu na ipo kwenye damu, lakini siyo kwamba kazi ya filamu ndiyo inaendesha maisha yangu.

Kihalisia unapotoa filamu nzuri, unaweza kuweka lengo la kupata hata Sh3 bilioni, lakini inabaki kuwa makisio tu.

Nina mambo mengi ya kufanya ambayo huniingizia kipato ili kuendesha maisha yangu, lakini sitaacha filamu kwani naipenda.