Diddy anapenda warembo, watoto ila sio ndoa

UKIACHANA na mfululizo wa tuhuma zinazomkabili hivi karibuni, tangu alipopata umaarufu miaka ya 1990 kupitia muziki, Sean Combs ‘Diddy’ amekuwa na uhusiano na mastaa kadhaa maarufu akiwemo Jennifer Lopez na Cassie.
Hadi sasa Diddy ana watoto sita ambao ni Justin, Christian, Chance, pacha D’Lila na Jessie na Love kutoka kwa wanawake wanne tofauti, huku akiwa amemwasili mtoto mmoja, Quincy kutoka kwa aliyekuwa mpenzi wake Kim Porter.
Licha ya kuwa na watoto wote hao na kuweka hadharani uhusiano wake na wanawake nane, Diddy ambaye alilelewa na mama pekee baada ya Baba yake kuuawa mwaka 1972, hajawahi kuoa hadi umri wake wa miaka 54 sasa.
Mwanzilishi huyo wa Bad Boy Records ambaye amekuwa akikabiliana na tuhuma za unyanyaji wa kingono kutoka watu mbalimbali, madai ambayo ameyakana, kwa miaka zaidi ya 30 chini ya umaarufu wake amekuwa na uhusiano wa wazi na wanawake wafuatao.
1. MISA HYLTON
Mapema miaka ya 1990 akichipukia kwenye tasnia ya muziki, Diddy alianzisha uhusiano na Misa Hylton, huku akimsaidia mbunifu huyo wa mitindo katika kazi yake na polepole penzi likachipuka.
Machi 2023 Hylton aliiambia BET kuwa walianza kuwa karibu wakati huo ambao Diddy alikuwa anafanya kazi uptown Records ya kusimamia kazi za wasanii wa lebo hiyo pamoja na chapa zao.
Walijaliwa mtoto mtoto wao wa kwanza na wa pekee, Justin hapo Desemba 30, 1993 ingawa waliachana muda mfupi baada ya kuzaliwa kijana huyo wa miaka 30 kwa sasa. Hata hivyo, Diddy na Hylton waliendelea na ukaribu kwa ajili ya malezi ya mtoto wao kwa miaka yote.
2. KIM PORTER
Hadi sasa huu ndio uhusiano wa Rapa huyo uliodumu kwa muda mrefu zaidi, mnamo Aprili 1, 1998 Diddy na Kim Porter walipata mtoto wao wa kwanza pamoja, Christian ila waliachana mwaka mmoja baada ya kuzaliwa kwake.
Uhusiano huu ulikumbwa na drama nyingi, kubwa ni pale Porter alipogundua Diddy alikuwa anatarajia mtoto na rafiki yake Sarah Chapman, huku akiwa na ujauzito wa pacha wao, D’Lila na Jessie waliozaliwa Desemba 2006.
Mnamo Julai 2007, Porter alitangaza kuachana na Diddy kwa mara ya mwisho ingawa wawili hao walibaki kuwa marafiki wa karibu hadi kifo cha Porter mwaka 2018 kutokana na ugonjwa wa Pneumonia.
3. JENNIFER LOPEZ
Uhusiano huu ulianza mnamo 1999 na wawili hao walikuwa pamoja kwa miaka miwili kabla ya kutengana 2001, katika mahojiano na Vibe 2003, Jennifer Lopez alitaja usaliti kama moja wapo ya sababu ya kuachana na Diddy.
Hata hivyo, kwa kipindi kifupi walichokuwa pamoja, uhusiano wa Diddy na Lopez ulikuwa na misukosuko mingi, waliwahi kushtakiwa kwa kosa la kumiliki silaha na mali za wizi.
Walihudhuria pamoja tuzo za Grammy 2000 ambapo Lopez alivaa mavazi yake maarufu ya Versace. Diddy aliiambia Entertainment Tonight mwaka 2017 kuwa mtoko huo ulibadili mengi katika ulimwengu wa mitindo.
4. SARAH CHAPMAN
Diddy na Chapman ambaye ni mfanyabiashara walikuwa marafiki kwa miaka mingi, uhusiano wao ulianza kipindi Diddy yupo na Kim Porter, huku mwaka 2006 wakipata mtoto wa kike, Chance.
Licha ya mwanzo mbaya wa safari ya malezi kama wazazi, Diddy ameendelea kuwa karibu na Chapman ili kumlea Chance na mara kadhaa amekuwa akiandika shukrani zake kwa mrembo huyo kwa kuwa mama bora.
Katika siku yake ya kuzaliwa mnamo Septemba 2023, Diddy kupitia ukurasa wake wa Instagram alitoa ujumbe kwa Chapman uliosomeka, “Asante Mungu kwa ajili yako kila siku! Tunashukuru sana kuwa na wewe katika maisha yetu! Nakupenda.”
5. CASSIE
Baada ya kuachana na Kim Porter, Diddy aliingia kwenye uhusiano na mwimbaji Cassie hapo mwaka 2007, karibu muongo mmoja wa penzi lao, walikuwa wakiachana na kurudiana na mara ya mwisho walibwagana rasmi mwaka 2018.
Mnamo Novemba 2023, Cassie alimshutumu Diddy kwa kumbaka na kumdhulumu kingono wakati wa uhusiano wao, Cassie alidai alikutana na Diddy kwa mara ya kwanza akiwa na umri wa miaka 19 na alikuwa amemsaini Bad Boy Records.
Ingawa Diddy alikanusha madai hayo, walisuluhisha suala hilo nje ya mahakama, Diddy alisema wameamua kutatua suala hilo kwa amani na kumtakia kila la heri Cassie na familia yake.
“Nimeamua kutatua suala hili kwa amani, nataka kuwashukuru familia yangu, mashabiki na wanasheria wangu kwa msaada wao madhubuti,” alisema Cassie ambaye jina lake halisi ni Cassandra Ventura.
6. LORI HARVEY
Mnamo Julai 2019 ulizuka uvumi kuwa Diddy na Lori Harvey ni wapenzi baada ya kuonekana pamoja huko SoHo, New York City, mwezi mmoja baadaye wakaonekana tena katika mapumziko Italia.
Hata hivyo, miezi michache baadaye, yaani Oktoba 2019, ilionekana wawili hao walikuwa wametengana huku Harvey akiacha kumfuata (unfollow) Diddy kwenye mitandao ikiwa ni siku chache kufuatia Rapa huyo kuonekana na mwanamke mwingine.
Mnamo Januari 2023, Harvey alipoulizwa na Mtangazaji, Adrienne Bailon wa E! kuhusu madai kwamba alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na Diddy na mtoto wake Justin, alikanusha madai hayo na kusema hayana ukweli wowote!.
7. YUNG MIAMI
Taarifa za uhusiano wa Diddy na Yung Miami zilianza kuvuja tangu mwaka 2021 lakini walithibitisha hilo mnamo Juni 2022 wakati Diddy alipoonekana kwenye Podcast ya Rapa huyo wa City Girls.
“Tuna uhusiano, tunatoka pamoja, sisi ni marafiki na tunaenda maeneo mbalimbali mapya, kusema kweli tuna nyakati nzuri za kuwa pamoja,” alisema Diddy katika Podcast hiyo alipoulizwa na Yung Miami wao ni kina nani?.
Hata hivyo, miezi michache baadaye, mnamo Septemba 2022, Yung Miami akiongea na Jarida la XXL alidai kuwa yupo ‘single’ na bado yupo na Diddy ambaye naye yupo ‘single’, alisema ipo hivyo maana bado hawajaoana!.
8. DANA TRAN
Ingawa Diddy hajawahi kuthibitisha uhusiano wake na Dana Tran, ambaye ni mtaalamu wa usalama wa mtandao na mwanamitindo, wawili hao walimjaliwa mtoto wao wa kwanza, Love mnamo Oktoba 2022.
“Nimebarikiwa sana kumkaribisha mtoto wangu wa kike Love Sean Combs duniani. Mama Combs, Quincy, Justin, Christian, Chance, D’Lila, Jessie na mimi mwenyewe tunakupenda sana! Mungu ndiye Mkuu!” Diddy aliandika X (Twitter) baada ya kuzaliwa Love.